Mashambulizi ya Kimtandao: Urusi yafanikiwa jaribio la 'kujitoa kwenye intaneti'

Vladimir Putin

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Jaribio hilo linatafsiriwa kama mpango wa serikali kuminya mawasiliano ya watu nchini Urusi

Serikali ya Urusi imefanikiwa kufanya majaribio ya mtandao uitwao Runet, ambao ni mbadala wa mtandao wa intaneti unaotumika hivi sasa duniani.

Maelezo kuhusu nini kilifanyika katika majaribio hayo hayakuwekwa wazi, ingawaje kulingana na Wizara ya Mawasiliano ya nchi hiyo, watumiaji wa kawaida hawakuona tofauti yoyote .

Na sasa matokeo haya yatapelekwa kwa rais Vladimir Putin.

Wataalamu bado wana wasiwasi kuhusu jinsi gani baadhi ya nchi wanaminya mawasiliano ya intaneti.

Mwanasayansi wa kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Surrey nchini Uingereza, Profesa Alan Woodward, amesema ''inahuzunisha kuona njia ya Urusi iliyoichukua ni muendelezo wa kuminya mtandao wa intaneti.''

''Kuna ongezeko kubwa la nchi zinazodhibiti nini raia wanaona, na kuangalia ni nini Irani na China wameshakifanya.''

Chanzo cha picha, Getty Images

''Inamaanisha watu hawatoweza kupata habari zinazoendelea nchini mwao, watakuwa kama wamewekwa ndani ya puto.''

Vyombo vya habari vya ndani, vimeripoti kuwa kaimu mkuu wa wizara ya mawasiliano akisema majaribio ya Runet yamefanikiwa kama yalivyopangwa.

"Matokeo ya zoezi kwa ujumla wake, yameonesha kuwa serikali na makampuni ya mawasiliano yapo tayari kujibu mapigo kutokana na hatari na vitisho vinavyojitokeza ili kuhakikisha kuwa intaneti na mitandao ya ndani ya Urusi inafanya kazi katika hali yoyote ile," amesema Alexey Sokolov.

Shirika la habari la taifa, Tass limeripoti kuwa majaribio yameonesha sehemu zenye mapngufu kwenye mifumo ya mawasiliano na vifaa. Pia imejaribu uwezo wa Runet kustahmili vishindo kutoka nje ya Urusi."

Je Runet inafanya kazi vipi?

"Lengo ni kufanya matumizi ya Intaneti ya Urusi yaungane na ya dunia kwa ujumla katika vituo maalumu ambavyo vitakuwa chini ya uangalizi wa serikali," amesema Profesa Woodward.

"Hali hiyo itawalazimu makampuni ya usambaza wa intaneti kufanya mipangilio maalumu ya usambazaji kwa nchi hiyo."

Kama ilivyo kwa China, Urusi pia inatarajiwa itatengeneza tovuti zake maarufu za ndani tu ili ziwe mbadala wa Google na Facebook katika siku za usoni, ameongeza Profesa huyo.

Kwa sasa nchi hiyo imetunga sheria ya kupiga marufuku uuzwaji wa simu janja ambazo hazina programu za kirusi.