Mahakama yaamua kuwa ukahaba si uhalifu Nigeria

Je sheria inasemaje kuhusu biashara hii
Maelezo ya picha,

Kamatakamata ya makahaba limekuwa jambo la kawaida miongoni mwa maaifa mengi ya Afrika mashariki

Mahakama kuu jijini Abuja imetangaza kwamba ukahaba sio uhalifu nchini Nigeria.

Uamuzi huo umejiri katika kesi iliyokuwa inashirikisha wanawake 16 waliokamatwa kwa kufanya ukahaba.

Ni mara ya kwanza kwa mahakama ya Nigeria kuamuru kuhusu uhalali wa biashara hiyo ambayo inazidi kuonekana kuwa uhalifu mkubwa miongoni mwa mataifa mengi Afrika.

Jaji Binta Nyako wa mahakama kuu ya Abuja alisema kwamba hakuna sheria inayoharamisha ukahaba nchini humo.

Kesi hiyo iliowasilishwa 2017 ilifuatia kukamatwa kwa baadhi ya wanawake mjini Abuja kwa madai ya kushiriki katika biashara hiyo.

Licha ya serikali ya taifa hilo kudai kwamba wanawake hao ni wahalifu mahakama ilipinga hilo na badala yake kuagizia kwamba walipwe fidia.

Wakili mmoja aliyekuwa akiwawakilisha wanawake hao Babatunde Jacob aliambia BBC kwamba mahakama iliamuru kwamba vyombo vya usalama vilikiuka haki za wateja wake wakati walipovunja na kuingia katika nyumba zao na kudai kwamba wanawake hao walikuwa makahaba.

Wataalam wa sheria wanaamini kwamba uamuzi huo utakuwa na athari kubwa kwa taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Licha ya serikali ya taifa la Nigeria kudai kwamba wanawake hao ni wahalifu mahakama ilipinga hilo na badala yake kuagizia kwamba walipwe fidia.

Kukamatwa kwa makahaba na vyombo vya serikali ni kitu cha kawaida. Katika msako mmoja mnamo mwezi Mei mwaka huu, zaidi ya wanawake 60 walikamatwa mjini Abuja kwa kudaiwa kushiriki katika bishara hiyo.

Wanawake hao walidai kwamba , walinyanyaswa, kupokonywa fedha zao kwa nguvu na kuaibishwa hadharani.

Ethiopia yapanga mikakati ya kupiga marufuku ukahaba

Hivi karibuni maafisa katika mji mkuu wa Ethiopia Adis Ababa walitangaza kuwa wanapanga mkakati wa kupiga marufuku ukahaba na kuombaomba wa mitaani , ikiwa ni hatua ya hivi karibuni katika msururu wa hatua za kusafisha sura ya taifa.

Afisa habari wa Meya wa Mji wa Adis Ababa Feven Teshome, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba marufuku hiyo ni muhimu ili kupambana na "matatizo ya kijamii " katika mji huo wenye zaidi ya watu milioni moja.

Maelezo ya picha,

Mahakama nchini Kenya

Nchini Kenya makahaba wamekuwa wakisistiza biashara ya ukahaba ihalalishwe.

Makahaba wafanya maandamano wakitaka haki zao Kenya

Mwaka 2013 waliandamana kulalamikia kile wanachosema ni unyanyasaji wanaofanyiwa na polisi pamoja na askari wa baraza la jiji wakati wakiendesha biashara zao.

Walikusanyika katikati ya mji na kuelekea katika ofisi za baraza la jiji kuwasilisha malalamiko yao wakisema kuwa wamechoka kuhangaishwa na polisi na wanataka ulinzi.

Mwanaharakati wa maswala ya biashara ya ngono, John Mathenge aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji, alisema kuwa wengi wao wameuawa na kunyanyaswa hata na wateja wao pamoja na maafisa wa usalama.

Maelezo ya picha,

Mitaa ya mji wa Bugarama iliopo katika kati ya nchi tatu: Rwanda, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Burundi

Biashara ya ngono ni haramu nchini Kenya lakini baadhi ya watetezi wa makahaba wanasema kuwa katiba haijaeleza bayana ikiwa mtu atakayekamatwa akijihusisha na biashara hiyo achukuliwe hatua gani za kisheria.

Makahaba na watetezi waowanataka watu wakome kuwabagua wanaofanya biashara ya ngono, wakisisitiza ni kazi kama zilivyo nyingine.

Wengi walilalamika kuwa jamii imepuuza watu wanaofanya biashara ya ngono wala haiwatetei wakati wanaponyanyaswa au kuuawa .

Ripoti iliyotolewa mwaka jana kuhusu makahaba mjini Nairobi ilisema kuwa wanahangaiswa sana na askari wa baraza la jiji na kuwa wengi wao huachiliwa tu pindi wanapotoa rushwa.

Makahaba mjini Nairobi Kenya waliungana na wenzao duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga unyanyasaji dhidi yao.

Suala la kuzuwia kwa biashara ya ukahaba limekuwa na utata mkubwa miongoni mwa mataifa ya Kiafrika kutokana na madai kwamba wengi wanaojiingiza katika biashara hiyo wanadai kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha.

Wanadai wanauza miili yao ili kupata pesa za kujitunza na kuzitunza familia zao ambazo hazina uwezo wa kiuchumi.

Mataifa mengi ya Kiafrika hayana mpango kabambe wa kukabiliana na biashara hii, hali inayosababisha idadi ya wanawake na wanaume wanaoingia mitaani kujiuza kuongezeka kila uchao.