Siasa za Tanzania: Mlima wa changamoto unaomkabili Freeman Mbowe kuelekea 2020

Mbowe na Zitto

Chanzo cha picha, Chadema

Ni matokeo yaliyotarajiwa, Freeman Mbowe ambaye amekiongoza chama kikuu cha upinzani Tanzania Chadema kwa miaka 15, amepewa tena ridahaa na wanachama kushikilia usukani wa chama kwa miaka mitano ijayo.

Upinzani dhidi yake kwa mwaka huu, kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita ulikuwa ni hafifu, akishinda uchaguzi huo uliofanyika Jumatano wiki hii alishinda kwa kishindo cha asilimia 93.5.

Baada ya kutangazwa mshindi, wafuasi wake kwa furaha wakamuimbia: "...tuvushe mwamba tuvushe."

Mwamba anayezungumziwa ni Mbowe, lakini awavushe kutoka wapi na kuelekea wapi ni jambo ambalo kila mtu anaweza kuwa na tafsiri yake.

Moja ya tafsiri inaweza kuwa kuwavusha kutoka kwenye changamoto zinazowakumba kwa sasa, na katika hilo changamoto ni za upinzani kwa ujumla.

Chadema ikiwa kama chama kikuu cha upinzani kiongozi wake anatazamwa pia kuwa kama kiongozi mkuu wa upinzani kwa ujumla wake.

Awamu hii ya nne madarakani kwa Mbowe inaanza zikiwa zimesalia wiki mbili tu uingie mwaka 2020, ambapo uchaguzi mkuu ambao unaweza kubadili sura ya upinzani mkuu unatarajiwa kufanyika. Mwaka huo utakuwa na changamoto lukuki ambazo tutaziangazia kwenye makala hii.

Uchaguzi Mkuu 2020

Kama uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwezi Novemba mwaka huu ni kioo cha kuakisi Uchaguzi Mkuu wa 2020 basi tufani ya kisiasa inaweza kutabiriwa kuwa ipo njiani.

Maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulikuwa unasimamiwa moja kwa moja na serikali ulikosolewa vikali na upinzani baada ya sehemu kubwa ya wagombea wake kukatwa majina yao kwa kilichoelezwa kuwa ni kukosa sifa baada ya kukosea kujaza fomu husika ama kuchelewa kuzirudisha.

Hatimaye, vyama vikuu vya upinzani vikiongozwa na Chadema vikatangaza kususia kura hizo.

Maelezo ya sauti,

CCM na upinzani Tanzania walaumiana juu ya uchaguzi wa serikli za mitaa

Msimamo wa serikali ya Tanzania ni kuwa uchaguzi huo ulifuata vigezo vyote vya kisheria na ulikuwa huru na wa haki.

Ni dhahiri kuwa mwenendo wa uchaguzi huo umekosolewa vikali na upinzani na wanaharakati, ukatiliwa mashaka na baadhi ya balozi za nje nchini Tanzania lakini umeondoa sura ya upinzani kwenye uongozi wa chini wa nchi.

Mwaka 2015 uliwkua mzuri kwa Chadema pamoja na upinzani kwa ujumla.

Chini ya mwamvuli wa umoja wa Ukawa, walimsimamisha waziri mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa ambaye alikihama CCM na kuingia Chadema kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho na kuungwa mkono na Ukawa.

Matokeo yakawa upinzani kupata uwakilishi mkubwa zaidi bungeni, na hata kwenye matokeo ya jumla licha ya kushindwa urais Lowassa alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.

Hata hivyo baadhi ya viti walivyoshinda 2015 wamevipoteza baada ya sehemu ya wabunge na madiwani wa upinzani kuhamia CCM katika kile walichokiita kumuunga mkono rais John Magufuli.

Hata Lowassa pia ameikacha Chadema na kurejea CCM.

Kutoshiriki kwa upinzani kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu kumeshindwa kutoa taswira ya namna gani wanakubalika na wananchi na hivyo 2020 ni ngumu kutabiri ushawishi wao.

Umoja wa upinzani

Nguvu ya upinzani kwa mwaka 2015 kwa kiasi kikubwa ilitokana na kuungana kwao kutengeneza Ukawa.

Kwa sasa sura na ushawishi wa vyama vilivyounda Ukawa imebadilika. Awali, washirika wenye nguvu zaidi walikuwa wawili- Chadema na CUF. Lakini magomvi ya ndani yamefanya CUF kugawanyika na uongozi uliopo kwa sasa wa CUF hauungwi mkono na Chadema.

Upande wa CUF ambao ulikuwa ukishirikiana na Chadema ulikuwa chini ya Maalim Seif Sharif Hamad ambao sasa umejiunga na chama cha ACT-Wazalendo ambacho si sehemu ya Ukawa.

Baada ya Maalim Seif kujiunga na ACT na wafuasi wake, chama hicho kinachoongozwa na Zitto Kabwe kimepata ushawishi mkubwa, hususani visiwani Zanzibar na kuwa sauti imara ndani ya upinzani kwa ujumla Tanzania.

Maelezo ya picha,

Maalim Seif na wafuasi wake wamehamia ACT mwakahuu na kukifanya chama hico kupata makali zaidi

Kutokana na mabadiliko hayo, ni jambo ambalo limekuwa likitazamiwa kutokea kwa Chadema na ACT kutengeneza umoja wao kuelekea uchaguzi.

Lakini hivi karibuni, jitihada hizo zimeingia doa, baada ya viongozi wa vyama hivyo kukosoana hadharani mitandaoni.

Sakata hilo lilianza baada ya Mbowe kuhudhuria sherehe za Uhuru wa Tanzania bara kwa mara ya kwanza toka Magufuli aingie madarakani na kufungua milango ya mazungumzo na maridhiano.

Hatua hiyo haikupokelewa vyema na Zitto ambaye ameikosoa katika mitandao yake ya kijamii.

Toka alipoingia madarakani, Magufuli amekuwa akilalamikiwa kwa kuminya upinzani. Vigogo kadhaa wamefunguliwa mashtaka na huku mikutano ya hadhara ya kisiasa kupigwa marufuku isipokuwa ya wabunge ama wawakilishi wa maeneo husika.

Endapo tofauti hizo hazitatatuliwa na wapinzani wasipokuwa na sauti moja, itakuwa rahisi zaidi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuuza sera na kukabiliana na upinzani uliogawanyika kwenye uchaguzi.

Demokrasia ya upinzani

Japo wapinzani wanahubiri demokrasia na kuikosoa serikali ya CCM kwa kukiuka demokrasia, wakosoaji wao wanavituhumu vyama hivyo ikiwemo Chadema kwa kukosa demokrasia ya ndani.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Fredrick Sumaye pia amejiondoa Chadema na kukituhumu chama hicho kwa kukosa demokrasia.

Sumaye pia alijiunga na Chadema akitokea CCM mwaka 2015 kama Lowassa, na akazunguka nchi nzima kuipigia kampeni Ukawa.

Maelezo ya video,

Sumaye: Chama cha Chadema hakina demokrasia.

Kiongozi huyo anadai amechezewa mchezo mchafu ndani ya Chadema baada ya kupigiwa kura za hapana kwenye nafasi ya kanda ya pwani baada ya kujitokeza "kuwania nafasi ya mwenyekiti wa chama taifa."

Ushindani wa kuwania uenyekiti wa chama hicho kabla ya hata mgogoro wa Sumaye pia ulizaa migogoro mkubwa baina ya Mbowe na wanasiasa wengine maarufu wa upinzani akiwemo Zitto.

Mwishowe Zitto alitimuliwa Chadema na kwenda kukiongoza chama cha ACT-Wazalendo ambacho, kwa kiasi kikubwa kilianzishwa na wanachama wa zamani wa Chadema ambao walikuwa wanamuunga mkono Zitto.

Hata hivyo 'kuminya' huko mabadiliko na nafasi za juu za uongozi na kushikiliwa na mtu mmoja kwa miaka mingi ni suala linalovikabili vyama vingi vya upinzani Tanzania.

Profesa Lipumba amekuwa Mwenyekiti wa CUF kwa zaidi ya miaka 20 sawa na John Cheyo wa UDP na Agostino Mrema wa TLP. Mpaka anajivua uanachama wa CUF mwaka huu, Maalim Seif alikuwa kwenye kiti cha Ukatibu Mkuu kwa zaidi ya miaka 20 pia.