Mbivu na mbichi za uongozi wa Magufuli katika kipindi cha Miaka minne

magufuli Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais Magufuli aliapishwa kuwa rais wa Tanzania siku kama ya leo miaka minne iliyopita.

Leo rais John Pombe Magufuli ametimiza miaka minne madarakani kama rais wa Tanzania, siku kama hii miaka minne iliyopita aliweza kula kiapo cha kuwatumikia watanzania katika kipindi cha miaka mitano, kama inavyosema katiba ya nchi hiyo.

Kabla ya kuwa rais wa nchi hiyo, Magufuli amehudumu katika nyadhifa mbalimbali nchini humo, alikua waziri wa ujenzi na amepitia na wizara nyingine.

Katika kipindi cha miaka minne amefanya mengi , ya kusifiwa na ya kukoselewa pia.

Magufuli ameonekana kuwa ni kiongozi anayetoa maamuzi ya haraka kwa kutoa marufuku ya jambo au kuwaachisha kazi watendaji katika nyadhifa zao.

"Ametumbuliwa" ni neno ambalo limekuwa maarufu katika vinywa vya wengi baada ya kiongozi huyo kuwafukuza kazi watendaji pale ambapo anaona mambo hayaendi sawa.

Katika utawala wa rais Magufuli, idadi kubwa ya mawaziri, wakurugenzi na watendaji wengine wameachishwa kazi na wengine kubadilishiwa mjukukumu kila kukicha.

Miaka ya nyuma, ilikuwa rahisi kwa wanafunzi kujua majina ya mawaziri wote jambo ambalo ni tofauti na sasa. Leo atakuwa huyu na kesho mwingine.

Kutokana na maamuzi yake ambayo yamekua hayatabiriki, yameweza kuleta mabadiliko makubwa katika taifa hilo.

Licha ya watendaji kuwa na hofu katika utendaji wao lakini huduma za umma kama afya zimeweza kuanza kupatikana kwa urahisi.

Mafanikio yake katika kipindi cha miaka minne.

Rais Magufuli alifanya ziara za kushtukiza na kuibua mengi ambayo yalikuwa yanatendeka ndivyo sivyo.Mfano mara tu alipoingia katika utawala aliweza kutembelea hospitali ya taifa hilo Muhimbili.

Ilikuwa ni jambo la kawaida wagonjwa na kina mama wajawazito kulala chini. Lakini baada ya ziara yake ya kushtukiza amebadilisha hospital hiyo na huduma muhimu kupatikana.

Kati ya mafanikio makubwa ambayo magufuli ameyafanya katika huduma za jamii ni kuhakikisha huduma ya maji inapatikana katika maeneo mengi.

Elimu bure kwa shule za msingi za serikali ni jambo ambalo aliweza kulifanikisha.

Ujenzi wa barabara ni jambo lingine ambalo amelipa kipaumbele kabla na baada ya kuingia madarakani. Wakati alipokuwa waziri wa ujenzi na hata sasa ambapo ni rais. Barabara nyingi zimeongezwa na hata kujenga barabara ya juu yaani fly over.

Unaweza pia kusoma;

Rais Magufuli anasisitiza kutokuwepo safari zisizo na lazima kwa watumishi wa umma na hata yeye mwenyewe hakuonekana akiwa anasafiri kwenda nje ya nchi mara kwa mara. Inawezekana haijawahi kuripotiwa kuwa aliwahi kwenda nchi za magharibi tangu aingie madarakani.

Pamoja na kutoonekana kupenda safari, rais huyo amefanya jitihada za kuboresha sekta ya usafirishaji.

Haki miliki ya picha Empics
Image caption Magufuli akizindua upanuzi wa uwanja wa kisasa wa ndege

Shirika la ndege ambalo lilikuwa limekufa kwa miaka mingi, ameweza kulirejeshea uhai kwa kasi.

Sasa Tanzania ina ndege za aina mbalimbali huku alipoingia kulikua na ndege moja mbayo pia ilikua mbovu.

"Shirika letu la ndege lilikuwa na hali mbaya sana, lilikuwa na ndege moja tu tena ilikuwa inafanyiwa matengenezo mara kwa mara, soko la ATCL lilishuka sana hadi kufikia asilimia 2.5.

Lakini sasa tumenunua ndege 7, na nyingine kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner itakuja mwaka 2020", alisema Rais Magufuli mwaka jana 2018 katika hafla ya kupokea ndege.

Upanuzi wa uwanja wa ndege wa kisasa, hadhi ya kimataifa uliweza kujengwa na umeanza kutumika sasa.

Mradi mwingine mkubwa ambao unaendelea ni wa gari moshi ,Reli ya kisasa inaendelea na ujenzi huku maendeleo ya ujenzi yakionekana kuwa chanya.

Mradi mwingine ambao umekua ukipingwa sana na wahifadhi wa mazingira na mashirika ya kimataifa, ni mradi mkubwa Zaidi wa uzalishaji umeme wa Stigler's Gorge, rais Magufuli alitia saini na kuanza mradi huo mara moja.

Pamoja na hali ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja, na hali ya maisha kuendelea kuwa duni kwa wananchi. Rais Magufuli amefanikiwa kuziba au kukemea mirija ya rushwa kwa kiwango kikubwa.

Wahujumu uchumi au wale walioitwa mafisadi wameweza kufikishwa na kufungwa gerezani. Majina ya watu maarufu matajiri yaliwashangaza wengi walipoishia gerezani.

Malipo ya kodi kutiliwa mkazo na kukamatwa kwa matajiri waliokwepa kodi na kuhujumu nchi bado hakukuleta matumaini kwa wananchi wengi wa kawaida.

Mambo ambayo anakosolewa sana katika kipindi cha miaka minne

Mara nyingine maamuzi ya rais Magufuli yamesababisha kuitwa dikteta.

Vyama vya upinzani vilisitishwa kufanya mikutano ya hadhara na wanasiasa wengi wa upinzani wamedai kunyimwa haki zao za msingi.

Viongozi wa upinzani wanakutwa wana kesi za kujibu kila kukicha mahakamani.

Mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu alidiriki kumuita rais huyo dikteta. Tundu Lissu sasa yuko ughaibuni baada ya kwenda kwa matibabu mara baada ya kupigwa risasi zapata 11.

Image caption visa vya waandishi kupotea na kufungwa vimeongeza katika awamu hii

Vyombo vya habari na wanahabari nchini humo, utendaji umekuwa mgumu kutokana hofu. Waandishi wa habari kadhaa wameripotiwa kupotea kwa kuvamiwa na watu wasiojulikana.Huku wengiwe wakiwa gerezani.

Utaratibu wa ripoti za ikulu au zinazomuhusu rais zimebadilika. Vyombo vya habari mara nyingi vinatumiwa kile ambacho kilirekodiwa na waandishi wa ikulu.

Baadhi ya watu wameshtakiwa kwa kumtusi rais kwenye mitandao ya kijamii.

"Kusikojulikana na watu wasiojulikana"

Ni wimbo kwa watanzania wengi katika utawala wake. Watu hao ambao hawajulikani ni ki nani wameshamiri sana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa rais Magufuli, wamehusishwa na vitendo vya utekwaji na mauaji ya baadhi ya watu.

Kuishi maisha ya chini

Pamoja na uongozi wake kuwa wa kuogopeka lakini ni kiongozi ambaye ni shabiki wa wananchi wengi wa kipato cha chini.

Ameonekana kujishusha na kuwa ngazi ya wananchi wa kawaida kwa kufanya kile ambacho hakuna rais angetegemewa kukifanya.

Rais Magufuli amewahi kwenda barabarani kufagia na kuzoa taka kama moja ya kuhamasisha watu kuwa wasafi.

Rais Magufuli alienda na kikapu feri ili kununua samaki,jambo ambalo si la kawaida kwa rais kufanya. amefanya hivyo ikiwa anasisitiza watu waache kutumia mifuko ya plastiki.

"Hapa kazi tu" ...ni msemo wa rais huyo akiwà anataka wananchi wa taifa hilo wafanye kazi kwa bidii badala ya kulalamika.

Kwenye upande wa burudani, rais Magufuli anapenda kupiga 'push up' katika mikutano ya hadhara kudhihirisha furaha yake.

Rais Magufuli anapenda kupiga ngoma na kucheza.

Inaonekana kuwa anapenda kusifiwa pia. Mwanamuziki mmoja wa muziki wa bongo fleva aliimba wimbo wa kumsifu hivi karibuni, msanii huyo aliamfanya rais kutamka hadharani kuwa "natamani Harmonise awe mbunge".

Kipaumbele kwa eneo alipotokea Magufuli

Magufuli alionyesha wazi kuweka kipaumbele kwa mji aliotokea Geita. Barabara nzuri na uwanja wa ndege umejengwa.

Haki miliki ya picha Storm Fm geita
Image caption Rais wa kenya Uhuru Kenyata akipokelewa na Rais Magufuli mjini Chato

Kwa mara ya kwanza rais wa Tanzania ameweza kumkaribisha rais wa nchi jirani eneo lingine la nchi tofauti na Dar as salaam.

Makazi ya rais Magufuli pia yanastaajabisha kwa kuwa na kanisa ambalo aliruhusu kila mwanakijiji kuabudu hapo.

Katika hotuba zake anamtanguliza Mungu mara nyingi kwa kudai kuwa Mungu amemwagiza kufanya jambo fulani.

Hivi karibuni rais alidai kuwa akifa Leo je miradi aliyoianzisha itaweza kuendelezwa?

Mtazamo kutoka mataifa ya nje juu ya rais Magufuli

Pamoja na kuwa na jitihada nyingi za maendeleo, Asasi za kiraia za kigeni na mataifa ya kigeni yalionekana kuwa mtazamo hasi dhidi yake.

Hii ilitokana na maamuzi yake dhidi ya wanafunzi wanaopata mimba shuleni wasirejee shule.

Pamoja na sera za kupinga mapenzi ya jinsia moja na uzazi wa mpango.

"Wanawake sasa wanaweza kuacha kutumia dawa za kupanga uzazi, Ukiwa na chakula cha kutosha zaa.", tunachotakiwa watanzania, ni kuchapa kazi ili kusudi watoto utakaowazaa uwalishe. Kama huwezi kufanya kazi, hapo ndipo utumie mpango wa uzazi, wale ambao hawafanyi kazi, wavivu ndio wanajipangia watoto"

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanafunzi wanaopata ujauzito wamepigwa marufuku kurudi shuleni nchini humo

Kauli zake zimeonekana kuwa zinaenda kinyume na haki za binadamu. Ingawa hivi karibuni ameonekana kugeuza kauli yake kwa kutoa lawama kwa wanaume wanaowapa mimba watoto shule.

"Serikali inatoa mchango kwa kutoa elimu bure na wanaume bure wanawapa mimba watoto wa shule! Hao wanaume bure 229 ndio viongozi? Kwa sababu kama sio hao viongozi, je viongozi wameshindwa kitu gani kuwapeleka hawa watoto kwenye haki?

"Watoto 229 wamekatiliwa maisha yao katika elimu," alisema Rais Magufuli.

Kuhamia Dodoma

Kati ya malengo ambayo rais huyo aliweka mara tu alipoingia madarakani ni kuhakikisha kuwa mji wa Dodoma unakuwa makao makuu ya Tanzania kiuhalisia. Rais John Pombe Magufuli ametangaza kuhamia rasmi katika mji mkuu wa taifa hilo, Dodoma mwezi Oktoba.

Rais Magufuli anakuwa rais wa kwanza kati ya marais watano waliotawala nchi hiyo , kutekeleza uhamisha wa makao makuu ya Tanzania kutoka jiji la kibiashara la Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Haki miliki ya picha Job De Graaf
Image caption Mji mkuu wa Dodoma

Uhamisho wa makao makuu ya serikali mkoani Dodoma, umechukua safari ya zaidi ya miaka 42 iliyopita.

Mabadiliko ya makao hayo yamekuja huku yakiwawaathiri watumishi kwa kiasi kikubwa kwa upande wa kifamilia zaidi huku mji wa Dodoma kupewa matumaini ya kukua.

Familia kutengana au safari za Dodoma kwenda Dar es salaam na kurudi kuwa nyingi.

Wapinzani wanasema nini kipindi cha miaka minne ya Magufuli?

Wapinzani wamekua wakilalamika sana na kubanwa na uongozi huu, wanaona kuwa wamerudi nyuma sana hasa katika uhuru wa kujieleza na mikutano ya hadhara.

''tumerudi nyuma sana katika suala la utawala bora na demokrasia, pamoja na haki za binaadamu, tunabanwa sana sana'' anasema Tumaini Makene msemaji wa chama cha upinzani cha Chadema.

Kwa upande wa wananchi wa kawaida wao wamegawana upande, wengine wanaona Magufuli amebadilisha mambo mengi ikiwemo usafiri wa barabara.

''napenda kumpongeza sana kwenye suala la miundominu, ujenzi wa barabara standard gauge, ni kipande ambacho ametumika vizuri kwenye wizara ya ujenzi, na hata baadhi ya mitaa kwa hapa Dar es salaam kuwa kuna lami zinaendelea kuwekwa katika baadhi ya mitaa'' anasema juma mkazi wa Dar es salaam.

Kwa upande wa uchumi amefanikiwa sana lakini kwa mimi mwananchi wa kawaida sioni umuhimu wowote ule, maisha yanazidi kuwa magumu tuu'' amesema mwananchi mmoja ambae hakupenda kutaja jina lake.

Mwaka ujao Tanzania inatarajia kuingia katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge, rais Magufuli anatarajiwa kugombea tena kwa awamu ya pili ya miaka mitano mingine. Je vipaumbele vyake vitakua nini katika kipindi kijacho? Ni suala la kusubiri na kuona.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii