Somkid Pumpuang: Muuaji sugu wa Thailand atambuliwa kwa jeraha alilokuwa nalo

Somkid Pumpuang, alivyokuwa ametolewa kwenye picha za wanaotafutwa na polisi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Somkid Pumpuang, aliyekuwa katika orodha ya wanaotafutwa na polisi akamatwa kwenye treni

Wanandoa wamemtambua mtu mwenye visa vingi vya mauaji Thailand, alipokuwa kwenye treni kwasababu ya jeraha alilokuwa nalo kwenye paji lake la uso na kukamatwa na polisi.

Somkid Pumpuang, 55, aliachiliwa mapema mwezi Mei, wakati akihudumia kifungo cha maisha kwa makosa ya mauaji ya watu watano.

Hatahivyo, alirejeshwa katika orodha ya watu wanaotafutwa na polisi baada ya kushukiwa kumuua mtu mwengine wa sita eneo la Kon Kaehn Jumapili iliyopita.

Polisi huko Thailand walianzisha msako dhidi yake baada ya mauaji ya hivi karibuni ya mwanamke mwenye umri wa miaka 51, Ratsami Mulichan.

Je walimtambuaje?

Wanandoa hao vijana, ambao hawakutajwa kwasababu za kiusalama, walikuwa wameketi mkabala na Somkid walipokuwa kwenye treni saa 08:37 Jumatano asubuhi.

Mchumba wa kike ambaye alikuwa mwanafunzi alimtambua Somkid kwa jeraha kubwa alilokuwa nalo sehemu ya nyusi ya jicho la kushoto, ambalo lilikuwa sawa na lile la kwenye picha iliyotolewa katika orodha ya wanaotafutwa na polisi.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Police walivamia kituo cha treni cha Pak Chong na kumkamata Somkid

Wachumba hao waliondoka sehemu waliokuwa wameketi na kwenda sehemu nyengine lakini mchumba wa kike akamueleza mwenzie sababu zilizokuwa zinamtia wasiwasi, kisha akarejea tena sehemu aliyokuwa ameketi awali na kumpiga mhalifu huyo picha kisha akaituma katika kituo cha polisi.

Treni hiyo ilipowasili katika kituo kinachofuata cha Pak Chong saa 10:45, maafisa wa usalama walikuwa wameshawasili na moja kwa moja wakaingia katika behewa alilokuwa Somkid na kumkamata.

Mchumba wa kike alisema kwamba jeraha hilo "lilimthibitishia kwamba huyo ni Somkid", ameiambia Televisheni ya Thailand.

Somkid Pumpuang ni nani?

Kabla ya kukamatwa, polisi walimtaja Somkid kama "mwanamume hatari".

Maafisa hao wanadai kwamba Somkid alimuomba urafiki Ratsami Mulichan katika mtandao wa Facebook kwa kujidai kuwa yeye ni mwanasheria na kumtembelea nyumbani kwake Disemba 2.

Wiki mbili baadaye, alipatikana nyumbani kwake akiwa amekufa, kulingana na gazeti la Bangkok Post.

Pia unaweza kusoma:

Mwaka 2005 Somkid alishtakiwa kwa makosa ya mauaji ya watu watano.

Waathirika wote walikuwa wanawake ambao walikuwa ama waimbaji katika vilabu vya usiku au wakandaji wa mahotelini.

Mwaka 2012, mahakama ya rufaa ilimuhukumu Somkid kifungo cha maisha.

Hata hivyo, mwezi Mei mwaka huu alipewa kifungo cha nje baada ya kuonesha kwamba amerekebisha tabia alipokuwa gerezani.