Je unaweza kusherehekea vipi msimu huu bila kuvuruga bajeti yako?

xmas

Siku kuu ya Krismasi inakaribia na kila mmoja yuko mbioni kuhakikisha msimu huu wa sherehe unakuwa wa kufana kwani ni muda wa kujumuika na ndugu jamaa na marafiki.

Kwanza kabisa hakikisha unatumia muda huu kufurahia kadiri ya uwezo wako lakini usitumie fedha ambazo huna mfukoni.

Wataalamu wa masuala ya kifedha wanasema kama ulitenga fedha kando kwa ajili ya sherehe ya Krismasi na mwaka mpya basi unaweza kusafiri na kuzitumia fedha hizo bila hofu.

''Hii ni safari,''anasema mshauri wa wa masuala ya fedha ambaye pia ni mwenyekiti na mwanzilishi wa Taasisi ya Centonomy ambayo hutoa mafunzo kuhusu jinsi ya kutafuta fedha na kuekeza fedha hizo.

Lakini kwa nini kila baada ya msimu wa sherehe watu hasalia na madeni na wengine kuuza vitu vyao vya thamani kujikimu mwezi wa Januari?

''Tatizo linakuja pale ambapo unafanya maamuzi ya dakika za mwisho kuhusu mipango ya sherehe ambayo hukuwa nayo,'' anaendelea kusema Bi Waceke:

Na kuongeza kuwa ''watu wanakurupuka dakika za mwisho kufanya mipango ya sherehe na kutumia fedha zao kiholela''.

Je unawezaje kusherehekea bila kuwa na hofu kwa kutumia fedha ambazo hukupangia?

Kujibu swali hili, Bi Waceke Nduati anasema ni vyema kuelewa maana halisi ya Krismasi.

Kwenda kujivinjari wakati wa krismasi au wakati mwingine wowote kunahitaji maandalizi ya hali ya juu.

Kwa mtazamo wake anasema Krismasi inahusu kusherehekea na watu uwapendao na kuongeza kwamba kuna njia nyingi sana ya kusherehekea na watu uwapendao bila kujiingiza kwenye madeni ambayo yanaweza kuepukika.

Pia anaongeza kuwa ni wakati mzuri wa kusoma kitabu, kujifunza kitu kipya kama vile mapishi alimradi ni kitu ambacho kitakuepusha na gharama zisizokuwa na maana kama kwenda maeneo ya burudani kutumia fedha ambazo huna kwa wakati huo.

Bi Waceke pia anashauri usichukue deni kwa ajili ya kusherehekea kwasababu deni inamaana kuwa huna uwezo wa kununua unachotaka kwa nafasi yako.

Jinsi ya kutengeza bajeti ya krismasi

  • Wataka kutumia pesa ngapi
  • Orodhesha majina ya watu unaotaka kuwanunulia zawadi
  • Tumia pesa ulizotenga kununua zawadi hizo
  • Lipia kila unachotaka kunua kwa pesa tasilimu usikopeshe.

''Watu wengi hujipata katika madeni kutokana na sababu wanataka kushindana na wenzao, kwa mfano kama jirani yako anaenda kujivinjari Dubai, usidhubutu kushindana na mwenzako kwasababu hujui anakotoa fedha zake'' anasema Waceke

Kwanza jielewe wewe na uhusiano wako na hela.

Kile unacholipwa si hoja cha msingi ni uwezo wako wa kuweka akiba. Ikiwa huwezi kuweka akiba kutokana na kidogo unachopata hata ukipata kikubwa hutaweza kuweka akiba.

Kabla ya kusherehekea

Mwezi Januari unakuja na gharama zake ni vyema kuzingatia vidokezo vifuatayo:

  • Tenga fedha za kugharamia huduma zote muhimu kama vile kodi ya nyumba, karo ya shule na chakula.
  • Bima ya gari lako na bima ya afya ikiwezekana lipa moja kwa moja ikiwa unahofia huenda ukazitumia fedha hizo.
  • Zitakazobakia tumia kuwafurahisha watu uwapendao katika maisha yako.
  • Kusherehekea sio lazima usafiri unaweza kuwa nyumbani na watoto wako ukaamua kuwapikia haswa kama wewe ni mama anaefanya kazi... tumia muda huu wa sherehe kujumuika na familia yako.
  • Jiulize kwa nini natumia pesa hizi zote...je nazitumia kufurahisha watu au kujifurahisha?

Mwisho Bi Waceke Nduati anasema, sawa na jinsi unavyosuluhisha tofauti katika uhusiano wako na watu ndivyo unavyotakiwa kusuluhisha tatizo la utumizi wa fedha katika maisha yako.

Unaweza pia kusoma: