Kukumbatiana ni salamu inayoenziwa na Wanyarwanda
- Yves Bucyana
- BBC Africa, Kigali

Katika salamu ya wanyarwanda kiwango cha kumkumbatia mtu ni sawa kwa kila unaemkumbatia unapomsalimia
Kukumbatiana ni ishara kuu ya salamu ya watu wa kabila la Wanyarwanda, salamu hii ikiwa ishara ya furaha na upendo miongoni mwa watu wa jamii hii.
Salamu hii ni ishara ya furaha na upendo miongoni mwa watu wa jamii hii.
Huenda likawa jambo lisilo la kawaida kwa baadhi ya jamii nyingine za Afrika mashariki yako ikiwemo kwa mtu kumkumbatia mtu yeyote anayekutana naye barabarani, lakini kwa jamii ya Wanyarwanda ni jambo la kawaida.
Ni nani anayekumbatiwa?
Kukumbatiana katika utamaduni wa Wanyarwanda ni ishara ya upendo na furaha ya ndani ya moyo ambayo mtu anakuwa nayo kwa mtu mwingine
Salaam hii ambayo ni ya jadi imekua ikiendelezwa kizazi hadi kizazi na huambatana na maneno kama vile ''Amashyo'' ambapo anayekusalimia hukutakia kuwa na ng'ombe wengi na ''Yezu Akuzwe'' akimaanisha ''Yesu atukuzwe'' na maneno mengine mengi ya kutakiana kheri.
Kukumbatiana katika utamaduni wa Wanyarwanda ni ishara ya upendo na furaha ya ndani ya moyo ambayo mtu anakuwa nayo kwa mtu mwingine.'', anasema mtaalamu wa masuala ya utamaduni nchini Rwanda Profesa Malonga Pacifique.
Unaweza kumkumbatia mpenzi wako, baba yako, ndugu yako awe wa kike au wa kiume, baba mkwe, mama mkwe, mme mwenza, rafiki au tu mtu mwingine yoyote yule pale unapomkuta katika tukio au mahali popote mfano, katika familia, harusini, sokoni na hata njiani iwapo atakua na mtu unayemjua, hata kama binafsi haumfahamu.
Kiwango cha kumkumbatia kwa kawaida huwa ni sawa kwa kila unaemkumbatia.
Utamaduni wa kukumbatiana unavyotekelezwa na tamaduni za kisasa?
Professa Malonga anasema hata iweje salamu ya kukumbatiana kamwe haiwezi kupotea kwa sababu ya umuhimu wake katika utamaduni wa wanyarwanda
Kutokana na mabadiliko na muingiliano wa tamaduni mbalimbali za kigeni kiwango, baadhi ya Wanyarwanda wanaoishi maeneo ya mijini wameanza kubadili mtindo wa salamu hii, wakijaribu kutosogeleana sana kimwili na baadhi wakiiga salamu za kawaida za kisasa kama kusalimiana kwa mikono au mabega hasa miongoni mwa vijana.
Hata hivyo wenzao wa maeneo ya vijijini bado wanaendelea kukumbatiana kwa ukaribu wa miiili yao, kulingana na mila yao.
Professa Malonga anasema hata iweje salamu ya kukumbatiana kamwe haiwezi kupotea kwa sababu ya umuhimu wake katika utamaduni wa Wanyarwanda, huku akilinganisha aina nyingine za salamu na anazoziita za unafiki:
''Watu wengine wanakutana na kupeana mabusu, mwingine utamuona akiinama au anachuchumaa.
Kwangu mimi salamu hizo ambazo zinatajwa kuwa za kisasa naziona kama za kinafiki'', anasema profesa Malonga.
Je vijana wanasemaje kuhusu salamu ya kukumbatiana?
Vijana hasa kutoka vyuo vikuu ambao walizungumza na BBC wanasema kwamba kuna aina nyingi za salamu ambazo hukinzana na utamaduni lakini si kwamba kukumbatiana hakupo tena.
Vijana wengi siku hizi wameiga salamu wanazoona kwenye filamu za Kimarekani, kusalimiana kwa mikono huku wakikutanisha mabega au pia kwa kugongeshana ngumi.
Si kwamba tunapenda aina hizi za salamu.
Ni kufuata tu mambo ya kisasa kama tunavyoona kwenye filamu za Kimarekani.', Anasema, Emmanuel Hakizimana mwenye umri wa miaka ,23, kutoka chuo Kikuu cha Elimu nchini Rwanda (KIE).
Vijana wengi siku hizi wameiga salamu wanazoona kwenye filamu za kimarekani, kusalimiana kwa mikono huku wakikutanisha mabega au pia kwa kugongeshanana ngumi
Bwana Emmanuel anakwenda mbali na kusema kwamba baadhi ya watu hivi karibuni wamua wakiogopa salamu ya kukumbatiana au hata kupeana mikono kwa hofu ya kuambukia magonjwa.
''Wakati mwingine watu wanaogopa magonjwa ya kuambukiza kama Ebola hasa katika maeneo yaliyoko karibu na nchi ya Congo, utakuta kwamba kukumbatiana ni nadra sana siku hizi''
Umuhimu wa kukumbatiana
Mtalamu wa Saikolojia Grace Destiny, anasisitiza kuwa kukumbatiana ni zaidi ya salamu, kutokana na kwamba kukumbatia mtu kunafanya mawasiliano yanayowasilisha moja kwa moja hisia za upendo baina ya watu wanaokumbatiana.
Bi Destiny ambaye ni mtalamu wa saikolojia ya mahusiano na familia, anasema kukumbatiwa ni ishara ya kukubalika na salaamu hii zaidi ina manufaa kwa jinsia ya kike.
Mwanamke pamoja na mtoto wa kike wanahitaji kukumbatiwa jinsia ya kiume na pale wanapokosa kukumbatiwa huwa wanakuwa na hisia za utupu.
''Mtu anapokumbatiwa hujihisi kuwa na hakikisho la juu la usalama wake na hii hufanya atulie kiakili.'' Anasema Mwanasaikolojia Grace Destiny na kusistiza kuwa wazazi wa kike na kiume wanapaswa kuwakumbatia watoto wao wanapokua, ili kuwaepusha na hisia za utupu ambazo ambao watataka zijazwe na watu wengi.
Chanzo cha picha, Grace Destiny
Mtaalamu wa saikolojia Bi Grace Destiny Anasisitiza kuwa wazazi wa kiume wawakumbatie watoto wao wa kike kwani huwajengea uwezo wa kujiamini na kuhisi upendo wa baba zao
Akisisitiza juu ya umuhimu wa mgusano wa mwili kwa njia ya kukumbatiwa : '' Kukumbatiwa ni muhimu sana kwa mfano mwanamke ambaye ananyanyaswa na mume wake, anaweza kuliwazwa au kubembelezwa tu kwa kukumbatiwa na hiyo ikamfanya asahau unyanyasaji aliotendewa na mumewe'', anasema Mwanasaikolojia.
Anasisitiza kuwa wazazi wa kiume wawakumbatie watoto wao wa kike kwani huwajengea uwezo wa kujiamini na kuhisi upendo wa wazazi wao wa kiume.
Bi Grace Destiny, anasema: ''Kwa jamii kama ya Wanyarwanda, kukumbatiana kunaimarisha hisia za Umoja wa kijamii, na familia ya kibinadamu kwa ujumla, mgusano wa kimwili hasa kwa jinsia tofauti ni muhimu sana''.
Anasema, kukumbatiana hujenga hisia za udugu wa kaka na dada miongoni mwa jamii kama ya Wanyarwanda na kujihisi wako salama.
Nadharia mbali mbali kuhusu faida za kukumbatiana.
- Kukumbatiana huongeza uwezo wa kinga ya mwili na kupunguza magonjwa ya moyo mbali na kupunguza homoni za Cortisol zinazosababisha msongo wa mawazo (stress).
- Kwa watu wanaokumbatiana mara kwa mara kwa muda wa sekunde kati ya 15 na 20 huwezesha miili yao kuongeza kiwango cha homoni za Oxytocin ambazo huimarisha mahusiano na kuimarisha urafiki zaidi.
- Utafiti uliofanywa na taasisi ya Marekani ya magonjwa ya akili unaonyesha kuwa kukumbatiana au kusalimiana kwa mikono kunaweza kusamsaidia mtu kupunguza msongo wa mawazo na athari zake.
- Kukumbatiana humfanya mtu ajiamini kwani mtu anapomkumbatia mtu mwingine na kumuona akiwa mwenye furaha huwafanya wote wawili kujihisi wanajiamini.
- Kukumbatiana hutoa funzo la kupenda na kupendwa, na pia kutambua kuwa kila binadamu anamuhitaji mwenzake.
- Huwafanya watu kutojifikiria wao peke yao na kuwafikiria watu.
- Iwe kwa baina ya wapenzi, ama wazazi na watoto wao, au baina ya watu wengine kukumbatiwa humfanya mtu ahisi anapendwa na kuwa mwenye furaha maishani mwake
Chanzo cha picha, Reuters
Baadhi ya Wanyarwanda hasa wanaoishi maeneo ya mpakani na DRC hivi karibuni wameanza kuhofia kusaliamiana kwa kukumbatiana au kumsalimiana kwa mkono kwa hofu ya maambukizi ya Ebola
Hata hivyo, kukumbatia kunaweza kuleta madhara pale unapomkumbatia au kukumbatiwa na mtu mwenye maradhi ya kuambukiza kama vile Ebola na mengine yanayoweza kuambukizwa kwa njia ya kukumbatiana au kusalimiana kwa mikono.
Kutokana na maambukizi ya Ebola katika nchi jirani ya Jamuhuri ya Kedemokrasi ya Kongo, Wanyarwanda hususan wale wanaoishi katika maeneo ya mipaka na DRC wamekuwa na hofu ya kusaliamiana au hata kukumbatiana na watu wasiowajua, licha ya kwamba salamu yao ya kukumbatiana ni vigumu kuiacha.

Utamaduni wa sherehe za kumtoa mwari una maana gani Tanzania?
Katika baadhi ya mikoa kusini na ile ya Pwani mwa Tanzania suala la binti kupatiwa mafunzo maalumu ya kimila na desturi ambayo si geni, wao wanaiita kumtoa mwari.