Ghasia Iraq: Bunge limeidhinisha kujiuzulu kwa waziri mkuu Abdul Mahdi

Wanafunzi wakiandamana mjini Basra 01/12/2019 Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanafunzi siku ya Jumapili waliandamana mjini Basra kuomboleza waliouawa katika ghasia

Bunge nchini Iraq limeidhinisha hatua ya kujiuzulu kwa waziri mkuu wa nchi hiyo Adel Abdul Mahdi baada ya wiki kadhaa za maandamano ya yaliyokumbwa na vurugu.

Haijabainika ni nani atakayemrithi bwana Abdul Mahdi. Spika wa bunge amesema rais Barham Saleh atapewa jukumu la kumteua waziri mkuu mpya.

Huku hayo yakijiri kiongozi wa kanisa katoliki duniani papa Francis ni kiongozi wa hivi punde mwenye ushawishi aliyelaani vitendo vya vikosi vya usalama kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

Watu 400 wameuawa tangu maandamano yalipoanza mwezi Oktoba katika mji wmkuu wa Baghdad na miji mingine nchini humo.

Maelfu ya wengine wamejeruhiwa. Raia wa Iraqi wanalalamikia ukosefu wa ajira na kushinikiza kukomeshwa kwa ufisadi na huduma bora ya umma.

Siku ya Jumapili ghasia ziliendelea kushuhudiwa katika miji ya Baghdad na Najaf.

Nini kinachofanyika katika bunge la Iraq?

Hatua ya kuidhinisha kujiuzulu kwa waziri mkuu Abdul Mahdi ilifikiwa katika kikao cha dharura kilichoitishwa siku ya Jumapili.

Sheria za Iraq zilizopo hazipo hazijaelezea kinaga ubaga jinsi wabunge wanvyostahili kushughulikia suala la kujiuzulu kwa waziri mkuu, lakini watunzi wa sheria siku ya Jumapili walichukua hatua kwa mujibu wa angalizo laMahakama ya juu zaidi, iliripoti shirika la habari la Associated Press.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri Mkuu Adel Abdul Mahdi akitoa tangazo la kujiuzulu kwake siku ya Ijumaa

Kwa mujibu wa katiba, anatarajiwa kuwasilisha ombi kwa mrengo ulio na wabunge wengi bungeni kumteua waziri mkuu mpya kuunda serikali.

Bwana Abdul Mahdi na serikali yake atasalia madarakani kwa kipindi cha mpito hadi serikali mpya itakapoteuliwa, ripoti zinasema.

Kuhusu Abdul Mahdi

Abdul Mahdi alishika nafasi hiyo kipindi cha mwaka mmoja uliopita, akiahidi mabadiliko ahadi ambayo haijatekelezwa. Vijana wa Iraq waliingia kwenye mitaa ya Baghdad kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

Baada ya maandamano ya kwanza yaliyodumu kwa siku sita na kugharimu maisha ya watu 149 Mahdi aliahidi kufanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri na kupunguza mishahara ya maafisa wa juu, na alitangaza pia kushughulikia suala la ukosefu wa ajira.

Lakini waandamanaji wanasema kuwa matakwa yao hayajatimizwa na kurejea tena mitaani mwishoni mwa mwezi Oktoba. Maandamano yalifanyika nchi nzima baada ya maafisa wa usalama kutumia nguvu kuwadhibiti waandamanaji.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maandamano yaliendelea mjini Najaf siku ya Jumapili

Papa alisema nini?

Papa amlisema anafuatilia matukio nchini Iraq "kwa hofu".

"Inasikitisha sana kufahamu kuwa waandamanaji wamekuwa wakikabiliwa kwa nguvu kupita kiasi, hali ambayo imesababisha mauaji wa watu kadhaa," alisema katika ibada yake ya kila wiki siku Jumapili.

Papa Francis amesema kuwa anataka kuzuru Iraq mwaka ujao

Maandamano ya kupindga serikali yalifanyika katika mji wa kusini wa Basra siku ya Jumapili kuomboleza waliouawa katika maandamano siku za hivi karibuni.

Huwezi kusikiliza tena
Waandamanaji walivyosherehekea siku ya Ijumaa baada ya Waziri Mkuu kusema kuwa ataachia madaraka

Hii inafuatia ripoti za vyombo vya habari nchini Iraq kuwa afisa wa polisi amehukumiwa kifo kwa kuwaua waandamanaji katika mkoa wa Wasit, kusini-mashariki mwa Baghdad.

Afisa mwingine aliripotiwa kuhukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani.

Hukumu hiyo ya kifo ikithibitishwa, itakuwa ya kwanza kutekelezwa dhidi ya afisa wa polisi wa Iraq katika kipindi cha miezi miwili ya ghasia nchini humo.

Lakini waandamanaji walisema matakwa yao hayakutekelezwa na kurejea tena barabarani mwishoni mwa Oktoba.

Maandamano yalishika kasi na kusambaa kote nchini baada ya vikosi vya usalama kujibu ghasia kwa nguvu kupita kiasi.

Maafisa wanasema polisi kadhaa pia wameuawa katika maandamano hayo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii