Kukamatwa kwa Tito Magoti: Polisi haijaweka wazi tuhuma dhidi ya mwanaharakati na wenzake

Titto Magoti

Chanzo cha picha, Titto Magoti/Instagram

Maelezo ya picha,

Tito Magoti alikamatwa Ijumaa asubuhi jijini Dar es Salaam na kuzuka taharuki kuwa ametekwa na watu wasiojulikana.

Polisi nchini Tanzania imekiri inamshikilia mwanaharakati Titto Magoti ambapo awali kulikuwa na wasiwasi kuwa ametekwa na watu wasiojulikana.

Magoti ambaye ni Afisa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania alikamtwa na watu waliovalia kiraia asubuhi ya leo.

Kamanda wa polisi jijini Dar es Salaam Lazaro Mambosasa ameithibitishia BBC kuwa wanamshikili Titto na wenzake wanne kwa "tuhuma za jinai".

Mambosasa hata hivyo hakueleza zaidi ni tuhuma zipi hizo akisema "kwa sasa uchunguzi unaendelea na tuhuma hizo hazijatajwa kwa sababu maalumu".

"Tunawashikilia wapo wanne, lakini Watanzania wasivyo wa kawaida wanamzungumzia mmoja tu," amesema Mambosasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Bi Anna Henga wali aliiambia BBC kuwa watu waliovalia kiraia kati ya wanne au watano walimvamia Magoti walimkamata kwa nguvu na kuingia nae kwenye gari kisha kutoweka naye kusikojulikana.

"...alikuwa ameenda Mwenge kununua simu, baada ya kushuka kwenye bodaboda tu alokuwa amepanda wakafika watu hao wasojulikana wakamchukua na kuondoka naye,"anaeleza Bi Henga.

Kijana wa bodaboda baada ya kushuhudia kadhia hiyo alirejea nyumbani kwa Magoti haraka na kuipasha habari familia yake ambayo pia iliwasha habari LHRC.

"Tayari tumeshaliripoti suala hili katika vituo kadhaa vya polisi jijini (Dar es Salaam) ambapo kote huko hayupo," Bi Henga awali aliiambia BBC.

BBC awali ilipowasiliana na Mambosasa alisema polisi hawakuwa na taarifa za 'kutekwa' na kuahidi kulifuatilia suala hilo.