Oloni: 'Wanaume hawafurahishwi na hatua yangu ya kusaidia kina dada kimawazo'

Dami Oloniskin

Chanzo cha picha, BBC3

Maelezo ya picha,

Kina dada sikilizeni! Dami Oloniskin

Awe kwenye kilabu au ananunua visodo, Dami Oloniskin mwenye umri wa miaka 29, kutakuwa na mtu anayetafuta ushauri wake kuhusiana na maisha ya kuwa na mchumba.

"Huwa najipata nikimwambia mtu, sikiliza, kwa sasa niko katika shughuli zangu!'' Mwanablogu huyo anayefahamika kama Oloni na mashabiki wake, anacheka, ''Jana, nilienda kwenye duka la kununua dawa na kwa haraka haraka nikanunua sababu za kuoga na za kuosha nyewele, ghafla nikasikia mtu akiniita, Samahani wewe ni Oloni?'"

Oloni mwenye ushawishi mkubwa ni shangazi anayewafunda wasichana wengi. Karibia watu elfu 200 wanamfuatilia katika ukurasa wa Instagram and Twitter (CLAP BAQ QUEEN @Oloni), pamoja na (@LaidBarePodcast) na pia ana kipindi anachoendesha katika runinga.

Anapendwa kutokana na ukweli anaoangazia wakati anajibu maswali ya mashabiki wake kuhusu masuala ya uhusiano na mapenzi.

Kwa sasa anapatikana katika mtandao wa Twitter ambapo mashabiki wake wanamuandikia simuli zao nzuri na za kuvutia kuhusu mapenzi jambo ambalo limemfanya kuwa sauti na mtu wa kutegemewa na wanawake vijana.

Lakini siyo kila mtu anayefurahia hilo.

Je kinachowachukiza wapenzi kiume ni kipi?

Maelezo ya picha,

Oloni anatoa majibu kuhusu maswali ya mapenzi bila kuficha lolote

"Wanaume wengi wanapata hofu kwa jinsi nilivyo na uwezo wa kuwasiliana na idadi kubwa ya wanawake. "Nafikiri hawafurahishwi na ukweli wa kwamba ninapata fursa ya kuwafunza na kuwaelimisha wanawake namna ya kufanya maamuzi sahihi katika masuala ya ngono pamoja na kuwapa maarifa ya kuongeza mahaba."

Oloniskin alianzisha blogu yake kuangazia masuala ya ndoa na mahusiano mwaka 2008 alipokuwa kijana.

Lakini wakati huo, alikuwa akiandika kuhusu maisha yake na mpenzi wake, anasema, na kuangazia masuala ambayo hayakuwa rahisi kuzungumziwa kwa uwazi nchini Nigeria hasa katika familia za Kikiristo.

"Nilikuwa nafurahia sana kuzungumzia masuala ya ngono na kutaka kuelimisha wanawake kwasababu nilihisi hili ni suala ambalo halizungumziwi hasa katika jamii zetu,'' anasema.

"Watu wanafikiria kwamba ukipenda kuzungumzia mambo ya mapenzi moja kwa moja, watu wanadhani wewe ni bingwa wa ponografia. Huo si ukweli. Hii inamaanisha kwamba unaufahamu mzuri wa suala lenyewe, suala la mapenzi unaliangalia kwa mtazamo chanya na unataka kufahamisha wanawake wengine wanaokuzunguka.''

Zaidi ya miaka 10 sasa, mwanadada huyo anapokea zaidi ya maombi 100 kutoka kwa watu wanaotaka ushauri kuhusu masuala ya ngono, na namna ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu ambaye utamaduni wake ni tofauti na yeye.

Anajibu watu katika mtandao wa Instagram, kupitia blogu yake na pia anatoa ushauri kwa njia ya simu kwa malipo fulani, ili kuzungumza na watu wanaopitia changamoto katika mahusiano yao.

Kwenye Blogu, Twitter... na sasa napatikana katika Televisheni

Maelezo ya picha,

Oloni akitoa ushauri wa kimapenzi kwa rafiki yake Yazmine, Tyler (kushoto) kwenye kipindi chake cha televisheni kinachofahamika kama ''My Mate's A Bad Date''

Katika kipindi chake kipya katika kituo cha televisheni cha BBC Three, kinachofahamika kama ''My Mate's a Bad Date'', anawashauri wanawake ambao hawajaolewa kwa njia ya simu, namna ya kudumisha uchumba.

Wakati Oloni anatoa ushauri wa maswali aliyoulizwa, akaelewa kwanini baadhi ya wanaume ambao wachumba wao wanamfuata kwenye mtandao wa kijamii hawako radhi naye.

Moja ya simulizi iliyomshangaza ilikuwa ni ya yule mwanamke aliyempigia simu baada ya kugundua ameambukizwa magonjwa ya zinaa.

"Dada mmoja aliniambia kwamba amemuuliza mpenzi wake kuhusu ugonjwa wa zinaa aliyejipata nao baada ya kufanya mapenzi naye, mpenzi wake akamjibu kwamba, 'Pengine uliupata kupitia matumizi ya choo'," anakumbuka alivyomjibu hewani. 'Hapana huyo ni mwongo'."

Oloni anachukulia simulizi hizi kama ushahidi wa kwamba suala la ngono halizungumziwi kikamilifu.

Hiyo ni moja ya sababu iliyomfanya aanzishe blogu yake. Anasema alitaka kuanza kuzungumzia kwa uwazi masuala kama magonjwa ya kuambukiza na vile wanawake wanavyoweza kujitosheleza kimapenzi.

"Nahisi kwamba kwasababu ya hilo, wanawake wengi hasa kutoka jamii yangu, wanajadiliana masuala hayo bila wasiwasi na wanapokutana na mimi, wananiambia kwamba, kama si mimi, hangewahi kupata ujasiri wa kuwaambia wapenzi wao fikra zao kwa uwazi - kwa hiyo nafurahi kusikia mabadiliko yameanza kushuhudiwa."

Vile Oloni kutoka jamii ya kikirsto, Nigeria, alikuwaje mshauri wa masuala ya ngono?

Maelezo ya picha,

"Kumlazimisha mtu siyo kupata idhini yake," anasema Oloni, ambaye haogopi kuwauliza wanawake na wanaume tofauti iliyopo kati ya maneno hayo mawili

Dada huyu mwenye umri wa miaka 29, kwa sasa ana uhusiano mzuri na kina dada wanaomzidi umri na maelfu ya wanawake wengine, lakini anasema kwamba elimu ya ngono anayotoa ilimfanya atengwe na Kanisa lake.

"Hili huwa nalifananisha na filamu ya Marekani ya Mean Girls, ambapo mshauri anasema, 'Ukifanya mapenzi utakufa,' anasema.

"Nakumbuka walivyonikalisha na kunishauri kwamba niachane na mpango huu wa kufunza wanawake kuhusu ngono? kisha wakatupa mipira ya kondomu na kutuambia kwamba tusijaribu kuwataja.''

Na alipotambua athari ya kufunza elimu ya ngono kwa namna hii, mwanablogi huyu amekuwa akitoa ushauri katika shule za upili ambako mwito wake umepokelewa vizuri.

Oloni anasema mafunzo kuhusu idhini ya kukubali kufanya ngono inastahili kuendelezwa: ''Mfano ni kwenye vilabu, unapotembea mbele ya mtu, kisha akakushika kiuno, ama kama anataka kucheza na wewe lakini hakubali kuwa wewe huna haja na hilo, mambo yote haya yapo chini ya 'idhini', na hayo ndiyo mazungumzo tunayokuwanayo mashuleni."

Kutoa idhini kwa kuridhia ni nini?

Maelezo ya picha,

Akizungumzi vile idhini ni jambo la msingi katika ngono

Mwanablogi huyo anakumbuka wakati alipowaeleza wanafunzi kuhusu visa mbalimbali na kuwaomba wanyooshe mikono yao juu iwapo wanaona kisa anachowasimulia je musika alitoa idhini au la.

"Kundi moja la wasichana lilisema, 'Ndio, idhini ilitolewa, huku kundi jingine likipinga na kusema kwamba hapo, muhusika hakutoa idhini kwasababu maneno ya kijana yalichangia msichana kubadili mawazo yake'," anasema.

"Kwa hiyo walielewa kwamba kumlazisha mtu, siyo sawa na kutoa idhini kwa kuridhia."

Anasema hili ni jambo ambalo yeye hakulifahamu akiwa na umri kama huo: "Bila shaka ningesema, ndiyo alitoa idhini yake kwasababu alikubali,".

Dhana ya kuwa na furaha milele

Je ni kitu gani kimoja tu ambacho Oloni anatamani angekifahamu wakati akiwa kijana kuhusu ngono?

"Kufanya mapenzi na mtu hakumaansishi kwamba mutapendana na kuwa na furaha milele."

"Nakumbuka nilipopoteza ubikira wangu, 'Nilidhani kwamba huyu ndiye atakuwa mume wangu," anasema.

"Unatakiwa kufanya mapenzi kujifurahisha wewe mwenyewe wala siyo kumfurahisha mwengine yeyote, na usifikirie kwamba kufanya hivyo, kutakupa hakikisho la kuwa na mtu huyo maisha yako yote."

Pia unaweza kusoma: