Binaadamu wote walio hai leo, walitoka kusini mwa mto Zambezi Botswana

Pan de Makgadikgadi, Botswana, Afrique

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Ardhi imekauka katika eneo hilo leo

Wanasayansi wamelitaja eneo la kusini mwa mto Zambezi kuwa ndiko binaadamu wote walio hai hii leo wanatokea.

Eneo hilo sasa limegubikwa kwa chumvi lakini kwa wakati mmoja lilikuwa ni ziwa kubwa, ambalo huenda likawa ndio chimbuko letu wanadamu tangu miaka 200,000 iliyopita.

Wazee waliotangulia waliishi huko kwa miaka 70,000, hadi hali ya hewa ya huko ilipobadilika, watafiti wanapendekeza.

Walianza kusogea wakati ardhi yenye rutuba ilipozidi kugunduliwa, na kuchangia uhamiaji wa vizazi viilivyofuata kutoka Afrika.

"Limekuwa wazi kwa muda fulani sasa kwamba kimaumbile, binaadamu wa leo waliokuwepo Afrika kwa kadiria miaka 200,000 iliopita," anasema Prof Vanessa Hayes, mtaalamu wa masuala ya jeni kutoka chuo cha utafiti Garvan Institute of Medical Research nchini Australia.

"Kile ambacho kimejadiliwa kwa muda mrefu ni eneo maalum la wapi walikozuka na kufuatia na kutawanyika kwa mababu waliotangulia."

Hatahivyo, kauli ya mwisho la Profesa Hayes limevutia shaka kutoka kwa watafiti wengine kwenye nyanja hiyo.

Ngome kuu ziwani

Eneo linalotajwa ni kusini mwa mto Zambezi kaskazini mwa Botswana.

Watafiti wanadhani mababu zetu, walitua karibu na mfumo mkubwa Afrika wa ziwa , Ziwa Makgadikgadi, ambalo sasa ni eneo lililo na chumvi nyingi.

"Ni eneo kubwa mno, huenda lingekuwa na maji maji sana, na ardhi yenye kuvutia," anasema Prof Hayes. "Na huenda lingekuwa eneo zuri la kuishi kwa binaadamu wa leo na pia wanyama."

Baada ya kuishi hapo kwa miaka 70,000, watu walianza kuondoka. Mabadiliko katika namna mvua inavyonyesha katika eneo hilo yalichangia mawimbi matatu ya uhamisho miaka 130,000 na 110,000 iliopita, yaliochangiwa kwa kufunguka kwa ardhi zaidi yenye rutuba.

Chanzo cha picha, Chris Bennett, Evolving Picture, Sydney, Australia

Maelezo ya picha,

Prof Hayes anajifunza namna ya kuwasha moto na wawindaji wa Jul'hoansi katika eneo la Kalahari Namibia

Wahamiajiwa kwanza walielekea kaskazini mashariki, na kufuatwa kwa wimbi la pili la wahamiaji waliosafiri kueleka kusini magharibi na idadi ya tatu ya watu walisalia katika eneo hilo mpaka hii leo.

Taswira hii imetokana na kuangalia nyuma muundo wa familia za binaadamu kwa kutumia mamia ya sampuli za chembechembe za DNA zinazotoka kwa kizazi cha mama kutoka kwa Waafrika walio hai.

Kwa kuchanganya elimu ya Jeni na jiolojia na kwa kuiga kwa kutumia kompyuta na hali ya hewa, watafiti walifanikiwa kutoa tasiwra ya namna bara la afrika lilivyokuwa miaka 200,000 iliopita.

Kuijenga upya hadithi ya binaadamu

Hatahivyo, utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Nature, umetazamwa kwa uangalifu na mtaalamu mmoja, anayesema huwezi kuunda upya hadithi ya chimbuko la binaadamu kutokana na DNA pekee.

Uchambuzi au tathmini nyingine imetoa majibu tofuati kwa kutumia ugunduzi wa mabaki ya kiumbehai kuashiria chimbuko lao limetokea Afrika mashariki.

Profesa Chris Stringer wa jumba la kitaifa la ukumbusho wa historia mjini London, ambaye hahusiki na utafiti huu amesema mageuzi ya binaadamu wa kale Homo sapiens ulikuwa ni mfumo mgumu.

"Huwezi kutumia usambazaji wa DNA mitochondrial peke yake kutambua eneo moja la chimbuko la binaadamu wa leo," ameiambia BBC.

"Nadhani inapita kiwango cha data kwasababu unatazama sehemu moja tu ya muundo huo kwahivyo hauwezi kukupa taarifa kamili ya chimbuko letu."

Hivyo basi, huenda kukawa na machimbuko mengi au maeneo walilkotoka binaadamu wa leo kuliko hilo moja, ambayo yangali kutambuliwa.

Hatua zilizopigwa katika mageuzi ya binaadamu kihistoria

  • Miaka 400,000 iliyopita: Neanderthal - binamu zetu - waanza kuonekana na kusogea Ulaya na Asia.
  • Miaka 300,000 hadi 200,000 iliyopita:Homo sapiens - binaadamu wa leo - waonekana Afrika.
  • Miaka 50,000 hadi 40,000 iliyopita: Binaadamu wa leo wafika Ulaya.