Francisco ouma:Mkenya anayemiliki pango kubwa akidai ni amri aliyopewa na Mungu

  • Faith Sudi
  • BBC Swahili
Francis ouma
Maelezo ya picha,

''Mungu aliniletea ramani katika ndoto, akanionyesha ramani ya pango na akaniamrisha nichimbe pango hili''

Francis ouma kutoka magharibi mwa Kenya anamiliki pango la vyumba 24 na kudai kwamba alichimba pango hilo baada ya kuamrishwa na Mungu.

Pango hilo liko mita chache kutoka nyumbani kwake.

Pango hilo lina milango miwili. Mlango wa kwanza ni wa mbao na unaelekea katika chumba kimoja kilichopo juu, kisha unateremka kwa ngazi karibu futi 3 chini ya ardhi ili uweze kuingia katika vyumba vilivyopo kwenye pango.

Maisha ya Ouma

"Nilianza kujenga nyumba hii Februari, mwaka wa 1967 saa sita za mchana. Mungu aliniletea ramani katika ndoto, akanionyesha ramani ya pango na akaniamrisha nichimbe pango hili. Siyo kwamba niliota… Hapana, ni Mungu mwenyewe aliyeniletea ramani"

Maelezo ya video,

Mkenya anayemiliki pango kumridhisha Mungu

Ndani ya pango hilo kuna giza totoro na lazima utumie taa kupata mwangaza.

Vyumba vyenyewe vinatofautiana kwa ukubwa na milango yake imetengenezwa kwa maumbo maalum yanayofanana na milango ya Kasri la zamani la Mfalme wa Misri.

"Unaona vyumba vingine ni vidogo na vingine ni vikubwa… hivi vyote vimejengwa kulingana na ramani ambayo nimepewa na naamini ni kwa sababu kila chumba kitakuwa na kazi yake. Ni sawa tu na vile nyumba ya binadamu huwa na vyumba kwa ajili ya matumizi tofauti tofauti. Vyumba vingine vinaweza kutumika kuhifadhi vitu. Kwa hiyo ni Mungu mwenyewe anayejua matumizi ya vyumba hivi"

Maelezo ya picha,

Ndani ya pango hilo kuna giza totoro na lazima utumie taa kupata mwangaza.

Mzee Francis ambaye ana umri wa miaka 73 anadai kwamba yeye huzungumza na Mungu moja kwa moja.

"Mungu ananipa taarifa zote nikiwa hapa. Anaweza kujitokeza kama mfano na akapotea. Kuna wakati kama nina chimba mahali ambapo hataki, yeye hunizungumzia na kusema niwachie hapo nisiendelee"

Hata hivyo ni kisa ambacho kiliwashangaza wazazi wa bwana Francis ambao sasa ni marehemu na hata wanakijiji walimwogopa sana.

"Watu walikuwa wananiangalia, nikienda mtoni kuoga, watu walikuwa wakinitizama kwa uwoga na kusema kwamba mimi nina chimba shimo la kuzikiwa siku nikifa… Lakini nikawaambia kwamba ninafanya kazi ya Mungu."

Maelezo ya picha,

Ndani ya pango hilo kuna jiwe lenye umbo la mstatili ambalo limenukuliwa amri tano

Mwaka 1979, Francisco alisitisha shughuli hiyo na akaenda mjini baada ya watu kumcheka na kusema kwamba atakufa bure bila boma lake kama wanavyoamini wanajamii wake kwamba mwanamume kamili lazima awe na mke na watoto.

"Nilienda mjini Eldoret na nikatafuta kibarua ambapo nilipata kazi ya ulinzi. Pia nikapata mchumba nikumuona na kwa sasa tumebarikiwa na watoto wanne. Tuliishi mjini kwa miaka 15, kisha nikaona kwamba ninapotea, sababu sikuwa nimemaliza kazi niliyokuwa nimepewa. Hivyo nikaamua kurudi na kuendeleza kazi ambayo nilikuwa nimepewa na Mwenyezi Mungu."

Ndani ya pango hilo kuna jiwe lenye umbo la mstatili ambalo limenukuliwa amri tano kwa wino mweusi na ambazo Francisco anadai alipewa na Mungu mwezi Juni mwaka huu.

Maelezo ya picha,

Amri kumi za pango la mzee Francis

'Niliamka siku moja asubuhi, nilipofika hapa pangoni nikapata nakala ya amri hizi tano zikiwa hapa chini, na nikajua tu ni agano ambalo Yesu Kristo mwenyewe aliahidi kwamba ataniletea. Kwa sababu alisema kwamba amri zile ambazo zilikuwa za Musa watu wameharibu."

Amri zenyewe ni hizi.

  • Umpende Mungu muumba.
  • Upende Yesu kwa dunia kufufuka peke yake.
  • Furahia mwanaadamu kwa kutengeneza pesa.
  • Kuna kabila mbili duniani, mke na mume
  • Abudu Mungu moja dunia moja.

Francisco anadai kwamba bado hajaonyeshwa hatima ya vyumba hivyo na anasubiri maono na kwamba kupatikana Kwa jiwe hilo la agano ni hatua ya kwanza.

"Hatua ya pili inakuja. Na hiyo siwezi kusema kwa sasa na nitangaze eti ni moto au kitu fulani… Hiyo nitakuwa ninamdanganya mwanadamu. Kwa hivyo ninasubiri ripoti ya mwisho nitakayopatiwa"

Maelezo ya picha,

Francisco anadai kwamba bado hajaonyeshwa hatima ya vyumba hivyo na anasubiri maono

Profesa Chacha Nyaigoti ni mwanasosholojianchini Kenya anachanganua kisa hiki Kisayansi.

"Mungu ni muweza na anaweza kuzungumza na binadamu yeyote. Lakini wakati mwingine watu hukurupuka na kujikuta wakitenda matendo yasiyoambatana na utaratibu wa maisha ya kawaida na ili kujieleza wanasema kwamba ni Mungu amewaagiza" anaeleza Profesa Chacha.

"Katika kisa kama hiki tunahitaji kuzingatia na kutathmini matendo ya miaka kadhaa ya awali ya watu kama hawa, utengamano wao na watu wengine kijijini na kudadisi iwapo yanaafikiana na mtu mwenye akili timamu ama anahitaji msaada kutoka kwa washauri wa matatizo ya kiakili. Na iwapo itapatikana kwamba ni matatizo ya kiakili basi kuna tiba."

Pia unaweza kusoma: