Maandamano Iraq, Misri na Lebanon: Je muamko wa mageuzi umeanza kutokota mashariki ya kati?

Waandamanji wamekuwa kila mahali katika eneo la mashariki ya kati ikiwemo Iraq

Chanzo cha picha, AFP

Huku msimu wa joto unapomalizika katika eneo la Mashariki ya Kati, je eneo hilo linakaribia mwamko mpya wa mageuzi?

Nchini Iraq, waandamanaji wanapigwa risasi hadi kufa. Nchini Lebanon, waandamanaji wamesitisha operesheni za serikali na wanaonekana kuwa tayari kuipindua serikali ya waziri mkuu Saad al - Hariri.

Katika majuma ya hivi karibuni, jeshi la serikali ya Misri lilivuruga jaribio la maandamano dhidi ya serikali ya kiimla ya rais Abdul fattah al-Sisi. Iraq, Lebanon na Misri zina tofauti nyingi.

Lakini waandamanaji wana malalamiko yanayofanana yanayowakumba mamilioni ya watu, hususan vijana , katika eneo zima la mashariki ya kati. Takriban asilimia 60 ya idadi ya watu wa eneo hilo iko chini ya umri wa miaka 30.

Idadi ya vijana inaweza kuwa kitu muhimu kwa taifa iwapo uchumi, mfumo wa elimu na taaisi za serikali zinafanya kazi vizuri kuweza kufikia mahitaji yao, lakini hilo halifanyiki miongoni mwa baadhi ya wakaazi.

Vijana nchini Lebanon , Iraq na kwengineko mara nyingi hukasirishwa na wanayopitia swala linalosababisha ghasia.

Ufisadi ulioenea

Malalamishi makuu ni dhidi ya ufisadi na ukosefu wa ajira. Jambo moja linalosababisha jingine.

Iraq imeorodheshwa kama mojawapo ya mataifa fisadi zaidi duniani, kulingana na takwimu kadhaa za ufisadi duniani.

Lebanon pia imeorodheshwa lakini haina ufisadi mwingi vile. Ufisadi ni kama saratani. Unakula matumaini ya wale wanaokuwa waathiriwa wake.

Wanaoathiriwa katika mfumo wenye ufisadi wanaweza kukasirika sana , na haraka sana iwapo hata wale waliosoma hawawezi kupata kazi huku wakiona watu wachache wakifaidika.

Wakati taasisi za serikali, kama vile mahakama na Polisi zinaposhirikishwa, ni ishara kwamba mfumo wote unaanguka.

Katika mataifa yote mawili ya Lebanon na Iraq, waandamanaji wanataka serikali zao kujiuzulu. Pia wanataka mfumo wote wa serikali kufanyiwa mabadiliko.

Moto wa kuotea mbali

Ukweli kuhusu janga la Iraq ni kwamba ghasia zimejikita katika jamii.

Wakati waandamanaji , wanaopiga kelele za ukosefu wa ajira, ufisadi na serikali , walipokwenda barabarani haikuchukua muda kwani risasi zilitumika dhidi yao.

Waandamanaji katika barabara za Iraq, kufikia sasa hawana viongozi.

Lakini hofu katika serikali ni kwamba kila muda unapoyoyoma na idadi ya waathiriwa kuzidi zinaweza kujiandaa vyema zaidi.

Chanzo cha picha, EPA

Waandamanaji wamezilenga ngome za serikali hususan ukuta wa kijani mjini Baghdad.

Ulikuwa kituo kikuu cha Marekani na sasa ni eneo ambalo afisi za serikali na mabalozi zimetapakaa.

Usiku kucha katika mji mtakatifu wa Karbala kulikuwa na ripoti ambazo hazijathibitishwa za mauaji ya raia wengi wakati wandamanaji walipofyetuliwa risasi.

Kanda ya video imechapishwa katika mitandao ya kijamii kuonyesha watu wakitoroka risasi.

Tangu maandamano hayo yalipoanza , kiwango cha walioathirika kimeongezeka.

Ripoti kutoka Baghdad zinasema kwamba baadhi ya wanajeshi wa Iraq wameonekana wakivalia bendera ya taifa katika mabega yao , wakiwaunga mkono waandamanaji.

Lakini ripoti pia zinasema kwamba watu waliovalia nguo nyeusi , wengine wakifunika nyuso zao wamekuwa wakifyatua risasi .

Baadhi ya madai ni kwamba huenda wanatoka kutoka kwa wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran.

Ni hali isioisha

Maandamano yalianza nchini Lebanon tarehe 17 mwezi Oktoba baada ya serikali kujaribu kuweka kodi kwa tumbaku, mafuta ya Petroli na simu za WhatsApp.

Kodi hizo mpya zilifutiliwa mbali haraka lakini walichelewa.

Ili kuanza, maandamano ya Lebanon, yalijaa vichekesho. Lakini hofu imeanza kutanda nchini humo kufuatia ghasia.

Hivyobasi tunauliza je ni muamko wa mapinduzi katika eneo la mashariki ya kati?

Zaidi ya yote ni ishara kwamba yalioanza mwaka 2011 hayajakamilika.

Chanzo cha picha, Reuters

Muamko wa mapinduzi ya mwaka huo hayakutoa uhuru uliopiganiwa na wengi dhidi ya viongozi wa kiimla.

Lakini athari zake bado zinaendelea kuwaathiri, ikiwemo vita nchini Syria, Yemen, Libya mbali na serikali inayoongozwa kiimla nchini Misri.

Na sababu zilizopelekea muamko wa mwaka 2011 bado zipo na katika visa vingine zimeongezeka.

Kufeli kwa serikali za kifisadi kufikia mahitaji ya vijana walio wengi ni hakikisho la wazi kwamba hasira na chuki inayowashinikza waandamanaji haitomalizika.