Tanzania: Mnada wa korosho waanza,wakulima wamenufaika?

Mnada wa kosrosho waanza

Mnada wa kwanza wa msimu wa korosho mwaka huu umeanza leo Alhamisi.

Mnada huo unafanyika mkoani Mtwara, kusini mwa Tanzania, mkoa ambao ni mmoja kati ya mikoa inayolima zao hilo nchini Tanzania.

Msimu wa mwaka huu unaanza wakati sekta hiyo haijaondokana na changamoto za mwaka uliopita.

Hata hivyo kuna mabadiliko makubwa kwenye mnada wa mwaka huu. Si kama miaka iliyopita, serikali haijaweka bei elekezi.

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA

Mwaka jana, Raisi wa Tanzania John Magufuli aliwazuia wafanyabiashara kununua korosho kutoka kwa wakulima, baada ya kukataa kununua mazao hayo kwa bei elekezi iliyowekwa.

Magufuli aliamuru ongezeko la bei ya korosho kwa 94%, akidai kuwa wakulima wamekuwa wakinyonywa na wafanya biashara.

Alichukua hatua ya kununua mazao yote na kulipeleka jeshi kubeba korosho kutoka kwa wakulima.

Baada ya raisi Magufuli kuingilia kati suala hili, bei ya korosho ilipanda kwenye soko la dunia.

Wakulima wanasema nini?

Wakulima wanasema kuwa bei za korosho zinazopangwa na wafanyabiashara hazikidhi gharama za uzalishaji kwa kuwa upatikanaji wa pembejeo ni mgumu, hivyo zao lao haliwalipi.

''Hatujaweza kupata mtetezi wa moja kwa moja na hatua zinazochukuliwa na serikali zinaishia njiani na utekelezaji unakuwa mdogo, hatujajua Raisi anakwama wapi au katika mapambano haya yuko peke yake''. Anaeleza mkulima wa korosho mkoani Mtwara Hamisi Athumani Minjale maarufu Jaba.

''Tunaingia kwenye msimu mpya kwa hali ngumu kwa kuwa wakulima wengi hawajalipwa, ukiingia kwenye ghala yangu nina zaidi ya tani 19 bado ninahitaji pesa za kuendesha shughuli za kilimo, hivyo biashara hii tunaifanya kigumugumu''. Anaeleza Minjale.

Kwa mujibu wa soko la bidhaa hiyo nchini Uingereza, bei ilipanda kwa 10% mpaka dola 3.8 za marekani kwa kilo, kutokana na masuala ya usafirishaji wa korosho kutoka Tanzania.

Mwezi Juni Waziri wa fedha na mipango, Dokta Philip Mpango aliliambia bunge kuwa mauzo ya korosho kwa ujumla katika soko la kimataifa yalishuka kwa zaidi ya 60%.

Mwezi uliopita,Waziri wa kilimo Japhet Asunga, aliviambia vyombo vya habari kuwa Tanzania inatarajia kuongeza uzalishaji wa korosho kwa 33.5% msimu huu.

Asunga alisema tani 300,000 za korosho zinatarajiwa kuzalishwa, kutoka tani 225,000 za msimu wa mwaka 2018/2019.

Tanzania ni mfanyabiashara muhimu katika soko la korosho duniani. Zao la korosho huzalishwa kwa wingi nchini Tanzania, likifuatiwa na chai, kahawa na katani.