Je, Ethiopia ilipanda miche ya miti bilioni 4 mwaka huu?

  • Na Peter Mwai
  • BBC Reality Check
Watoto wakipanda miti Ethiopia

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mamilioni ya watu Ethiopia walishiriki kampeni ya kupanda miti nchini humo kwa lengo la kuvunja rekodi

Ethiopia ilitekeleza mradi mkubwa wa upanzi wa miti mwaka huu, ikiwa na lengo kubwa la kupanda miti bilioni nne katika kipindi cha miezi mitatu pekee.

Hatua kuu katika kipindi hicho ilikuwa tarehe 29 Julai raia nchini humo walipojitokeza kushiriki katika upanzi wa miti kwa lengo la kuvunja rekodi ya dunia.

Mwisho wa siku walipanda miche ya miti 350 milioni kwa mujibu wa serikali.

Mwishoni mwa Agosti, serikali ilidai kwamba ilikuwa imetimiza malengo yote mawili, lakini je inawezekana kupanda idadi kubwa hivyo ya miti katika kipindi kifupi hivyo?

Upo ushahidi gani kwamba malengo hayo yalitimizwa?

Ethiopian Water and Energy Minister, Seleshi Bekele.
Getty
Tumetimiza malengo yote mawili tuliyojiwekea....tumejifunza mengi pia kutokana na mradi huu kuhusu ukuzaji wa miti nchini.
Seleshi Bekele
Waziri wa Maji na Kawi, Ethiopia

Kampeni hiyo iliiyokuwa imepewa jina Mkakati wa Urithi wa Kijani, ilikuwa unaongozwa na kupigiwa debe na Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliyeshinda Tuzo ya Amani ya Nobel hivi majuzi.

Wengi wamekuwa wakiangazia sana mradi huu kwa makini kwani wanasiasa katika mataifa mengi duniani wamekuwa wakiitaja Ethiopia kama mfano wa kuigwa katika upanzi wa miti katika mataifa yao.

Aidha, Ethiopia imetajwa kama mfano bora katika juhudi za kupunguza madhara ya ukataji wa miti na mifumo duni ya kilimo inayoharibu mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwezi huu nchini Uingereza, vyama vikuu vya siasa viliahidi kupanda mamilioni ya miti, na kuitaja Ethiopia kama kielelezo.

Chama cha Leba kiliahidi kupanda miti bilioni mbili kufikia mwaka 2040, nacho chama cha Conservatives kikaahidi kupata miti 30 milioni zaidi kila mwaka. Chama cha Kijani kiliahidi kupanda miti 700 milioni kufikia 2030.

Canada ina mpango wa kupanda miti bilioni mbili katika kipindi cha miaka 10.

Kuvunja rekodi

Tutathmini kwanza shughuli ya siku moja ya kujaribu kuvunja rekodi.

Lengo lilikuwa kupanda miti 200 milioni maeneo mbalimbali nchini humo 29 Julai.

Baada ya shughuli hiyo kukamilika, serikali ilitangaza kwamba walifanikiwa kupita lengo hilo kwa mbali, ambapo walipanda zaidi ya miche 350 milioni katika kipindi cha saa 12.

Walitangaza idadi kamili ya miti hiyo - miche 353,633,660.

Lakini GWR waliambia BBC kwamba bado hawajapokea ushahidi wowote kutoka kwa serikali ya Ethiopia kuhusu jaribio hilo.

"Kwa hivyo, tunawahimiza waandalizi wawasiliane nasi kuhusiana na hili ili kundi letu la Watathmini wa Nyaraka na Stakabadhi waweze kuutathmini," alisema msemaji mmoja wa Guinness World Record Jessica Spillane.

Afisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia ilikataa kuzungumzia takwimu hizo na kusema kwamba taifa hilo tayari limejibu mengi ya maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa kuhusu upanzi huo wa miti.

Kwa maelezo zaidi kuhusu tuliyobaini kuhusu yaliyotokea siku hiyo ya upanzi, soma makala hii nyingine ya Reality Check hapa..

Chanzo cha picha, Girmay Gebru, BBC

Maelezo ya picha,

Miti iliyopandwa inahitaji maji kunawiri katika mazingira magumu

Inawezekana kupanda miti bilioni nne?

Sasa, tutathmini mpango wa kupanda miti bilioni nne katika kipindi cha miezi mitatu.

Hiyo ni sawa na kupanda miti 45 milioni kila siku.

Ukiondoa siku ya kuvunja rekodi ambapo miti 350 milioni ilipandwa siku moja, basi utabaki na idadi ya miti 40 milioni inayohitajika kupandwa kila siku.

Ukiangalia kwa mtazamo mwingine, Ethiopia ina raia 105 milioni hivi. Itahitaji kila raia kupanda miche 40 katika kipindi hicho cha miezi mitatu kutimiza lengo hilo.

Serikali ilisema mpango ulikuwa kupanda miti katika ardhi ya ukubwa wa hekari 6.5 milioni maeneo ya mashambani, pamoja na maeneo mengine ya mijini.

Ukichukulia idadi ya wastani kwamba unaweza kupanda miti 1,500 kwenye hekari moja, ardhi iliyotengwa Ethiopia inatosha kupanda miti hiyo bilioni nne.

Lakini hilo halijasema lolote kuhusu idadi hasa ya miti iliyopandwa kipindi hicho.

Takwimu pekee tulizo nazo zimetolewa na serikali ya Ethiopia yenyewe.

Kwa mujibu wa takwimu hizi, miti iliyopandwa ni 3.5 bilioni katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Juni hadi mwisho wa Agosti.

Mwishoni mwa mwezi Agosti, Waziri wa Kilimo Oumer Hussein alisema miti 3.7 bilioni ilikuwa imepandwa.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuna miche 1.3 bilioni iliyokuwa imetayarishwa lakini haikuwa imepandwa kufikia mwisho wa Agosti.

Lakini je, kuna njia yoyote ambayo inaweza kutumiwa kuthibitisha takwimu hizi za serikali?

Chanzo cha picha, Getty Images

Utahesabuje miti mingi kiasi hiki?

Hautuwezi kuhesabu miti yote hiyo sisi wenyewe, japo tulimtuma mwandishi wetu katika eneo moja lililopandwa miti hivi karibuni ili kupiga picha miche ambayo inapata wakati mgumu katika eneo kame la Tigray, kaskazini mwa nchi.

Pengine picha za setilaiti zinaweza kutoa suluhu. Tuliwasiliana na kampuni moja ambaoy hutoa picha za kina za kutoka angani za maeneo mbalimbali. Wao walituambia kuwa miche hiyo itakuwa ni vigumu kuitambua maana ni shida kuitofautisha na nyasi zinazozizunguka.

Tuliwasiliana na mtaalamu wa mazingira Tim Christophersen anayeratibu masuala ya miti na misitu na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika Umoja wa Mataifa.

Hakutoa jibu kamili lakini alisema amefurahishwa na kujitolea kwa Ethiopia katika upanzi wa miti.

Alisema Ethiopia imeahidi kurejesha misitu katika ardhi ya ukubwa wa hekari 15 milioni kufikia mwaka 2030, kama sehemu ya "Ahadi ya Bonn".

"Ethiopia imeomba usaidizi wa jamii ya kimataifa katika upanzi, na muhimu zaidi katika utunzaji wa miti," aliambia BBC.

Inaonekana wazi kwamba azma ya Ethiopia kupanda mabilioni ya miti imesifiwa na wahifadhi wa mazingira, lakini hakujakuwa na juhudi za kina za kutathmini idadi ya miti ambayo imepandwa mwaka huu.

Sehemu ya tatizo ni jinsi idadi ya miti inayopandwa inavyojumlishwa.

Julai, EU na serikali ya Ethiopia zilitia saini makubaliano ya ufadhili wa kifedha ya €36 milioni kusaidia taifa hilo la Afrika kukuza miti na kuhifadhi misitu.

Mashirika ya ndani ya nchi yamekabidhiwa fedha za kufadhili upanzi wa miti maeneo mbalimbali na si ajabu kwamba inawezekana baadhi yamekuwa yakiripoti idadi ya miti iliyotiwa chumvi kufurahishwa wakubwa wao. Idadi ya miti wanayosema walipenda huenda inajumlishwa na kutangazwa kuwa idadi ya miti iliyopandwa kitaifa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Tree planting needs to be balanced against the need for farmland

Changamoto

Bila kujali idadi kamili ya miti iliyopandwa, bila shaka Ethiopia imefanya juhudi kubwa kukabiliana na uharibifu wa misitu na kupanda miti.

Nusu karne iliyopita, Ethiopia ilifunikwa na misitu kiasi cha asilimia 40. Leo hii kiasi hicho ni asilimia 15.

Ili mpango wa upanzi wa miti uliofanywa mwaka huu ufanikiwe kuongeza kiwango hiki, basi miche iliyopandwa itahitaji kutunzwa kwa makini na kumwagiliwa maji mara kwa mara.

Serikali imekuwa ikiwahimiza raia kutunza miti waliyoipanda, lakini hili litatosha?

Itahitaji kutumiwa kwa kiasi kikubwa cha maji ambayo ni adimu katika baadhi ya maeneo lakini pia huenda miti hii ikachangia kuwepo kwa mazingira yanayorahisisha uhifadhi na upatikanaji wa maji.