Mzozo wa karo watikisa Chuo Kikuu cha Makerere licha ya Museveni kuagiza wanajeshi waondoke chuoni

Chuo kikuu cha Makerere Uganda

Chanzo cha picha, Makerere University

Maelezo ya picha,

Chuo kikuu cha Makerere Uganda

Polisi nchini Uganda wamefyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wanafunzi wa chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda waliokuwa wamekusanyika katika eneo la Freedom Square.

Wahadhiri wa Chuo hicho pia wametawanywa na wanafunzi wakalazimishwa kuondoka katika vyumba vya madarasa. Ghasia hizi zimetokea siku moja tu baada ya rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni kuwaagiza wanajeshi kuondoka katika chuo hicho, baada ya ripoti kuwa waliwapiga wanafunzi katika chuo hicho

Unaweza pia kusoma:

Picha za Televisheni ya NTV Uganda zilizotumwa kwenye mtandao wa twitter zinaonyesha polisi wa kutuliza ghasia wakiwasili katika chuo hicho.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu hicho maarufu wamekuwa wakiandamana kupinga Ongezeko la 15% ya karo. lililoidhinishwa na baraza la Vyuo vikuu nchini Uganda tangu wiki iliyopita.

Bwana Museveni amewataka wadau wote katika Chuo Kiku cha Makerere kufanya mazungumzo ili kutatua mzozo wowote uliopo kuhusu karo.

Unaweza pia kusoma:

Utawala wa Chuo Kikuu na viongozi wa wanafunzi walikutana Jumatatu kujadili suala hilo , lakini wakashindwa kufikia makubaliano, jambo lililofanya mkutano wao kuahirishwa. Uongozi wa vyuo vikuu nchini Uganda unadai kuwa nyongeza ya sasa ni ndogo ikilinganishwa na inayotozwa na vyuo vingine vikuu nchini humo:

Ghasia hizi zinatokea saa kadhaa tu baada ya bodi ya utawala ya wa chuo hicho, Baraza la vyuo vikuu kuahidi kuwa vimesitisha sera ya asilimia 15 ya karo kufuatia maandamano ya wanafunzi yaliyoanza wiki iliyopita.

Vyombo vya habari nchini humo vinasema kuwa tangu Jumanne, kumekuwa na ripoti za wanajeshi na polisi wa kutuliza ghasia kuingia ndani ya vyumba au makazi ya wanafunzi usiku na kuwapiga.

Polisi yadai huenda maandamano yana uchochezi wa kisiasa

Wakati huo huo polisi nchini Uganda inachunguza ripoti kuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere wanalipwa na wanasiasa na wanaharakati kufanya maandamano.

Msemaji wa polisi Fred Enanga amesema kuwa taarifa walizonazo ni kwamba malipo kwa wanafunzi hao yanatolewa kwa njia ya simu za mkononi, na kwamba taarifa hiyo ni moja ya taarifa zinazochunguzwa kuwa chanzo kilichochochea maandamano katika chuo cha Makerere : ''Tayari tumeweza kupata moja ya vituo vya huduma ya kupokea na kutoa pesa kwa njia ya simu katika eneo la Wandageya, ambako wanatoa pesa kwa ajili ya maandamano'' alisema Enanga, na kuongeza kuwa watoaji wa huduma za pesa kwa njia ya simu wanachunguzwa ili kufahamu chanzo cha udhamini wa pesa hizo.

Unaweza pia kusikiliza

Maelezo ya sauti,

Mwanafunzi aunda mabomu ya machozi Uganda