Rais mstaafu Kenya Daniel Arap Moi atibiwa hospitalini

Rais Mstaafu Daniel arap Moi

Chanzo cha picha, ALEXANDER JOE

Rais wa zamani nchini Kenya Daniel Torotich Arap Moi amefikishwa hospitalini kufanyiwa ukaguzi wa afya yake kwa mara ya pili katika muda wa wiki mbili, vyombo vya habari nchini Kenya vinaarifu.

Katika taarifa rasmi hivi punde msemaji wa kiongozi huyo mstaafu Lee Njiru ameeleza kwamba Mzee Moi yupo hospitali anahudumiwa na kikosi cha wataalamu wa afya wanaoongozwa na daktari wake binafsi Dkt David Silverstein.

Ameongeza kwamba "yupo macho na anafahamu kinachoendelea."

Awali gazeti la Daily Nation kwa kunukuu duru kutoka familia ya kiongozi huyo wa zamani limeeleza kuwa Moi alikimbizwa hospitalini siku ya Jumapili baada ya kupata "matatizo ya kupumua."

Hata hiyvyo, jamaa mwingine kutoka familia ya Moi ameikana taarifa hiyo, linaripoti gazeti hilo.

Familia hiyo imeeleza katika taarifa yake, kutofurahishwa na habari ambazo imezitaja kuwa 'mbaya na za kuzusha mshtuko' zinazosambazwa.

Gazeti jingine nchini, The Star, limeripoti kwamba Moi "yuko katika hali mahututi":

Kuingia na kutoka hospitalini

Si mara ya kwanza taarifa za kiongozi huyo wa zamani kuugua kusambaa katika vyombo vya habari nchini.

Mwishoni mwa mwaka jana palikuwa na taarifa pia Daniel Moi alifikishwa hospitalini kufanyiwa uchunguzi kama ilivyo kwa wakati huu.Kwa mara nyingine alinukuliwa msemaji wake Lee Njiru aliyesema kwenye vyombo vya habari nchini "Mzee aliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya matabibu wakiongozwa na daktari wake Dkt David Silverstein, kuridhika na afya yake baada ya uchunguzi," wakati huo.

Mnamo Machi tena mwaka jana kiongozi huyo mstaafu alipelekwa katika hospitali ya Ichilov huko Tel Aviv, nchini Israel ambako taarifa zilieleza alikwenda kufanyiwa uchunguzi.

Baada ya kulazwa kwa muda aliruhusiwa kurudi nchini ambapo ilibainika baadaye kwamba alikwenda kufanyiwa uchunguzi wa goti lake lililokuwa linamsumbua," kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi yake iliotumwa kwa vyombo tofauti vya habari.

Chanzo cha picha, Raila Odinga

Maelezo ya picha,

Rais wa zamani nchini Kenya Daniel Moi na kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipotembelewa na kiongozi huyo Aprili 2008

Raila Odinga ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliofika huko Kabarak, ambako ndio makao makuu anayoishi kiongozi huyo wa zamani, ili kumtakia afya njema baada ya kulazwa hospitalini nchini Israel kwa takriban mwezi mmoja.

Daniel Moi alizaliwa mnamo September mwaka 1924 katika eneo la milimani huko Baringo eneo la Bonde la ufa kaskazini mwa Kenya.

Aliinukia kutoka kuwa kijana aliyekuwa mchungaji mifugo , na kuwa mwalimu katika shule ya kimisionari na baadaye kushikilia usukani wa taifa kama rais wa pili Kenya alipomrithi Jomo Kenyatta.

Chini ya utawala wa rais Kenyatta, Moi alikuwa makamu wake wa rais.

Alipokea wadhifa huo mkuu mnamo 1978 Agosti wakati Kenyatta alipofariki.

Aliiongoza Kenya kwa takriban miaka 24 kati ya 1978 hadi 2002.

Moi alikuwa kiongozi pia wa chama tawala wakati huo nchini Kenya KANU, kilichofanikiwa kupata ushindi katika uchaguzi za miaka kadhaa nchini.

KANU kiilipoteza usukani mnamo 2002, wakati Mwai Kibaki akiwa na muungano wa kisiasa, National Rainbow Coalition alipochaguliwa kuwa rais wa Kenya.

Tazama pia:

Maelezo ya video,

Ni ipi nguvu ya upinzani katika mataifa ya Afrika?