Uchaguzi Chadema: Je, Sumaye na Mwambe kumuangusha Mbowe uenyekiti taifa baada ya kushindwa kanda?

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, CHADEMA , bwana Freeman Mbowe Haki miliki ya picha CHADEMA
Image caption Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, CHADEMA , bwana Freeman Mbowe

Baada ya kukiongoza chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema kwa miaka 15 Freeman Mbowe anawania tena nafasi ya uenyekiti kwa miaka mingine mitano.

Wanachama wawili wa chama hicho wamechukua fomu ili kushindana naye, nao ni waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, Frederick Sumaye na Mbunge wa Jimbo la Ndanda mkoani Mtwara, Cecil Mwambe.

Sumaye na Mwambe ni vigogo wanaowania nafasi hiyo ya kitaifa japo hivi karibuni wametoka kushindwa katika kinyang'anyiro cha nafasi ya uenyekiti wa Kanda ya Pwani na Kusini mtawalia.

Kwa mujibu wa kalenda ya chama hicho, uchaguzi wa mwenyekiti unatarajiwa kudfanyika Desemba 18 mwaka huu, baada ya kutanguliwa na uchaguzi wa wenyeviti wa kanda.

Demokrasia ndani ya Chadema

Haki miliki ya picha Getty Images

Kikiwa ni chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema kimekuwa mstari wa mbele kutuma mashambulizi kwa chama tawala CCM na serikali yake.

Moja ya mashambulizi hayo ni kuwa CCM na serikali yake wanabana demokrasia na uhuru wa kujieleza na kuhoji ndani ya nchi.

Lakini kwa wapinzani wa Mbowe ndani ya Chedema na baadhi nje ya chama hicho wamekuwa wakimshutumu kiongozi huyo kwa kuminya demokrasia ndan ya chama.

Mbowe yupo kwenye usukani wa Chadema kwa miaka 15, huku akimudu kuhimili vishindo vya upinzani na kuchaguliwa kwa kishindo.

Katika uchaguzi uliopita wa chama mwaka 2014, alikuwa akiwania nafasi hiyo na Gambaranyera Mongateo ambaye hakuwa maarufu katika siasa za Chadema kama ilivyo kwa Sumaye na Mwambe kwa hivi sasa.

Mbowe alishinda kwa asilimia 97.3 kutokana na kura 789 alizopata dhidi ya Mongateo aliyepata kura 20 tu.

Kwa wapinzani huu ni wakati mwafaka kwa sasa Mbowe kukiacha chama kwa uongozi mwingine ikiwa ni ishara ya kusisimua demokrasia na kufurahisha ushindani ndani ya chama.

Ushindani wa kuwania uenyekiti wa chama hicho ulizaa mgogoro mkubwa baina ya mbowe na mwanasiasa mwegine maarufu wa upinzani nchini Tanzania, Zitto Kabwe.

Mwishowe Zitto alitimuliwa Chadema na kwenda kukiongoza chama cha ACT-Wazalendo ambacho, kwa kiasi kikubwa kilianzishwa na wanachama wa zamani wa Chadema ambao walikuwa wanamuunga mkono Zitto.

Hata kushindwa kwa Sumaye na Mwambe katika nafasi za kanda kwa baadhi ya wachambuzi kunahusishwa na wao kuchukua fomu ya kumkabili Mbowe kwa nafasi ya kitaifa.

Sumaye, katika Kanda ya Pwani hakuwa na mpinzani kwenye kinyang'anyiro hicho.

Hata hivyo, alipingwa kwa kura 48, kati ya kura 76 alizopigiwa.

Baada ya matokeo, Sumaye alikiri kuwa "ameadhibiwa" kwa kuchukua fomu ya uenyekiti wa chama taifa.

Cecil Mwambe alishindwa kutetea kiti chake katika uenyekiti Kanda ya Kusini baada ya kupata kura 31, huku mpinzani wake Selemani Mathew akipata kura 53.

Anguko hilo pia limehusishwa na siasa za ndani ya chama hicho kwa kile kinachoitwa 'kupingana na mwenyekiti'.

Dk. Vicencia Shule wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) amemwambia mwandishi, "Mzazi bora ni yule anayemuona mtoto wake akikua. Hivyo ndivyo inavyokuwa kwenye uongozi, mkuu wa kazi aliye bora ni yule ambaye anatengeneza wenye uwezo zaidi yake wengi kwa wakati,"

"Mimi ni muumini wa kuweka nukta. Kila kitu lazima kifikie mwisho na kingine kianze. Kwa mfano ni vizuri kuweka nukta na kuanza sentesi mpya kuliko kuwa na sentesi ndefu haina kituo ala mwisho hadi inapoteza maana."

Richard Ngaya, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) na mchambuzi wa siasa na utawala bora haamini kama kuanguka kwa vigogo hao ni fitina za ndani za kisisa.

"Kukatwa kwa Sumaye ni zao la kipimo cha wanachama ambao wameonyesha hawana imani naye pamoja na kuwa alikuwa mgombea pekee. Wanachama wamempima kwa kipindi alichokuwa mwenyekiti na kuona hajafanya vyema majukumu ya uenyekiti na kuhofia hataweza kuwavusha mwakani kwenye uchaguzi mkuu, ukizingatia Kanda ya Pwani ina wapigakura wengi, ni muhimu sana.

Ameongeza kuwa, "Kwa upande mzuri, kujenga taswira nzuri ya chama kumpa Sumaye uenyekiti inabidi iendane na uwezo wa kuongoza. Si Sumaye pekee hata mwingine yeyote."

Nguvu ya Mbowe ni ipi?

Haki miliki ya picha CHADEMA,TWITTER
Image caption Je, vyama vya upinzani Tanzania vina demokrasia?

Watetezi wa Freeman Mbowe wanasema hawana wasiwasi na kiongozi huyo kwani ameleta mafanikio makubwa ndani ya chama hicho tangu alipokikuta kikiwa na wabunge wasiozidi watano hadi kufikisha takribani 50 .

Vilevile kiongozi huyo ameweza kufanya chama chake kujizolea kura milioni 6 katika uchaguzi mkuu nafasi ya urais ambapo kete yake ya kumpigania Edward Lowassa kuwa mgombea wa vyama vya upinzani ilizaa matunda kwa wingi wa wabunge na wawakilishi kwenye halmashauri mbalimbali nchini.

Kiongozi mmoja mwandamizi kutoka chama tawala cha CCM na serikali ya awamu ya tano, amemwambia mwandishi wa makala haya, "Namfahamu Mbowe, nimekuwa ndani ya chama hicho.

Zipo kasoro, lakini watu wanatakiwa kumtazama ngwe hii anafanya nini.

Binafsi nimeona kwa jicho la tatu, kumchukua Tundu Lissu kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni ishara kuwa Mbowe anajiandaa kung'atuka madarakani.

Tatizo hatujui ni lini atang'atuka na mikakati yake ni ipi mara atakapoondoka. Lissu ameingizwa kwa mkakati maalumu wa mwenyekiti wa sasa, na huenda atashinda kwenye uchaguzi wa nafasi hiyo."

Mtanzania Profesa Joseph Mbele kutoka Chuo cha Mtakatifu Olaf, Minessota nchini Marekani anamchambua Freeman Mbowe kama kiongozi wa mfano ambaye anapaswa kuigwa na jabali lisilotikisika kisiasa nchini Tanzania.

Image caption Mwanasiasa maarufu wa Tanzania kupitia CHADEMA, Tundu Lissu

Anasema, "Mbowe hatingishiki na umaarufu wa wenzake, akina Tundu Lissu, Peter Msigwa, Godbless Lema, au Halima Mdee. Wote wako naye, naye yuko nao.

Hiyo ndio tabia ya mtu anayejiamini. Kutokana na akili yake hiyo na busara zitokanazo, Mbowe amefanikiwa kuijenga Chadema mwaka hadi mwaka, hadi leo kimekuwa ni chama kikuu cha upinzani, chenye kuongoza majimbo na miji mikubwa.

Ingekuwa kuna fursa na uhuru sawa kwa kila chama kufanya shughuli zake kama inavyoelekezwa na katiba na sheria, nina hakika Chadema ingekuwa mbali zaidi."

Je, nani anafaa kumrithi Mbowe?

Haki miliki ya picha HISANI
Image caption Viongozi wa Chadema

Jovinson Kagirwa, mwanasheria na mchambuzi wa siasa na utawala bora nchini Tanzania, amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa, "Mwenyekiti anayefaa katika hatua hii ndani ya Chadema ni John Heche au Tundu Lissu.

Nje ya wanasiasa hawa wawili, ni afadhali chama kikae na kaimu mwenyekiti. Katika nyakati hizi mtaji sio fedha, bali mtaji hapa ni kufufua mioyo ya wanachama na wafuasi wao, kitu ambacho kinaogopwa na wapinzani wa upinzani kwa sasa ni mioyo ya watanzania kufufuka na kuanza kudai madai yao.

"Haiwezekani mwenyekiti wa chama cha upinzani kama Chadema unashindwa kumkemea mwenyekiti wa CCM pale anapotumia lugha mbaya kuwakemea wapinzani.

Kwa sababu tumeshaingia kwenye 'mob democracy', vyama vya upinzani vinahitaji kiongozi mwanaharakati kama tulivyoona maoni ya mwanasiasa mkongwe na mwenyekiti wa TLP, Augustine Lyatonga Mrema kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ambapo alisema kuwa harakati ndio siasa za sasa."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii