Kukamatwa kwa Tito Magoti: LHRC yasema hakuna taarifa ya kituo kipi cha polisi ofisa wake anaposhikiliwa

Titto Magoti

Chanzo cha picha, Titto Magoti/Instagram

Maelezo ya picha,

Tito Magoti alikamatwa Ijumaa asubuhi jijini Dar es Salaam na kuzuka taharuki kuwa ametekwa na watu wasiojulikana.

Uongozi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania umesema mpaka sasa hauna taarifa ya kituo ambacho afisaa wake anashikiliwa na jeshi la polisi.

Magoti alikamatwa Ijumaa asubuhi jijini Dar es Salaam na watu ambao walikuwa wamevaa kiraia na kuzuka taharuki kuwa ametekwa na watu wasiojulikana.

Baadae jioni, Kamanda wa polisi wa Dar es Salaam Lazaro Mambosasa akathibitisha kuwa mwanaharakati huyo pamoja na wenzake watatu hawakutekwa na badala yake wamekamatwa.

Hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Bi Ana Henga amesema saa 24 baada ya Magoti kukamatwa bado hakuna taarifa ya wapi anashikiliwa.

"Pamoja na Polisi kusema wanaye #TitoMagoti kwa "Mahojiano na Uchunguzi" hawajatoa taarifa za kituo gani anafanyiwa mahojiano hayo na kwa kosa gani. Magoti na wenzake (kama wapo) wanayo haki ya kupata wanasheria kwa mujibu wa Sheria za Tanzania," Bi Henga amechapisha hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter.

BBC Ijumaa iliongea na Mambosasa hata hivyo hakueleza zaidi ni tuhuma zipi zinazomkabili Tito na wenzake na kusema "kwa sasa uchunguzi unaendelea na tuhuma hizo hazijatajwa kwa sababu maalumu".

Kwa mujibu wa Bi Henga, hata baada ya polisi kuthibitisha kumkamata Tito, walienda Kituo Kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam lakini hawakumkuta ofisa huyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Bi Anna Henga wali aliiambia BBC kuwa watu waliovalia kiraia kati ya wanne au watano walimvamia Magoti walimkamata kwa nguvu na kuingia nae kwenye gari kisha kutoweka naye kusikojulikana.

"...alikuwa ameenda Mwenge kununua simu, baada ya kushuka kwenye bodaboda tu alokuwa amepanda wakafika watu hao wasojulikana wakamchukua na kuondoka naye."

Kijana wa bodaboda baada ya kushuhudia kadhia hiyo alirejea nyumbani kwa Magoti haraka na kuipasha habari familia yake ambayo pia iliwasha habari LHRC.