Fatou Jallow: Malkia wa urembo 'aliyebakwa' na Yahya Jammeh nchini Gambia atoa ushahidi

Fatou Jallow anasema kuwa alitoroka The Gambia baada ya kubakwa na sasa anaishi nchini Canada

Chanzo cha picha, FATOU JALLOW

Malkia wa urembo nchini Gambia amemshutumu rais wa zamani wa taifa hilo Yahya Jammeh kwa 'kumbaka' baada ya kukataa kufunga naye ndoa.

Akitoa ushahidi kwa tume ya maridhiano na ukarabati , Fatou Jallow alisema kwamba rais Jammeh alimnyanyasa kingono katika chumba kimoja ili kumuadhibu.

Tume hiyo ilibuniwa ili kuchunguza madai ya unyanyasaji dhidi ya Jammeh wakati wa kipindi chake cha utawala wa miaka 22.

Ushahidi wa bi Jallow ulikamilisha kikao cha wiki tatu kilichoangazia udhalilishaji wa kingono.

Bwana Jammeh alitoroka Gambia 2017 baada ya kukataa kustaafu kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi wa urais.

Kwa sasa anaishi mafichoni nchini Guinea ya Ikweta.

Ushahidi wake ni miongoni mwa ripoti ya shirika la haki za kibinadamu la Human Rights Watch ambayo inaelezea madai mengine ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono uliotekelezwa na bwana Jammeh.

BBC ilijaribu kuwasiliana na bwana Jemmeh ambaye kwa sasa anaishi mafichoni Equitorila Guinea , kuhusu madai hayo.

Awali msemaji wa chama chake cha APPR alikana madai hayo yaliyotolewa dhidi ya bwana Jammeh.

''Sisi kama chama na raia wa Gambia tumechoka na msururu wa madai ambayo yameripotiwa dhidi ya rais wa zamani'', alisema Ousman Rambo Jatta katika taarifa iliotumwa kwa BBC.

Chanzo cha picha, Getty Images

"Rais huyo wa zamani hana muda wa kujibu uongo na kampeni za kumuharibia jina. Ni mtu anayemuogopa mungu ambaye anaheshimu sana wanawake wa Gambia'', alisema naibu wa kiongozi wa chama hicho cha APPR.

Awali Bi Jallow aliiambia BBC alitaka kukutana na bwana Jammeh mwenye umri wa miaka 54 mahakamani ili ashtakiwe.

''Nimejaribu sana kuficha na kufutilia mbali habari hiyo na kuhakikisha kuwa haitakuwa moyoni mwangu. Kwa kweli sikuweza , hivyobasi nikaamua kuzungumza kwa sababu ni wakati wa kusema ukweli na kuhakikisha kuwa Yahya Jammeh anasikia kile alichokitenda.

Tume hiyo ya maridhiano na marekebisho inachunguza ukiukaji wa haki za kibinaadamu wakati wa utawala wa miaka 22 wa bwana Jammeh , ikiwemo ripoti za mauaji ya kiholela , ukatili na kukamatwa na kuzuiliwa kiholela.

Alilazimishwa kutoka madarakani mnamo mwezi Januari 2017 baada ya mataifa jirani kutuma vikosi vya kijeshi alipokatalia madaraka.

Alikataa kuolewa na Jammeh

Bi Jallow alisema kuwa alikuwa na umri wa miaka 18 wakati alipokutana na Jammeh baada ya kushinda shindano la malkia wa urembo wa 2014 katika mji mkuu wa Banjul.

Miezi kadhaa baada ya kupata taji hilo, anasema kwamba rais huyo wa zamani alijifanya kama mzazi wakati alipokutana naye akimpatia ushauri, zawadi na fedha na kuandaa maji kupelekwa katika nyumba yao ya familia.

Na katika chakula cha jioni kilichoandaliwa na msaidizi wa rais huyo , anasema alimuuliza iwapo wangeoana.

Alikataa wazo hilo mbali na zawadi alizokuwa akipatiwa.

Bi Jallow anasema kuwa msaidizi huyo baadaye alisisitiza kwamba anafaa kuhudhuria sherehe ya kidini katika ikulu ya rais kama malkia wa urembo mnamo mwezi Juni 2015.

Lakini alipowasili , alipelekwa katika makazi binafsi ya rais huyo.

''Ilikuwa wazi kile ambacho kingetokea'', alisema akitaja hasira ya bwana Jammeh baada ya yeye kukataa kufunga naye ndoa.

Bi Jallow anasema alipigwa kofi na kudungwa sindano katika mkono wake.

''Alifuta sehemu zake za siri katika uso wangu, akanisukuma nipige magoti na kunifanyia vibaya''

Wasichana wa itifaki

Msichana huyo baadaye alisema kuwa alijifungia nyumbani kwao kwa siku tatu na kuamua kutorokea Senegal.

Alipokuwa mjini Dakar mji mkuu wa Senegal , Bi Jallow alitafuta usaidizi wa mashirika kadhaa ya haki za kibinadaamu.

Wiki chache baadaye alipatiwa ulinzi na kupelekwa nchini Canada ambapo amekuwa akiishi tangu wakati huo.

Chanzo cha picha, AFP

Shirika la Human Rights Watch (HRW) na Trial International yanasema kuwa bwana Jammeh alikuwa na mfumo wa kunyanyasa wanawake , ambapo wanawake wengine walikua wakilipwa mshahara na serikali na kufanya kazi katika ikulu kwa jina 'wasichana wa itifaki'', ambao walikuwa wakifanya kazi za ukarani lakini umuhimu wao mkubwa ulikuwa kushiriki ngono na rais.

BBC haikuweza kubaini madai hayo, lakini afisa mmoja wa zamani nchini humo ambaye alikubali kuzungumza bila jina lake kufichuliwa alisema kuwa anajua kuhusu mambo mabaya yaliokuwa yakitendeka katika ofisi ya rais: Maafisa wa itifaki walikuwa wanawake na waliajiriwa ili kuridhisha mahitaji ya rais.

Anakumbuka kumuona bi Jallow katika ikulu mara nyingine wakati wa usiku.

Mwanamke mwengine ambaye aliajiriwa kama afisa wa itifaki akiwa na umri wa miaka 23 alilazimishwa 'kushiriki' ngono na bwana Jammeh mwaka 2015.

Mwanamke huyo ambaye aliomba kutofichuliwa jina , alisema kuwa siku moja rais huyo alimwita chumbani mwake: Alianza kunivua nguo na kusema kuwa alikuwa ananipenda, angenifanyia chochote ningetaka na familia yangu, na kwamba nisiambie mtu yeyote na iwapo nitakiuka hilo nitakiona cha mtema kuni.

''Nilihisi sina chaguo. Siku hiyo alilala nami bila kutumia kinga yoyote''.

'Wanawake wengine walihisi heshima'

Mwanamke mwengine ambaye alifanya kazi kama afisa wa itifaki alisema kuwa alijuwa kwamba iwapo mmoja wao angeitwa ingekuwa kwa sababu ya kushiriki ngono.

Wengine walitaka. walihisi kuheshimiwa ama walitaka pesa, aliambia shirika la haki za kibinadamu la HRW akificha jina lake.

Chanzo cha picha, AFP

Alielezea vile alivyonyanyaswa kingono na rais huyo nyumbani kwake huko Kanilai, 2013 wakati alipokuwa na umri wa miaka 22: "Jioni moja msaidizi mmoja wa rais aliniita na kuandamana naye katika nyumba ya kibinafsi ya rais .

''Alinitaka kuvua nguo. aliniambia kwamba mimi ni msichana mdogo niliyehitaji ulinzi na alitaka kunipaka maji ya kiroho''.

Katika kisa kingine siku iliofuata, alianza kulia wakati bwana Jammeh alipoanza kumshika mwili wake.

Alikasirika na kumfukuza.

Anasema kwamba baadaye alifutwa kazi huku ahadi ya kupata ufadhili wa masomo ikifutiliwa mbali.

Rais Barrow amesema kuwa atasubiri ripoti hiyo ya tume ya maridhiano kabla ya kuamua iwapo atamrudisha bwana Jammeh nyumbani kutoka mafichoni nchini Guinea ya Ikweta