Balozi wa Marekani aliyekosoa kufungwa kwa wapenzi wa jinsia moja aondoshwa Zambia

Daniel Foote, Balozi wa Marekani Zambia

Chanzo cha picha, United States Department of State

Maelezo ya picha,

Daniel Foote alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Zambia

Marekani imemuita balozi wake wa Zambia nyumbani huku mzozo wa kidiplomasia ukiendelea kati ya nchi hizo mbili baada ya Balozi huyo kukosoa vikali hatua ya Zambia ya kuwafunga jela wapenzi wa jinsia moja, vyanzo vya ubalozini vimesema.

Mwezi uliopita, Daniel Foote alisema kuwa ameshtushwa na uamuzi wa jaji wa kuwafunga wanaume hao kifungo cha miaka 15 gerezani baada kupatikana wakifanya mapenzi mwaka 2017.

Serikali ilimshtumu kwa kujaribu kushinikiza sera zitakazo fuatwa na Rais Edgar Lungu akamtaja kama miongoni mwa watu wasiotakikana katika taifa hilo.

Zambia inashikilia tamaduni zake linapokuja suala la vitendo vya mapenzi ya jinsia moja ambavyo ni kinyume cha sheria nchini humo.

"Huwezi kulazimisha serikali kufanya maamuzi fulani - 'kwasababu tu munatupa msaada, tunataka nyinyi mufanye hivi' - hilo haliwezekani," Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia Joseph Malanji aliiambia BBC.

Mwezi uliopita, Mahakama ya juu zaidi katika mji mkuu, Lusaka, ulimuhukumu Japhet Chataba na Steven Samba kifungo cha miaka 15 jela.

Wapenzi hao wa jinsia moja walikuwa wamekodi chumba cha kulala na mfanyakazi mmoja akachungulia kupitia dirisha lililokuwa wazi na kuwafumania wakifanya ngono, mahakama ilifahamishwa hivyo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais wa Zambia Edgar Lungu amemtaka Balozi wa Marekani kuondoka nchini humo

Katika taarifa iliyotolewa mapema mwezi huu, Bwana Foote amesema alikuwa akionyesha kutoridhishwa kwake na sheria iliyotumika na kifungo kilichotolewa, mtazamo ambao hakubaliana nao.

Pia alionya kuhusu uhusiano unaoendelea kuzorota kati ya nchi hizo mbili na kusema "Serikali ya Zambia inataka wanadiplomasia ambao wako tayari kusaidia lakini wafunge midomo yao".

Bwana Foote aliongeza kuwa msadaa wa mamilioni ya fedha umefujwa lakini hakuna ambaye ameshtakiwa kwa makosa ya rushwa.

Zambia ni moja ya nchi zinazopokea kiwango kikubwa cha msaada kutoka Marekani takribani $500m (£390m) kwa mwaka.

Vyanzo vya ubalozini vimethibitisha kwa vyombo vya habari vya eneo kwamba Bwana Foote ametakikana kurejea Marekani.

"Raisi Lungu amesema hataki kufanya kazi na mtu kama huyo na hivyo basi hakuna haja ya yeye kuendelea kuwa nchini humo," chanzo ambacho hakikubainishwa kimezungumza na Shirika la Habari la AFP

"Kumbuka kwamba kuna masuala ya ukosefu wa usalama na Marekani imemtaka balozi wake arejee. Hatutarajii mbadala wake hivi karibuni."

Bwana Foote amekuwa Balozi wa Marekani nchini Zambia tangu Desemba 2017.