Burkina Faso: Wanawake wengi wauawa katika shambulio la wanajihad

Ramani ya taifa la Burkina Faso ikionyesha mji wa Ouagadougou naArbinda

Wapiganaji nchini Burkina Fasso wamewaua raia 35, 31 wakiwa wanawake katika shambulio lililolenga kambi moja ya kijeshi na mji nchini Burikina Faso , maafisa wamesema.

Wanasema kwamba wanajeshi saba na wapiganaji 80 waliuawa baada ya jeshi kukabiliana na shambulio hilo la Jumanne katika mkoa wa Arbinda uliopo kaskazini mwa Soum.

Rais Roch Marc Christian Kabore alitangaza siku mbili za maombolezo ya kitaifa katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

Pia unaweza kusoma:

Hakuna kundi ambalo limekiri kutekeleza shambulio hilo kufikia sasa.

''Shambulio hilo ambalo sio la kawaida lilichukua saa kadhaa'', jeshi la Burkina Faso limesema.

Wakati walipokuwa wakitoroka wapiganaji hao waliwauwa raia 35 ikiwemo wanawake 31 na kuwajeruhi wengine sita, kulingana na msemaji wa serikali Remis Dandjiou ambaye alinukuliwa akisema na chombo cha habari cha AFP.

Mapema mwezi huu takriban watu 14 waliuawa baada ya wapiganaji kufyatua risasi ndani ya kanisa mashariki mwa taifa hilo. Mashambulio ya wanajihad yameongezeka nchini Burkina Faso tangu 2015.

Taifa hilo ambalo lilikuwa na amani limekumbwa na ghasia za kiwango cha juu kufuatia uvamizi wa mara kwa mara mbali na kusambaa kwa wapiganaji nchini Mali .

Mamia ya watu wameuawa mwaka huu huku mamilioni kati yao wakiwachwa bila makao.

Mgogoro huo ulienea hadi katika mpaka wa taifa jirani la Mali ambapo wapiganaji wa Kiislamu waliteka eneo la kaskaini mwa taifa hilo 2012 kabla ya wanajeshi wa Ufaransa kuwatimua.