Bosco Ntaganda ahukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa makosa ya uhalifu DRC

Ntaganda Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bosco Ntaganda alipatikana ana hatia ya kuongoza kampeni ya ukatili mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo

Kiongozi wa zamani wa waasi wa Congo amehukimiwa kifungo cha miaka 30 jela la Mahakama ya Kimataifa ya jinai kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu .

Waoiiganaji waliomtii Bosco Ntaganda walitekeleza mauaji ya ukatili dhidi ya raia, Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), walisema mwezi Julai.

Ntaganda, ambaye alipewa jina la bandia "Terminator", alipatikana na makosa 18 mkiwemo ubakaji, utumwa wa ngono , na kuwatumikisha watoto kama wanajeshi.

Hukumu dhidi yake ni ya muda mrefu kuwahi kutolewa katika historia ya mahakama ya ICC

Onyo: Taarifa hii inaweza kuwa na maelezo ambayo yanaweza kuwaogofya baadhi ya wasomaji

Ntaganda alikuwa ni mtu wa kwanza kupatikana na hatia ya utumwa wa ngono na mahakama ya ICC kwa kwa ujumla ni mtu wa nne ambaye mahakama hiyo imempata na hatia tangu ilipoundwa mwaka 2002.

Ntaganda amnbaye alizaliwa nchini Rwanda mwenye umri wa miaka 46-muasi wa zamani amekuwa akihusika na mizozo mbali mbali ya kivita nchini Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Wachambuzi wanasema kujisalimisha kwake katika ubalozi wa Marekani nchini Rwanda kilikuwa ni kitendo cha kujilinda kutokana na hatari iliyokuwa inamkabilibaada ya kupoteza mamlaka ndani ya kikundi chake cha waasi wa M23.

Bosco Ntaganda ni nani?

  • Alizaliwa nchini Rwanda 1973 ambako alikulia
  • Alikimbilia DRC akiwa kijana mdogobaada ya watu wa kabila lake la Watutsi kushambuliwa
  • Akiwa na umri wa miaka 17, alianza maisha yake ya mapigano -wakati fulani akiwa kama muasi na wakati mwingine kama mwanajeshi wa Rwanda na DRC
  • Baina ya mwaka 2002-3: Alikuwa kiongozi wa wanamgambo katika jimbo la Kongo la Ituri
  • 2006: Alishtakiwa na Mahakama ya ICC kwa madai ya kuwaingiza watoto jeshini katika jimbo la Ituri
  • Alikuwa mkuu wa vikosi vilivyofanya mauaji ya kikatili ya Kiwanja mwaka 2008 ambapo watu 150 waliuawa
  • 2009:Alijiunga na jeshi la taifa la Kongo akapewa cheo cha Generali
  • 2012: Alitoroka jeshi, na kuanzisha uasi uliowalazimisha watu 800,000 kuyakimbia makazi yao
  • 2013: Alijisalimisha katika ubalozi wa Marekani mjini Kigali nchini Rwanda, baada ya migawanyiko ndani ya kundi la waasi
  • 2019: Amepatikana hati ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya ICC na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela

Alifanya nini?

Mwezi Julai , majaji watatu walimpata Ntaganda na hatia ya makosa yote 18 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliofanyika katika jimbo lenye utajiri wa madini lililoko mashariki wa DRC la Ituri kati ya mwaka 2002 na 2003.

Ntaganda alikuwa "kiongozi muhimu " ambaye alitoa amri ya "kuwalenga na kuwauwa raia" jaji Robert Fremr alisema katika hukumu yake.

Waendeshamashtaka walikuwa wamesema Ntaganda alikuwa mtu muhimu katika kupanga, na kuendesha harakati za waasi wa Union of Congolese Patriots (UCP) na tawi lake la kijeshi la Patriotic Forces for the Liberation of Congo (FPLC).

Kikundi cha kijeshi kiliendesha mashambulio dhidi ya watu walioaminiwa kuwa hawatoki katika kabila la Wahema, ICC ilibaini.

Katika shambulio moja , wapiganaji 49 waliwakamata watu katika shamba la migomba nyuma ya kijiji kwa kutumia "fimbo, vifungo pamoja na visu na mapanga ".

"Wanaume , wanawake na watoto pamoja na watoto wachanga walipatikana katika shamba hilo .Baadhi ya miili ilipatikana ikiwa uchi, baadhi yake ikiwa imefungwa kwa kamba na baadhi ilikuwa imekatwa kichwa ," Alisema jaji Fremr.

Ghasia katika jimbo hilo ziliwauwa watu zaidi ya 60,000 tangu mwaka 1999 huku wanamgambo wakipigania udhibiti wa vyanzo vichache vya madini, yanasema makundi ya haki za binadamu.

Majaji waliamua kuwa Ntaganda binafsi alimuua Padri wa kikatoliki wakati wapiganaji aliowaongoza walipofanya uvamizi jimboni humo.

Image caption Uhalifu ulifanyika wakati Ntaganda alipohudumu kama naibu mkuu wa majeshi wa kiongozi wa waasi wa UCP Thomas Lubanga

Uhalifu ulifanyika wakati Ntaganda alipohudumu kama naibu mkuu wa majeshi wa kiongozi wa waasi wa UCP Thomas Lubanga.

Mwaka 2012 Lubanga alikuwa mtu wa kwanza kupatikana na hatia na mahakama ya ICC na akahukimiwa kifungo cha miaka 14 jela.

Wote waliopatikana na hatia hadi sasa na mahakama ya ICC wanatoka barani Afrika. Mtu wa tano , Jean-Pierre Bemba, makamu wa zamani wa rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo , awali alipatikana na hatia ya uhalifu wa kivita kabla ya kufutwa na mahakama ya rufaa ya ICC mwaka jana.

Unaweza pia kusoma:

Taarifa za zamani kumuhusu Ntaganda

Ntaganda alikuwa mpiganaji chini ya rais wa sasa wa Rwanda , Paul Kagame, wakati Bwana Kagame alipokuwa kiongozi wa Rwanda Patriotic Front (RPF) kikundi kilichopigania kumaliza mauaji ya kimbari ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi .

Baada ya ghasia za Rwanda kusambaa hadi nchi jirani ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo , Ntaganda alikuwa akipigana kama muasi na wakati mwingine kama mwanajeshi wa jeshi la taifa katika jeshi la Rwanda na jeshi la Kongo.

Mwaka 2012, alikuwa mmoja wa waasisi wa kikundi cha waasi wa M23 baada kutoroka na mamia ya wanajeshi kutoka jeshi la taifa la Congo.

Baadae wapiganaji wake waliuteka mji wa masharaki mwa DRC wa Goma kabla ya kuafiki kuondoka mjini humo. Takriban watu 800,000 waliripotiwa kuyakimbia makazi yao.

Kundila waasi wa M23 hatimae lilishindwa na vikosi vya serikali ya Kongo mwaka 2013.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii