Abu Bakr al-Baghdadi: Marekani yatoa picha za kwanza jinsi ilivyotekeleza uvamizi wake

Abu Bakr al-Baghdadi: Marekani yatoa picha za kwanza jinsi ilivyotekeleza uvamizi wake

Kanda ya video imeonesha wanajeshi wakiwafyatulia risasi wanamgambo ardhini wakati walipokuwa wakikaribia nyumba ya Abu Bakr al- Baghdadi ambapo kabla ya kuingia ndani ya nyumba hiyo.

Baghdadi alitorokea katika handaki na kujilipua. Baada ya uvamizi huo nyumba hiyo iliharibiwa na silaha kali.

Mkuu wa kitengo cha ulinzi Jenerali Kenneth Mckenzie , alisema kwamba jumba hilo lililoharibiwa lilikuwa kama eneo la kuegesha magari likiwa na mashimo mengi.

Jenerali McKenzie alisema kwamba watoto wawili walifariki na Baghdadi katika handaki hilo na sio watatu kama ilivyoripotiwa awali.

Hatahivyo hakuweza kuelezea maelezo ya rais Trump kwamba Baghdadi alikua akipiga kelele na kulia wakati alipokuwa akikaribia mauti yake.

''Alitambaa hadi katika handaki moja na watoto wawili wadogo na kujilipua huku wapiganaji wake wakisalia ardhini. Unweza kuelewa ni mtu wa aina gani kupitia kitendo hicho'' , aliambia mkutano na wanahabari.

''Hayo ndio maelezo yangu ya kile alichokifanya. Sina uwezo wa kuthibitisha kitu chengine chochote kuhusu dakika zake za mwisho''. Siwezi kuthibtisha hilo kwa njia moja ama nyengine''.

Jenerali Mckenzie alisema kwamba wanawake wanne - ambao walikuwa wakivalia fulana zilizojaa vilipuzi na mwanamume mmoja waliuawa ndani ya uwa la nyumba hiyo.

Alisema kwamba idadi kadhaa ya wapiganaji isiojulikana pia walifariki baada ya kuzifyatulia risasi ndege za Marekani.

Aliongezea: Nataka kuweka wazi kwamba licha ya shinikizo kali na kiwango cha juu cha shambulizi hilo kila juhudi zilifanywa ili kuzuia kuwaua raia wasio na hatia na kuwalinda watoto tulioshuku huenda walikuwa katika nyumba hiyo.

Jenerali Mckenzie alithibitisha kwamba kiongozi huyo alitambuliwa kupitia vinasaba vya DNA , akiongezea kwamba sampuli zake zilikuwa katika faili tangu Baghdadi alivyohudumia kifungo katika jela moja ya Iraq 2004

Alisema kwamba mabaki ya Baghdadi yalipelekwa katika kambi moja ya kuyatambua na baadaye yakazikwa baharini katika kipindi cha saa 24 baada ya kifo chake kulingana na sheria ya mizozo.