Kuna umuhimu gani kwa wanawake wa Uganda kupiga magoti wakisalimia na kukaribisha chakula

Kupiga magoti
Maelezo ya picha,

Utamaduni wa kupiga magoti, Uganda

Licha ya utamaduni wa wanawake wa jamii ya Baganda kupiga magoti mbele ya wanaume kukosolewa kuwa kitendo kinachowadunisha watu wa jinsia hiyo, wanawake wa jamii hiyo na hata wa jamii zingine za Uganda wangali wanahisi kwamba ni desturi ambayo inamfanya yeye kuheshimiwa na wanaume na kuwa mwenye hadhi kama mwanamke.

Hivyo kuwapigia wanaume magoti ni hiari ambayo wanawake wengi wanazingatia hata wakipata elimu ya juu lakini bado wanakumbatia utamaduni wa kimagharibi.

Lakini je, ni nini jadi ya utamaduni huu? Katika hadithi na hekaya za Baganda mwanamume ndiye ana wajibu wa kumtunza na kumpenda mkewe na kumhurumia kiumbe yeyote wa kike.

Kwa upande wake mwanamke anamtarajia mwanamume kumfanyia hayo naye amtimizie yale ambayo hawezi kujifanyia yeye.

Hivyo kitendo cha kupiga magoti hakilengi kuendeleza taasubi za kiume na utamaduni lakini kuendelea kuwakumbusha viumbe hao wawili kwamba wana majukumu ambayo yanamhusu kila mtu kumtegemea mwenzake.

Maelezo ya picha,

Mwandishi wa BBC, Issack Mumena akipokea kikombe cha maji

Mwanamuke Mganda awe ameolewa ama hajaolewa ni jambo la utamaduni kumuamukia mtu akiwa amepiga magoti hadi chini, iwe anampatia mtu mkubwa kitu au kumsalimia.

Mwanamke Mganda akiwa ameolewa ndiyo zaidi maana kila mumewe anapotaka kitu kwa mfano, maji ya kunywa chakula ni lazima apige magoti anapoweka chakula menzani aidha anapompatia mumewe.

Mwanamuke Mganda aliyeolewa ana majukumu makubwa kwa mumewe kama anafanyakazi za ofisi au biashara, mara anapotoka nyumbani kwenda kazini ni shariti mwanamke Mganda ampigie magoti na kumtakia kazi njema na siku njema.

Akirudi kutoka kazini anampigia magoti mlangoni wakati anafunguwa mlango kumkaribisha mumewe na kuchukua mfuko wa mume wake aliokuja nao au chochote alichokuwa amebeba.

Pia watoto wadogo, baba anaporudi kutoka kazini wote wanakuja sebuleni alikofikia kumsalimia na wote wanapiga magoti kutoka mtoto mdogo wa miaka mitatu hadi juu.

Cristine Namukasa amenifahamisha kwanini wanawake wanapiga magoti, anasema mwanamke yoyote wa kabila la Baganda ni lazima apige magoti kuonyesha ishara ya heshima katika mila na destruri za Baganda, hii ni kumuonyesha mwanamke ametulia.

Kwani katika mila mwanamke hatakiwi kuzungumza kama amesimama hata anapozungumza sauti yake inaonyesha unyenyekevu.

Lakini Namukasa ameongeza kuwa kunatakiwa kufanyiwa mabadliko kidogo, kwa mfano unapokutana na mtu sehemu kama barabarani, vituo vya magari katika msongamano wa watu wengi wasipige magoti aidha utamaduni unatakiwa kukuzwa na vizazi vijavyo kwani vinaonyesha heshima ya mwanamke Muganda.

Utamadani huu wa kabila la Baganda karibu umesambaa sana katika makabila mengine nchini Uganda na wao wanapiga magoti wanaposalimu watu wakubwa kwa mfano Baba, Mama na wengine wenye umri mkubwa.