Nini chanzo cha msako dhidi ya vyombo vya habari ?

Burundi imeshuhudia msako mkali dhidi ya vyombo vya habari na upinzani tangu mwaka 2015 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Burundi imeshuhudia msako mkali dhidi ya vyombo vya habari na upinzani tangu mwaka 2015

Wanahabari wanne wanaofanya kazi katika vyombo vya habari vya kibinafsi nchini Burundi wameshtakiwa kwa madai ya kuhujumu usalama wa taifa, baada ya kuangazia shambulio la waasi katika mji wa Bubanza ulio kaskazini magharibi mwa nchi hiyo .

Wanahabari hao wa Gazeti la Iwacu na dereva wao wamekuwa wakizuiliwa tangu tarehe 22 Oktoba kwa madai ya kujaribu kuwahoji wakazi wa Bubanza ambao walikuwa wakitoroka mapigano kati ya vikosi vya usalama na waasi.

Burundi imeshuhudia msako mkali dhidi ya vyombo vya habari na upinzani tangu mwaka 2015.

Kutokana na hatua hiyo vyombo vya habari vya kibinafsi na vile vya kimataifa ikiwemo BBC vimefungiwa na baadhi ya wanahabari kukimbilia ughaibuni kwa kuhofia usalama wao.

Maripota wasiokuwa na mipaka, Without Borders (RSF),wameonya kuwa msako wa Burundi unalenga kuvinyamazisha vyombo vyote huru vya habari kufikia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Burundi imeorodheshwa kuwa nchi ya 159 kati ya 180 kwa ukandamizaji wa uhuru wa wanahabari kwa mujibu wa ripoti ya dunia ya RSF ya mwaka 2019.

Kilichotokea

Oktoba 22, wanahabari wanne wa Iwacu waliotumwa kwenda kuangazia makabiliano kati ya wanajeshi wa nchi hiyo na waasi wa Red Tabarawe wenye makao yao DR Congo, mjini Bubanza walikamatwa na kupokonywa vifaa vyao vya kazi kama vile kamera na simu za rununu.

Walizuiliwa bila kufunguliwa mashataka kwa siku nne kabla ya mwendesha mashtaka wa umma wa Bubanza, Clement Ndikuriyo, kutuhumu dereva wao kwa kushirikiana na waasi wa Red Tabara.

Watano hao wameshatakiwa kwa kosa la kukiuka kanuni ya usalama wa kitaifa wa Burundi, kosa ambalo hukumu yake ni kifungo cha miaka 10 jela.

Tarehe 18 Oktoba, Baraza la kitaifa la habari la Burundi, lilitoa agizo kwa wawakilishi wote wa vyombo vya habari nchini humo kusaini mara moja "Kanuni ya maadili kwa waandishi wa habari katika kipindi cha uchaguzi cha 2020".

Mwenyekiti wa baraza hilo Nestor Bankumukunzi, alisema taratibu zitazingatiwa kabla ya wanahabari kuruhusiwa kufanya kazi nchini humo "kitaaluma".

Lakini kuna hofu huenda serikali ikatumia kanuni hiyo kuwalenga wanahabari fulani wakujitegemea na ambao wanachukuliwa kuwa chanzo kikuu cha ghasia katika nchi hiyo ambayo upinzani umenyamazishwa kwanguvu na mamlaka na waasi wanaounga mkono serikali.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii