Je India ndiyo chanzo kikuu cha vifusi vilivyoja katika anga za juu?

Vifusi vimeongezeka katika anga za juu katika miongo ya hivi karibuni

Chanzo cha picha, ESA

Maelezo ya picha,

Vifusi vimeongezeka katika anga za juu katika miongo ya hivi karibuni

Afisa wa ngazi ya juu zaidi wa kisiasa wa Pakistani ameushutumu mpango wa India wa safari za anga kwa kuwa chanzo cha vifusi katika anga za mbali.

Waziri wa Sayansi na Teknolojia Fawad Chaudhry ameiomba jamii ya kimataifa kufahamu kuwa India "inahusika " na uchafuzi wa anga za juu.

Vifusi vya anga za juu ni mamia ya vipande vilivyomeguka kutoka katika sehemu za roketi kuu kuu au kwenye setilaiti na vinachafua anga za juu-hususan katika uzio wa dunia (obiti).

Kauli za Bwana Chaudhry zimefuatia uvumbuzi uliofanywa na Shirika la anga za juu la Marekani, NASA, wa vifusi kutoka kwenye chombo cha anga za mbali cha India kilichoanguka kwenye Mwezi Septemba mwaka huu.

Lakini je madai hayo yalitokana na data? na je India kwa sasa ni chanzo cha uchafu unaoweza kuwa hatari katika anga za mbali?

Ni kiwango gani cha uchafu wa vifusi kulichopo katika anga za juu?

Kuna vipande zaidi ya 23,000 vya vifusi ambavyo ni vikubwa kuliko sentimita 10 (4 inchi) na Mtandao wa uchunguzi wa anga za juu wa Marekani uliona vifusi vingi miongoni mwake, kwa mujibu wa ofisi ya mpango wa NASA unaofuatilia shughuli za uzio(ODPO).

Vingi kati ya vifusi hivyo viko katika eneo la maili 1,250 kutoka kwenye uso wa dunia, pamoja na setilaiti gushi zaidi ya 2,000 pamoja na Kituo cha Kimataifa cha anga za juu.

Kuna uwezekano mkubwa wa mgongano kutokea na vingi kati ya vifusi vilivyopo sasa vinatokana na migongano hii katika anga za juu.

Wakati Uchina ilipofanya jaribio katika moja ya setilaiti zake za hali ya hewa mwaka 2007, vifusi vilivyokadiriwa kuwa 3,000 vilitengenezwa.

Na mgongano uliotokana na ajali ya setilaiti za mawasiliano za Marekani na Urusi mwaka 2009 pia iliongeza idadi ya vipande vikubwa vya vifusi katika obiti kwa mujibu wa ODPO.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

India imetangaza mpango kabambe wa safari za anga kwa siku za usoni.

India inahusika kwa kiasi gani?

India bado inazalisha uchafu wa anga za juu kwa kiwngo cha chini kuliko nchi tatu zenye kiwango cha juu cha uchafuzi wa mazingira ya anga za juu: Urusi, Marekani na Uchina kwa mujibu wa data za ODPO.

Vifusi vilivyotengenezwa na India, vinaongezeka- kutoka vipande 163 mwaka 2019 hadi 117 mwaka 2018.

Mwezi Machi mwaka huu, India ilikua ni nchi ya nne kufanya jaribio la kombora la kulipua setilaiti.

Ilisema kungekua na madhara kama kipande chake kingesalia duniani.

Lakini Marekani ililaani shambulio hilo na NASA ikasema iliona vipande vipatavyo 50 vilivyomeguka kutokana na jaribio hilo ikiwa ni zaidi ya mara tatu baada ya kufanyika.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

India ni nchi ya nne kufanya jaribio la kombora la kukabiliana na setilaiti

"Ikiwa vitendo vya Uchina, vya zaidi ya muongo uliopita vilikua ni vibaya zaidi India ambayo ilitengeneza vifusi zaidi hivi karibuni ingepaswa kujua kuwa inafanya kitu kinachomuathiri kila mmoja," Christopher D Johnson, mshauri wa sheria wa anga za mbali katika Wakfu wa uhifadhi wa mazingira ya anga za juu wenye makao yake nchini Marekani aliiambia BBC.

"Tunastahili kujifunza kutokana na matukio yaliyopita na kutambua kwamba hakuna haja yoyote ya kusababisha vifusi katika anga za juu ambavyo vinatishia kila mmoja kutumia anga ya mbali."

Je nini kinafanywa kutatua tatizo la vifusi katika anga ya juu?

Mzunguko wa dunia unaendelea kushuhudia maelfu ya setilaiti, huku nyengine nyingi zikiendelea kupangwa kurushwa na kuongeza uwezekano wa kugongana.

Lakini hakuna sheria yoyote inayopinga majaribio ya setilaiti.

Nchi kadhaa na makampuni ya kibinafsi yanafanya majaribio ya mbinu mpya, kupunguza athari za vifusi vya kwenye anga kuanzia chusa, sumaku kubwa hadi nyavu.

Mwaka 2025, Shirika la Anga za Juu la Ulaya litazindua setilaiti yake ya kwanza kuondoa vifusi kutoka kwenye mzunguko wa dunia.

Hata hivyo Shirika la Anga la Marekani NASA , limesema kwamba uondoaji wa vifusi hivyo kwenye anga bado ni changamoto kubwa "kiuchumi na kiufundi".

Pia Unaweza Kusoma: