Ghana: Mtoto wa miaka 12 adahiliwa Chuo Kikuu

Viemens Bamfo

Chanzo cha picha, Viemens Bamfo

Maelezo ya picha,

Viemens Bamfo ni mtoto mdogo zaidi kati ya wanafunzi 3000 waliodahiliwa

Mtoto wa miaka 12 ameshinda nafasi ya kusoma chuo kikuu masomo ya utawala wa Umma.

Viemens Bamfo, ni mtoto mdogo zaidi kati ya wanafunzi 3000 waliodahiliwa katika chuo kikuu cha Ghana.

Alishinda mtihani wa majaribio kwa alama za juu baada ya kufundishwa na baba yake Robert Bamfo nyumbani.

Ameiambia BBC kuwa anatamani kuwa na kazi ya juu kabisa nchini Ghana.

''Ninataka kuwa raisi wa Ghana, ninataka kupeperusha bendera ya Ghana na kuifanya Ghana kuwa nchi huru ya kweli kama ilivyo Marekani, Uingereza, China na nchi nyingine.''

Ana matumaini ya kusoma sheria ya katiba, mifumo ya kisiasa, masuala ya uongozi, uchumi na utunza fedha.

Bwana Bamfo, ambaye ana shahada ya kwanza ya uhandisi wa kemikali, amesema mafanikio ya mtoto wake si jambo la kushtukiza.

''Nimewekeza muda na nguvu nyingi kumuwezesha kuweza kukabiliana na changamoto na fursa zinazoambatana nazo.Hivyo sikushtushwa.''

Alieleza siri ya mafanikio katika malezi ya mwanae:

''Awali nilimfundisha mwanangu asikubali kutafsiriwa mtu wa wastani, na kuwa anapaswa kuwa wa tofauti kwa kuweka bidii na amejiandaa kupambana kufikia lengo hilo.''