Marekani yasaini muswada kupinga vikwazo vya China dhidi ya waislamu wa Uighur

Marekani yasaini muswada kupinga vikwazo vya china dhidi ya waislamu wa Uighur
Maelezo ya picha,

Marekani yasaini muswada kupinga vikwazo vya china dhidi ya waislamu wa Uighur

Bunge la Marekani limepitisha muswada ili kupambana na vile wanavyovisema kuwa ni vikwazo visivyo na mantiki, mateso na unyanyasaji kwa waislamu wa jamii ya Uighur nchini China.

Imelenga vile vikwazo vinavyowalenga wanachama wa serikali ya China na kumtaja kiongozi wa chama cha kikomunisti katika mkoa wa Xinjiang,Chen Quanguo.

Muswada huo bado unahitaji idhini kutoka kwa seneta na Rais Donald Trump.

Kwa upande wa China, Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo ameoneshwa kutofurahishwa na kusema hatua hiyo ni ya ''uovu''.

Muswada wa haki za kibinadamu za Uighur wa mwaka 2019 ulipitishwa bungeni na wabunge 407 kwa 1 usiku wa Jumanne.

Kupitishwa kwake kunakuja mara baada ya Rais Trump kutia saini sheria inayounga mkono maandamano ya demokrasia mjini Hong Kong pia kusababisha ukandamizaji kutoka kwa China.

Thomas Massie kutoka chama cha Republican kutoka Kentucky, amepiga kura kupinga muswada huo wa Uighur, vilevile hakuupigia kura muswada wa Hong Kong.

Mwandishi wa BBC nchini China John Sudworth amesema kama muswada huu utapitishwa basi ''itaashiria jaribio muhimu sana la kimataifa kushinikiza China kuhusu kuwaweka kizuizini waislamu wengi wa Uighur na wale kutoka makundi mengine ya kiislam.''

Maelezo ya video,

Ni kwanini waandamaji hawa wanapigwa?

Je ni nini kipo katika muswada huo?

Lengo kuu la muswada huu ni kuweka wazi unyanyasaji wa haki za binaadam zijulikazo duniani kote, ikiwemo kufungwa kwa waislamu millioni 1 wa Uighur.

Na pia unaushutumu China ''kwa kuwabagua waislamu wa jamii ya Uighur katika mifumo yao kwa kuwanyima haki mbali mbali za kiraia na kisiasa, ikiwemo haki za kujieleza, dini, uhuru wa kuandamana na mashtaka ya haki.''

Muswada huu unashutumu sera za China zinavyowakandamiza waislamu mkoani Xinjiang.

Hizi ni pamoja na:

  • Uangalizi wa wote kutumia teknolojiia za kisasa, ikiwemo ukusanyaji wa sampuli za vinasaba kutoka kwa watoto.
  • Utumiaji wa kodi za QR nje ya nyumba ili kujua ni mara ngapi watu husali.
  • programu ya kutambua sauti na uso za watu na teknolojia ya kugundua wahalifu.

Muswada wa Uighur unalenga maafisa kutoka China ambao wanadhaniwa kuhusika na ukiukaji wa haki za kibinaadamu katika mkoa wa Xinjiang.

Vievile unamtaja kiongozi wa chama cha kikomunisti cha Xinjiang Chen Quanguo, ambaye inasemekana kuwa mbunifu wa kambi hizo.

Muswada huo unamtaka Rais Donald Trump kupinga unyanyasaji wa waislam wa Uighur, China kufunga kambi zote haraka iwezekananavyo na kuhahakisha haki inatendeka.

Raia wa China wanasema nini?

Waziri wa mambo ya nje kutoka China ameuita muswada huo kuwa ni wa ''uovu' na kuitaka Marekani kuacha kuingilia masuala ya ndani ya China.''

Msemaji mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya China, Hua Chunying amesema ''Muswada huu unachafua sheria za haki za kibinadam mkoani Xinjiang na kushambulia vibaya sheria ya serikali ya China katika Mkoa wa Xinjiang,''

''Tunaiomba Marekani kurekebisha makosa yao mara moja, na kuzuia muswada huu kuwa sheria, na kuacha kutumia matatizo ya Xianjing kama njia ya kuingilia masuala ya ndani ya China.''

China pia imeonesha kukasirishwa na muswada wa Hong Kong, na kusimamisha safari za meli za jeshi la Marekani na ndege zote zinazokwenda Hong Kong, na kuweka vikwazo kwa makundi ya kutetea haki za binaadamu nchini Marekani.

Ni nini kinaendelea mkoani Xinjiang?

Makundi ya kutetea haki yanasema maelfu ya waislamu wanashikiliwa katika makambi ya gereza katika sehemu mbali mbali ndani ya mkoa huo.

Maelezo ya picha,

Mamlaka za China zinasema waislamu wa Uighur wanaelimishwa katika vituo vya mafunzo ya ufundi ili kukabiliana na msimamo mkali wa kidini.

Mamlaka za China zinasema waislamu wa Uighur wanaelimishwa katika vituo vya mafunzo ya ufundi ili kukabiliana na msimamo mkali wa kidini.

Lakini ushahidi unaonesha wengi wakiwa wameshikiliwa kwa kuikubali dini yao kwa mfano kwa kusali, kuvaa ushungi au kwakuwa na uhusiano na nchi kama Uturuki.

Rekodi zilizotazamwa na BBC zinaonesha kuwa China wanawatenganisha watoto wa Kiislamu mbali na familia zao kwa makusudi.

Mtafiti kutoka Ujerumani, Dkt Adrian Zenz, aliiambia BBC mapema mwaka huu kuwa hatua hiyo ni jaribio la ''kutengeneza kizazi kipya kilichotenganishwa mbali na asili zao, imani na lugha zao.''

''Ninaamini ushahidi unasababisha kuwa kitendo hiki ni mauaji ya tamaduni.''

Balozi wa China nchini Uingereza amekataa shutuma hizo na kudai kuwa ni za ''uongo''.