Miaka 15 jela kwa kuchoma bendera ya wapenzi wa jinsia moja

Adolfo Martinez, 30, alikubali makosa yake baada ya kufanyiwa mahojiano na vyombo vya habari akiwa jela.

Chanzo cha picha, Police handout

Maelezo ya picha,

Adolfo Martinez, 30, alikubali kutekeleza uhalifu wakati wa mahojiano na vyombo vya habari akiwa jela

Jaji mmoja nchini Marekani amemuhukumu kifungo cha miaka 15 jela mwanamume aliyeiba bendera wa wapenzi wa jinsia moja kutoka kwa kanisa lao na kuichoma nje ya kilabu ya wasichana wanaocheza wakiwa uchi.

Adolfo Martinez, 30, alifanyiwa mahojiano na vyombo vya habari akiwa jela, na kukubali kwamba alichukua bendera hiyo kutoka kwa kanisa la Ames United Church of Christ kwa sababu chuki aliyo nayo dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.

Martinez alipatika na hatia mwezi uliopita, kwa makosa ya uhalifu unaosababishwa na chuki, unyanyasaji na utumiaji mbaya wa silaha pamoja na kurejelelea kutenda makosa.

Tukio hilo limetokea karibia usiku wa manane 11 Juni katika mji wa Ames, Iowa.

Polisi imesema uhalifu huo ulianza katika kilabu iliyopo Dangerous Curves, ambapo polisi waliitwa kwasababu mwanamume huyo alikuwa akitoa vitisho. Wakati wanawasili, tayari alikuwa ameondolewa na wahudumu wa baa hiyo.

Baada ya kuondoka kwenye kilabu hiyo, Martinez alikwenda moja kwa moja hadi katika kanisa wanakoabudu wapenzi hao wa jinsia moja na kushukisha bendera ya, kisha akarejea nayo hadi kwenye kilabu walichokuwa na kuichoma. Kama haitoshi, alitishia kuchoma baa hiyo pia.

Chanzo cha picha, Google Maps

Maelezo ya picha,

Kanisa la wapenzi wa Jinsia moja lililopo Iowa

Mwanamume huyo alikamatwa baadaye siku ile, na kufanya mahojiano na vyombo vya habari akiwa jela ambapo alikiri kutenda makosa hayo.

"Ilikuwa fahari yangu kufanya hivyo. Hizo ni baraka kutoka kwa Mungu," akasema, "nimefanya hivyo kwasababu ninapinga mapenzi ya jinsia moja".

"Kwa maneno rahisi, nimechoma kile walichokuwa wanajivunia," ameliambia shirika la televisheni la KCCI.

Mahojiano na vyombo vya habari akiwa jela, yamejumuishwa katika kesi kama ushahidi dhidi yake.

Mchungaji wa kanisa hilo Bi. Eileen Gebbie, ambaye alijitambua kama mpenzi wa jinsia wa moja, anasema, anakubali kwamba matendo ya Martinez yalishinikizwa na chuki.

"Mara nyingi mimi huona kwamba kanisa la Ames haliendani na jinsi watu wengine wanavyofikiria, na pia hapa kuna jamii kubwa ya watu wa jinsia moja," ameliambia gazeti la Des Moines Register baada ya Martinez,kukamatwa Mwezi Novemba.

"Lakini watu 12 ambao siwajui, na hawajawahi kuchangia kwa namna yoyote katika kanisa hili, wanasema kwamba mwanamume huyo alifanya makosa kwa kuwa mbaguzi na kuendeleza chuki."

Mwendesha mashtaka Jessica Reynolds amesema Martinez alikuwa mtu wa kwanza kushtakiwa kwa kutenda makosa ya uhalifu yanayosababishwa na chuki.

"Ukweli ni kwamba kuna watu ambao wanalenga wengine na kutenda uhalifu kwasababu ya ubaguzi, jinsia yao au hata kwa kuzingatia hisia zao za kijinsia," Jessica Reynolds ameliambia gazeti la Ames Tribune.

"Na hilo linapotokea, ni muhimu sana sisi kama jamii kuwa imara na kuhakikisha watu wanawajibishwa kwa matendo yao."

Pia unaweza Kusoma: