Rwanda: Kizungumkuti cha msongamano wa wanafunzi kitatuliwe vipi?

Sensa ya hivi karibuni ya Wizara ya elimu imebainisha kwamba shule nyingi zina idadi kubwa ya wanafuzi
Image caption Sensa ya hivi karibuni ya Wizara ya elimu imebainisha kwamba shule nyingi zina idadi kubwa ya wanafuzi

Serikali ya Rwanda imeanza kushughulikia suala la msongamano wa wanafunzi katika shule kadhaa za nchi hiyo.

Katika shule nyingi hasa za mikoani chumba kimoja cha shule kinaweza kuwa na wanafunzi zaidi ya 80, wote wakiwa chini ya usimamizi wa mwalimu mmoja pekee.

Wataalamu wa elimu wanasema kwamba msongamano wa wanafunzi madarasani ni moja wapo ya sababu inayochangia kushuka kwa viwango vya elimu katika shule za Rwanda.

Katika shule ya msingi ya Gashora kusini mashariki mwa Rwanda na maeneo mengine ya vijijini suala la idadi kubwa ya wanafunzi isiyolingana na idadi ya madarasa ya shule ni jambo la kawaida.

"Sisi hapa darasani tunakaa sakafuni na kuna wengine wanaokaa kwenye madumu ya maji lakini yule anayerauka mapema ndiye anayekalia kiti. tunapendekeza serikali kutafakari swala hili na kutupatia vifaa'' anasema Mwalimu Beata Mushime

Sensa ya hivi karibuni ya wizara ya elimu imebainisha kwamba shule nyingi zina idadi ya kupindukia ya wanafunzi ambako katika baadhi ya maeneo chumba kimoja kinaweza kuwa na wanafunzi zaidi 100.

Image caption Darasa moja linaweza kuwa na kuwa na wanafunzi zaidi 100

Mwalimu Beata Mushime anasema kwamba sio kazi rahisi kufundisha watoto katika hali ya msongamano darasani.

''Ukiangalia shule nyingi eneo hili zinakabiliwa na tatizo la msongamano mkubwa wa wanafunzi, iwe shule za sekondari ambako darasa la kwanza lina watoto 90 na katika shule za msingi darasa la kwanza lina watoto 85.'' alisema.

Aliongeza kuwa idadi hiyo ni kubwa sana na kutilia shaka ikiwa mwalimu mmoja ana uwezo wa kufundisha idadi kubwa kama hiyo.

''Labda kila darasa lingekuwa na wastani wa wanafunzi 40 hapo ingeeleweka.''

Katika badhi ya maeneo waliamua kutafuta njia mbadala kutatua suala hilo ambapo wanafunzi wanapishana kusoma kwa nyakati tofauti.

Baadhi yao wanasoma asubuhi na wengine mchana ,lakini mpango huo pia una changamoto zake anasema bwana Janvier Tuyishime ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya Gashora.

''Mtindo wa wanafunzi kusoma kwa kupokezana ni mgumu.dakika 40 kwa somo moja haitoshi.inaweza kumalizika nikiwa nimeweza kutoa ufafanuzi kwa wanafunzi tuseme 30 tu''.

''Tafakari hali ilivyo katika darasa lililo na wanafunzi 90, kwa hiyo ni kama wengine hawapati kitu.'' alisema mwalimu huyo mkuu.

Image caption Katika baadhi ya maeneo wanafunzi wanapishana kusoma kwa nyakati tofauti ili kukabiliana na tatizo la msongamano wa wanafunzi

Afisa mkuu wa bodi ya taifa ya elimu Irene Ndayambaje ameiambia BBC kwamba suala hilo limekuwa likiwasumbua kwa muda lakini sasa wakati umewadia wakati wa kulipatia ufumbuzi:

"Njia pekee iliyopo ni kuongeza idadi ya madarasa ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya waalimu''

Bi Ndayambaje pia amesema bodi yake inatafakari mpango wa kujenga shule zaidi karibu na vijiji ili kupunguza safari ndefu ambazo watoto wanafanya kwenda au kutoka shuleni.

''Masuala hayo lazima yapatiwe ufumbuzi mnamo siku chache zijazo.''

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii