Zaidi ya watu 270,000 wakimbia makazi yao kutokana na mafuriko Somalia

Mafuriko yameharibu zaidi ya theluthi nne ya mji wa Beledweyne Haki miliki ya picha nrc.smugmug.com

Zaidi ya watu 270,000 wameyahama makazi yao kutokana na mafuriko makubwa kuikumba Somalia.

Mafuriko hayo yaliyotokea baada ya kingo za mto Shabelle kupasuka.

Waathirika wa mafuriko hayo yametokea kwa watu ambao awali waliyahama makazi yao na kuanza kuishi chini ya miti kwa kuwa mafuriko yalisomba tenti zao.

Wakati mvua zaidi na mafuriko vikitarajiwa, Baraza la wakimbizi la Norway (NRC) imetoa wito kutoa msaada kwa ajili ya maelfu ya watu wanaoishi katika eneo ambalo tayari limeathiriwa na mzozo na usalama duni.

''Mafuriko yameharibu zaidi ya theluthi nne ya mji wa Beledweyne na vijiji vya karibu vikiwa vimefurika maji. Haya ni maeneo masikini ya sehemu ya Somalia, ambayo kwa sasa hakuna umeme, maji safi na salama ya kunywa, mifugo imepotea na mazao ya yameharibiwa. Timu yetu inahofia familia karibu 30,000 kuwa zimehama makazi kutokana na mafuriko katika eneo la Bardaale, kusini mwa Somalia. Jamii hizi zinahitaji msaada wa haraka ,'' amesema Mkurugenzi wa NRC nchini Somalia, Victor Moses.

Athari kwa wakazi

Kwa mujibu wa Shirika la wakimbizi duniani na Baraza la kuhudumia wakimbizi la Norway, NRC watu 273,000 wamekosa makazi kutokana na mafuriko mwezi Oktoba pekee, wengi katika kijiji cha Baladweeyne wameathirika zaidi kutokana na kufurika kwa mto wa Shabelle.

Haki miliki ya picha nrc.smugmug.com

Idadi kamili ya watu walioyahama makazi yao kutokana na ukame, mafuriko na mzozo mpaka sasa mwaka huu nchini Somalia imefikia watu 575,000.

''Nchi tayari imeharibiwa na ukame, ambao umechangia maelfu ya watu kuyaacha makazi yao mwaka huu. Jamii zilizoathirika zimekuwa tegemezi zaidi kwa misaada ya kibinaadamu na inakuwa vigumu kurejea katika hali zao za kawaida,'' Moses ameeleza.

Watoto, wanawake na wazee wanakabiliwa na njaa kali, wako hatarini kupata athari za kiafya katika maeneo waliopo, misaada ya kibinaadamu haiwafikii kutokana na ukosefu wa usalama na mizozo, kwa mujibu wa shirika la NRC, wanahitaji sana chakula, maji, malazi , huduma za kiafya, vyoo na vyandarua.

Haki miliki ya picha nrc.smugmug.com

''Hifadhi ya chakula imeharibiwa, watoto, wakinamama na watu wazima wako kwenye hatari ya kukumbwa na baa la njaa na magonjwa.

Magonjwa kama kipindupindu yanaweza kulipuka na kusambaa haraka''.Aliongeza Moses

Zaidi ya yote, mvua kubwa imetabiriwa kunyesha nchini Somalia pia kukitarajiwa mafuriko zaidi katika kipindi cha majuma kadhaa yajayo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii