Yesu wa Tongareni ni nani?

''Yesu'' wa Tongareni (kulia) pichani na mmoja wa wake zake pamoja na mtoto wake
Image caption ''Yesu'' wa Tongareni (kulia) pichani na mmoja wa wake zake pamoja na mtoto wake

Katika kijiji cha Luhohwe kilichopo jimbo la Bungoma magharibi mwa Kenya anapatikana mwanaume anayejulikana kama 'Yesu' wa Tongareni.

Maisha yake yalikuwa ni ya kawaida hadi ilipofika mwaka 2009 ambapo anadai Mungu alimjia na kumpatia jina Yesu, na kuanzia siku hiyo hapaswi kuitwa au kutaja majina yake ya awali.

Mwandishi wa BBC Roncliff Odit, alipomtembelea hivi karibuni maghribi mwa Kenya, Yesu wa Tongareni alisema aliitwa jina Yesu na Mungu mwenyewe: ''Mungu akanena nami akanipa jina Yesu...

Nawatangazia watu wamrejelee Mungu katika njia ya toba wapate ondoleo la dhambi, ili majina yao yawe katika kitabu cha uzima wa milele'' alisisitiza Yesu wa Tongareni kwa sauti ya madaha.

Mazungumzo yake na Odit yalikatizwa ghafla na kuwasili kwa wafuasi wake ambao walipiga magoti mbele yake na kuanza kuabudu kwa sauti za juu: ''Pokea sifa, heshma na utukufu juu mbinguni, duniani na hata milele na milele ...amina''.

Image caption Wafuasi wake hupiga magoti na kumuabudu kwa kupiga magoti mbele yake na kuanza kuabudu kwa sauti za juu

Tofauti na Yesu Kristo ambaye wewe unamuamini au umesikia kuhusu habari zake, yesu wa Tongareni ameoa, ana mke na hata watoto.

Kulingana na mke wake, kuoa kwa yesu wa Tongareni kunatokana na maandiko matakatifu.

''Katika ufunuo wa Yohana mlango ni wa 21, mstari wa 9'', ...na kabla hajamaliza kusoma sehemu hiyo ya ufunuo wa Yohana ... mume wake (Yesu wa Tongareni) alimkatiza na kumalizia kusoma; ''Maandiko yanasema hivi, kisha mmoja wa wale malaika saba waliokua na yale mabakuli saba yaliyokua yamejaa mapaa saba ya mwisho, akaja na kuniambia njoo nami nitakuonyesha bibiharusi mkewe mwanakondoo'', alisoma Yesu huyo wa Tongareni.

Image caption Yesu wa Tongareni anasema, familia yake haikuipokea vyema taarifa ya kubadilisha jina na kuitwa Yesu

Yesu wa Tongareni anasema, familia yake haikuipokea vyema taarifa ya kubadilisha jina na kuitwa Yesu na kuacha mienendo yake ya zamani.

Unaweza pia kusoma:

''Wengi walinena huyu ameharibika kichwa, huyu ni mwendawazimu, hata amerukwa na akili na anaongea lugha zisizoeleweka'' alisisitiza yesu wa Tongareni ambaye alisema anaamini akili yake iko sawa kulingana na mapenzi ya Mungu.

Aliwaomba watu wawe kati toba ili waokolewe, akiamini kuwa katika jiji la Naoirobi ni watu wawili tu watakaookolewa siku ya mwisho( ya kiama).

Si mara ya kwanza kwa eneo la magharibi mwa kwa watu Kenya kujitambulisha kuwa na uwezo wawakuaminiwa kiimani.

Katika miaka ya nyuma mwanamume mmoja magharibi mwa Kenya aliyejiita Jehova Wanyonyi alidai kuwa yeye ndiye Mungu.

Alikuwa na waumini na alikuwa ameoa wanawake zaidi ya wanawake 10 na watoto zaidi ya 100.

Wake zake pamoja na watu wengine watano waliomzingira wakati wote walijiita malaika.

Image caption Jehova Wanyonyi kutoka eneo la magharibi mwa Kenya alijiita kuwa yeye ni ''Mungu''

Malaika hao waliamini kuwa Yesu atakaporudi atakaribishwa na Jehova Wanyonyi na malaika hao watamuweka chini ya miguu ya Wanyonyi ili aweze kuurithi ufalme wa mbingu.

Hata hivyo kiongozi huyo wa madhehebu wa kundi linalojiita Waisraeli, alipotea na baadae serikali ya Kenya ilitangaza kuwa alifariki na wafuasi wake kuzika maiti yake mahali pasipo julikana.

Hata hivyo wafuasi wake walisema kuwa Jehova Wanyonyi bado yu hai na anaendelea kufanyiwa matibabu katika hospitali moja nchini ingawa hawajui ni ipi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii