Sheria hiyo mpya inatoa uraia kwa wahamiaji haramu ambao sio waislamu

Mamia ya watu waandamana Mumbai , India

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mamia ya watu waandamana Mumbai , India

Maandamano yanayojumuisha mamia ya wakazi nchini India yamepigwa marufuku sehemu mbalimbali za mji wa Delhi, na katika majimbo ya Uttar Pradesh na Karnataka.

Huduma zote za simu zilisitishwa katika baadhi ya maeneo ya Delhi, karibu na eneo ambalo maandamano hayo yalikuwa yakifanyika.

Kumekuwa na mfululizo wa maandamano kwa siku kadhaa sasa nchini India, huku siku zingine zikijawa na vurugu kali.

Sheria hiyo mpya inatoa uraia kwa wahamiaji haramu ambao sio waislamu na wanaotoka katika nchi za Pakistani, Bangladeshi na Afghani tu.

Agizo la polisi lililotokana na sheria kali, linalopiga marufuku mkusanyiko wa watu zaidi ya wanne katika sehemu moja.

Lakini makumi na maelfu ya watu waliandamana katika mitaa ya miji ya nchi hiyo ikiwemo Delhi, Bangalore, Hyderabad, Patna na Chandigarh.

Wakati maandamano ya Alhamisi yamekuwa ni ya amani, hadi sasa watu wawili wamepelekwa hospitali wakikabiliwa na majeraha mabaya, baada ya ghasia kuzuka kati ya waandamanaji na polisi katika mji wa Mangalore, kulingana na kamishna wa polisi.

Vurugu kama hizi pia zimeripotiwa mjini Lucknow, mji mkuu wa Uttar Pradesh, ambapo mabasi yamechomwa.

Makundi ya asasi za kiraia, vyama vya kisiasa, wanafunzi, wanaharakati na raia wa kawaida waliweka msululu wa ujumbe wao katika mitandao ya instagram na Twitter, wakiwaomba watu wajitokeze na kuandamana kwa amani.

Kati ya watu waliokamatwa ni pamoja na mwanahistoria na mkosoaji maarufu wa serikali Ramachandra Guha, kutoka mji wa kusini wa nchi hiyo, Bangolore na mwanaharakati wa kisiasa Yogendra Yadav mjini Delhi.

Akizungumza katika kipindi cha BBC Newshour, Bwana Guha alikamatwa pamoja na mamia ya watu kutoka jamii mbali mbali, ''Hii inaonyesha kwa uwazi kabisa kuwa sehemu kubwa ya India hawakubaliani na sheria hii ya ubaguzi.''

Maelezo ya picha,

Mabasi yalichomwa moto katika mji wa Lucknow

Maandamano bado yanaendelea katika baadhi ya miji, kama vile Delhi na Bangalore, wkakati maelfu wakiwa wamektana mjini Munmbai. Waigizaji wa Bollywood na watengenezaji filamu wanatarajiwa kuungana na maandamano hayo mjini humo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Polisi wamekuwa wakiwasindikiza wanafunzi kuingia kwenye mabasi yao ya shule

Wakati huohuo polisi wameweka vizuizi katika njia inayounganisha Delhi na mji wa Jaipur, huku wakikagua magari yote yanayoingia katika mji mkuu.

Hii ilisababisha foleni kubwa na kusababisha waandamanji kuchelewa kupanda ndege.

Imeripotiwa kuwa kampuni maarufu ya ndege ya Indigo, ilihairisha safari 19 kwa sababu wafanyakazi wake walishindwa kufika uwanja wa ndege.