Sumaye: Labda mke wangu na watoto sasa watanivika taji kwa uamuzi huu

Sumaye

Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Fredrick Sumaye amejivua uanachama wa chama cha upinzani Chadema akidai chama hicho hakina demokrasia.

Sumaye ametangaza uamuzi wake leo Jumatano Disemba 4, 2019 ikiwa ni miaka minne toka ajiunge na upinzani akitokea chama tawala cha CCM.

Kigogo huyo amekituhumu chama hicho kuminya demokrasia na kumfedhehesha katika mchakato wa uchaguzi wa ndani.

Sumaye alikuwa akitetea kiti chake cha mwenyekiti wa Kanda ya Pwani na kuangukia pua.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 28, Sumaye hakuwa na mpinzani lakini aliambulia kura 28 za Ndiyo na kupingwa kwa kura 48.

Kwa mujibu wa Sumaye, anaachana na Chadema lakini hajiungi na chama kingine cochote cha siasa.

"Najua katika kujikosha watasema nimepewa pesa. Lakini kama nilijiunga Chadema kwa pesa. basi na kuondoka pia nimepewa pesa. Lakini kama nilijiunga kwa utashi wangu basi na leo najiondoa kwa utashi wangu...Mimi sijawahi kuwa kibaraka wa mtu, kundi au kibaraka wa chama chochote na sitakuwa hivyo hata siku moja."

'Hakuna demokrasia Chadema'

Hii leo Sumaye amedai kuwa kushindwa kwake kulipangwa na alifanyiwa mchezo mchafu wa kisiasa baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Chadema taifa.

Nafasi ya Mwenyekiti Chadema inashikiliwa na Freeman Mbowe kwa miaka 15 sasa na amechukua tena fomu ya kuwania kiti hicho kwa miaka mitano mingine.

"Nongwa ilikuja baada ya kuamua kuchukua fomu ya kugombea kiti cha taifa," amesema Sumaye.

Kwa mujibu wa Sumaye, alichukua fomu ya nafasi ya taifa ili kuondosha hisi zilizopo kuwa hakuna demokrasia ndani ya Chadema, na pia kuondoa hisia kuwa nafasi ya Mwenyekitikwa Chadema ni Mbowe tu na haisogolewi na mtu mwengine.

Huwezi kusikiliza tena
Sumaye: Chama cha Chadema hakina demokrasia.

"Mimi binafsi sikuamini kuwa hisia hizi ni za kweli, kumbe nilikuwa nimekosea sana kufikiria hivyo...Baadhi ya wajumbe wa kamati kuu ambao walifanya mipango ya mimi kuletewa fomu za kanda na kuwa mgombea pekee, waligeuka na kuhakikisha kuwa kura za hapa ndiyo zinashinda. Wajumbe karibia wote walipigiwa simu na baadhi yao kufichwa hotelini kwa kazi hiyo," ameeleza Sumaye.

"...sababu kubwa ati kwa nini nimechukua fomu ya kiti cha taifa. Basi wangelinitahadharisha tu kuwa katika chama chetu nafasi hiyo ina utaratibu wa nje ya katiba ningeelewa na labda ningetii, na kama nisingetii wangenisubiri kwenye vikao vya chama na si nafasi ya kanda."

Image caption Sumaye amelaumu kundi analosema lipo karibu na mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kwa kumfanyia hila ili aanguke.

Sumaye anasema alijua kuwa anataka kuchezewa mchezo mchafu na akatahadharisha kabla ya uchaguzi wa kanda kufanyika, na kuonya kuwa wakipiga kura kwa "walivyoshawishiwa" kutadhihirishia umma kuwa hakuna demokrasia kwenye chama hicho.

"Si muafaka wala busara kwangu kuendelea kugombea nafasi hiyo. Mbowe alituonya kuwa sumu haionjwi kwa ulimi na mimi sitaki kuionja hiyo sumu...najua utashinda, lakini Mbowe hilo kundi lako la ndani usipoliangalia litavunja chama. Najua utashinda lakini unganisha chama. Profesa (Abdallah) Safari alituaonya kwa maneno ya kufikirisha lakini hatimaye alishambuliwa kwa matusi, najua nami inawezekana nikashambuliwa."

'Familia yangu itanivika taji'

Sumaye ameeleza waandishi wa habarikuwa kuondoka CCM na kujiunga na kujiunga upinzani halikuwa jambo rahisi.

"Mashamba yangu yalichukuliwa, hata baadhi ya huduma zangu na haki zangu zilianza kuwa tofauti na za wastaafu wenzangu. Familia yangu ilianza kuona mateso ya mimi kuwa upinzani, walinilaumu na kusononeka sana. Pamoja na hali hii ya mateso nilikaza shingo kwa vile niliamini kuwa kinachopiganiwa na wapinzani, kama kitafanikiwa ni kikubwa kuliko hiki cha familia yangu."

Sumaye amesema hila alizofayiwa zimemfedhehesha, na jambo hilo limeamsha hasira zilizokuwa zimetulia kutoka ndugu na marafiki zake.

"Ningeweza kukaza shingo kama pale mwanzo na labda yangepita tu, lakini malengo yetu tunayafikiaje na kufanikwa kwa demokrasia ipi ndani ya chama?"

Labda kwa kitendo hiki mke wangu na wanangu sasa watanivika taji kwa kuwaondolea adha walizokuwa wanapambana nazo kwa mimi kuwa upinzani."

Mada zinazohusiana