Uganda: Wakataa kutumia choo kwa kuwa kimefungwa kamera

Mamlaka zinasema hatua hiyo ni katika kulinda usalama

Chanzo cha picha, AFP

Wakazi wa mji wa Tororo mashariki mwa Uganda, wamekataa kutumia choo cha umma kilichotengenezwa kwa ufadhili wa Benki ya dunia katika kituo cha mabasi kwa madai ya kufungwa kamera za usalama, Gazeti la Daily Monitor nchini Uganda limeripoti.

Watu wanasema ''kufuatilia watu wazima wanaokwenda ''kupata haja msalani'' ni kinyume cha utamaduni wao.

Lakini karani wa mji huo, Paul Omoko, amenukuliwa akisema kuwa kamera zinachukua picha za watu mlangoni na si ndani ya vyoo.

Amesema nia ni kuimarisha usalama kwa sababu ''magaidi wanapenda kutega mabomu kwenye vyoo vya umma''.

Mkuu wa wilaya Nickson Owole amesema ''wale wanaojaribu kuikana teknolojia hii huenda wana ajenda ya siri''.

Choo cha umma kilifadhiliwa na benki ya dunia chini ya mradi wa maendeleo ya miundombinu ya Manispaa nchini Uganda.

Wakazi walisema kuwa hawattumia choo hicho mpaka kamera zitakapoondolewa.

''Wanaweza kuelekeza kamera kwenye maeneo mengine ya kituo lakini si maeneo ya choo,'' alisema dereva mmoja, Mohamed Mwima.

''Kwa sisi waafrika, inafedhehesha kwa mtu kuona utupu wa mwingine. Viongozi wetu wanapaswa kuwajulisha watu wanaotoa misaada kabla ya kuweka kamera,'' alisema Sadick Hirya, dereva mwingine.