Nini chanzo cha uhaba mkubwa wa maji Nairobi?

Watu wakiwa katika shughuli ya kutafuta maji Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wakenya wengi wanakabiliwa na changamoto ya kupata maji ya bomba

Jiji kuu la Kenya linaloendelea kukua kwa kasi linakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na usambazaji wake, hali inayowafanya watu wengi kupata maji kutoka vyanzo visivyo salama.

Je, tatizo la uhaba wa maji jijini Nairobi ni kubwa kiasi gani ikilinganishwa na miji mingine barani Afrika?

Nahason Muguna, mkuu wa kampuni ya usambazaji maji katika jiji la Nairob, (NCWSC), hivi karibuni alionekana katika televisheni ya kitaifa akielezea hofu yake kuhusu uimarishaji wa huduma maji wakati ambapo idadi ya watu ikiendelea kuongezeka kwa kasi katika miongo michache iliyopita.

Mwaka 1990, zaidi ya 90% ya wakaazi wa maeneo ya mijini nchini Kenya walikuwa wakipata maji safi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Sasa, inakadiriwa kuwa ni 50% ya wakaazi milioni 4.5 wa Nairobi ambao wanaweza kupata maji safi ya bomba.

Wakaazi wengi wanapata maji kutoka kwa wauzaji maji wanaotumia njia zisizo za halali kupata bidhaa hiyo.

Tangu mwaka 2017 maji yamekuwa yakitolewa kwa mgao kwa wakazi wa jiji la Nairobi na viunga vyake.

Maeneo tofauti ya jiji yanapata maji kwa siku tofauti za wiki, kwa siku chache na zingine kwa saa chache.

"Kile ambacho kinaweza kuitatua shida ya maji katika jiji la Nairobi ni kubuni vyanzo vipya cha maji,"anasema Bw. Muguna. "Maji tunayotumia sasa yalitakiwa kuwatosheleza wakaazi wa jiji hadi mwaka 2000 pekee."

Miradi inaendelea ya kupanua kiwango cha mabwawa na kujenga mabomba mapya ya kusafirishia maji hayo. Sehemu ya ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwaka ujao.

Bw. Muguna anasema miradi hiyo ilitarajiwa kukamilishwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita, lakini ilikabiliwa na changamoto ya kifedha.

Taarifa nyengine:

Nairobi inahitaji maji kiasi gani?

Kwa sasa kuna upungufu wa 25% ya usambazaji maji katika makaazi ya Nairobi, kwa mujibu wa kampuni ya maji ya Nairobi, NCWSC.

Kuna musuala yanayoibuka kuhusu kiwango cha maji ya bomba, hasa katika makaazi yasiokuwa rasmi.

Maji taka kutoka mitaro na mashimo ya maji taka yanaweza kupenya na kuingia katika mabomba ya usambazaji maji masafi kutokana na kudhoofika kwa mabomba na kiasi kikubwa cha maji hayo hayawezikunywika, kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO).

Haki miliki ya picha Getty Images

Serikali ina lengo la kufikia kiwango cha kitaifa cha upatikanaji wa maji na kuhakikisha maji hayo yanamfikia kila mtu kufikia mwaka 2030.

Hata hivyo, malengo yaliopita hayakufikiwa, licha ya ahadi kutolewa kuwa upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu kitaifa itafikia 80% mwaka 2015.

Ukadiriaji wa kitaifa wa upatikanaji wa maji safi kwa kila nyumba ulikuwa 57% kufikia mwisho wa mwaka 2018.

Hali iko vipi Nairobi ikilinganishwa na miji mingine?

Utafiti kuhusu usambazaji maji katika miji 15 ya nchi zilizo na mapato ya chini kote duniani ulifanywa na taasisi ya Marekani ya rasilimali ya maji.

Nairobi bila shaka sio moja ya miji iliyo na uhaba mkubwa wa maji ikilinganishwa na miji mingine iliyoangaziwa katika utafiti huo.

Kati ya miji iliyofanyiwa utafiti huo, Kampala na Lagos imebainishwa kuwa na kiwango cha chini cha upatikanaji maji ya mfereji, huku mitaa mingi ya mabanda katika mji mkuu wa Nigeria ikigunduliwa kutokuwa na maji ya bomba.

Utafiti huo pia unasema gharama ya upatikanaji wa maji iko juu katika miji mingi ya nchi zinazoendelea kukua, hali inayochangia sehemu kubwa ya mapato ya wakazi wa miji hiyo kutumiwa kununua maji ya mfereji ama maji ya chupa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii