BBC yabaini biashara ya utumwa dhidi ya Wanawake mtandaoni nchini Kuwait

Maelfu ya wanawake wanapatikana mtandaoni tayari kuuzwa

Unapoendesha gari kuzunguka mitaa ya Kuwait hutawaona wanawake hawa. Wako mafichoni, wakinyimwa haki zao za msingi, hawawezi kuondoka na wako hatarini kuuzwa kwa mtu atakayekuwa tayari kutoa dau la juu.

Lakini ukitazama kwenye simu unaweza kuona maelfu ya picha zao, wakiwa wamegawanywa kwenye makundi kutokana na rangi zao, na wengine wanapatikana kwa kiasi kidogo cha dola

Uchunguzi uliofanywa na BBC idhaa ya kiarabu ulibaini kuwa wafanyakazi wa majumbani wananunuliwa kinyume cha sheria na kuuzwa kwa njia ya mtandao, soko linaloonekana kwa kutumia app kama 'Google play na Apple App Store' na 'algorithm na hashtag' kupitia Facebook na Instagram.

Soko la utumwa

''Wanachofanya ni kutangaza soko la watumwa mtandaoni,'' anasema Urmila Bhoola, mwandishi maalumu wa UN kuhusu aina za utumwa. '' Ikiwa Google, Apple, Facebook au kampuni nyingine yoyote wanayofanya kazi hii mitandaoni wanapaswa kuwajibishwa.''

Makazi tisa kati ya kumi nchini Kuwaiti zina wafanyakazi wa majumbani- wanatoka katika maeneo masikini ya dunia, mbao wamefika nchini humo kwa ajili ya kupata fedha na kusaidia familia zao huko wanakotoka.

Wakiwa wamejifanya wenza waliwasili kuwait, timu hiyo ya wachunguzi kutoka BBC idhaa ya kiarabu walizungumza na watumiaji 57 wa app na kuwatembelea zaidi ya dazeni, watu waliokuwa wakijaribu kuwauza wafanyakazi wao wa nyumbani kwa kutumia app maarufu '4sale'.

Wauzaji walikuwa wakizizuia pasi za kusafiria za wanawake na walikuwa wakiwapa nafasi mara chache kuzungumza na simu au wengine walikuwa hawapati nafasi hiyo kabisa.

App ya 4Sale iliruhusu wateja kuwachagua watu kwa rangi zao, kukiwa na bei ya kila mmoja pembeni ya picha yake.

Timu ya uchunguzi ya BBC imekuwa ikisikia maoni kama vile ''raia wa India ni wachafu,'' wakiwaelezea wanawake.

Haki za binaadamu zilikiukwa

Wachunguzi hao walitakiwa na watumiaji wa app, ambao walijitambulisha kama 'wamiliki' wa wanawake hao, kuwanyima haki za msingi za binadamu, kama vile kuwapa ''siku,au dakika au sekunde'' ya mapumziko.

Mwanaume mmoja, polisi, alisikika akisema: ''Niamini ni mzuri sana, anapenda kucheka ana sura ya furaha.Hata ukimfanyisha kazi mpaka saa 11 alfajiri hatalalamika.''

Aliiambia BBC namna wafanyakazi wa majumbani wanavyotumiwa kama bidhaa. ''utamuona mtu akimnunua kwa dola 2000, na kuwauza wa dola 33,000.''

Aliwadokeza wanunuaji: ''pasi ya kusaafiria, usimpe. wewe ndiye mfadhili wake. Kwanini umpe pasi ya kusafiria?''

Katika tukio la kushtusha timu ya BBC ikapatiwa msichana, ambaye kwa jina tutamuita 'Fatou', mwenye miaka 16.

Alisafirishwa kutoka Guinea, na alikuwa akifanya kazi za majumbani nchini Kuwait kwa miezi sita, ingawa sheria inasema msichana wa kazi za nyumbani anapaswa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 21.

Muuzaji wake alikuwa hampi muda wa mapumziko Fatou, pasi yake ya kusafiria na simu vilichukuliwa, hakuruhusiwa kutoka kwenye nyumba akiwa peke yake- vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria za Kuwait.

Sheria ya mwaka 2015 ilifanya Kuwait kuwa moja kati ya nchi za ghuba zenye sheria kali ya kulinda wasichana wa majumbani. Lakini sheria hii ilikua haifuatwi na kila mtu.

App kama 4Sale iliwawezesha waajiri kuuza udhamini wa wafanyakazi wao wa majumbani kwa waajiri wengine, ili kupata faida. Hatua hii ilikua inatengeneza mazingira ya kuwepo kwa soko haramu na kusababisha wanawake kukumbwa na visa vya udhalilishaji na unyonyaji.

Biashara hii ya utumwa haifanyiki Kuwait pekee.

Nchini Saudi Arabia uchunguzi ulibaini mamia ya wanawake wakiuzwa kwa Haraj, app maarufu ya kuuza bidhaa. Kulikuwa na mamia zaidi Instagram, inayomilikiwa na Facebook.

''Ni Jehanamu ''

Timu ya BBC ilisafiri mpaka Guinea kujaribu kuwasiliana na familia ya Fatou, mtoto ambaye waligundua alipelekwa kuuzwa nchini Kuwait.

Kila mwaka mamia ya wanawake wanasafirishwa kutoka Guinea kuelekea nchi za kiarabu kama wafanyakazi wa majumbani.

''Kuwait hali ni mbaya ,'' alisema mmoja wa wafanyakazi wa majumbani ambaye anakumbuka alipokuwa akiamriwa kulala sehemu ambayo hulala ng'ombe. ''Nyumba za Kuwait ni mbaya sana,'' anasema mwingine. '' Hakuna kulala, hakuna chakula, hakuna chochote.''

Fatou alipatikana kwa msaada wa mamlaka za Kuwaiti na kupelekwa kwenye makazi yaliyo chini ya serikali yanayowasaidia wafanyakazi wa majumbani.

Siku mbili baadae alirudishwa kwao Guinea.

Aliiambia BBC: ''Walikuwa wakinifokea na kuniita mnyama. Inaumiza, ilinifanya niwe mwenye huzuni, lakini sikuweza kufanya chochote.''

Sasa amerejea shuleni mjini Conakry, aliiambia timu ya BBC iliyomtembelea, ''Nina furaha sana. Hata sasa, nikizungumzia hili nina furaha sana.

Maisha yangu yana nafuu sana. Ninajisikia kama nimerejea kutoka utumwani.''

Hashtag zimeondolewa

Serikali ya Kuwait imesema hivi ni ''vita dhidi ya tabia hii'' na kusisitiza kuwa app hizi zitadhibitiwa vikali''.

Mpaka sasa hakuna hatua iliyochukuliwa kisheria dhidi ya mwanamke aliyejaribu kumuuza Fatou. Muuzaji hakuwa tayari kusema lolote kuhusu ombi la BBC kutoa maoni yake.

Tangu timu ya BBC ilipowasiliana na app na kampuni za teknolojia kuhusu uchunguzi wake, App ya 4Sale imeondoa sehemu ya wafanyakazi wa ndani kwenye ukurasa wa facebook yenye hashtag "خادمات للتنازل#" yaani ''kusasirishawafanyakazi wa ndani''.

Lakini Google na Apple wameiambia BBC kuwa tabia hii haina nafasi kwenye app zao. Na kuwa wanashirikiana na wataalamu wao kuzuia shughuli zinazokwenda kinyume na sheria kufanyika kwenye majukwaa yao.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii