Simulizi tano za kujitolea zilizoleta mabadiliko Afrika 2019

Peter Tabichi akibebwa juu juu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Peter Tabichi akibebwa juu juu

Watu mbalimbali duniani waliojitoa kuhakikisha maisha yao yanatia moyo wengine mwaka huu (2019) barani Afrika.

Tunaangazia tena simulizi ya mwalimu, mwanafunzi, wakili, kwaya na mwanaharakati ambao kwa namna moja au nyengine, maisha yao yamewatia moyo wengine katika mwaka 2019.

1. 'Vijana wana uwezo mkubwa'

Bruda Peter Tabichi

Maelezo ya video,

Mwalimu wa Sayansi nchini Kenya ashinda tuzo ya dunia ya mwalimu bora zaidi.

Akiwa amebebwa na wanafunzi wake, mwalimu Bruda Peter Tabichi alipewa makaribisho ya aina yake nchini Kenya aliporejea kutoka Dubai alipopata tuzo baada ya kutambulika kama mwalimu bora duniani.

Mwalimu Tabichi alipata ushindi huo mwezi Machi lakini nyuso za wanafunzi wake zilizokuwa zimejaa bashasha na kung'aa zilikuwa ushahidi tosha wa jinsi mwalimu Tabichi anavyokubalika nyumbani.

Mtawa wa kiume wa "Mtakatifu Francis" ambaye anafunza hisabati na fizikia, anatoa kiasi kikubwa cha mshahara wake kama msaada kwa watoto maskini katika shule moja ya upili kaunti ya Nakuru.

Tukiakisi mwaka ulivyokuwa, Mwalimu Tabichi aliiambia BBC kwamba tuzo hiyo ilionyesha wazi kwamba vijana wa Afrika wana uwezo mkubwa wa kubadilisha dunia kwa mtazamo chanya.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Peter Tabichi akiwa na wanafunzi na tuzo aliyotuzwa

Vilevie, ushindi wake umechochea watu wengi na kuonyesha kwamba walimu wanajukumu wanatekeleza jukumu muhimu katika kuleta mabadiliko yanayohitajika kwenye jamii kupitia elimu", akaongeza.

Tabichi pia anahamasisha wanafunzi hasa wasichana ili wavutiwe zaidi na masomo ya sayansi.

"Peter Tabichi ni mwalimu wa kipekee," mwanafunzi Teresia ameiambia BBC," na anastahili kutambuliwa na tuzo aliyopata".

2. Amekuwa mama na kuhitimu masomo yake kwa wakati mmoja

Almaz Derese

Chanzo cha picha, Almaz Derese

Maelezo ya picha,

Almaz Derese alijifungua Yididiya, hapa mtoto wake ana miezi mitatu, nusu saa kabla ya kufanya mtihami wa kitaifa

Hakuna kilichoonekana kupata ufumbuzi kwa Almaz Derese, 21, raia wa Ethiopia, wakati alipokuwa anatakikana kufanya mtihani wake wa mwisho wa shule ya upili.

Juni mwaka huu, alipata mtoto muda mfupi kabla ya kuanza kwa mtihani wa taifa. Alijifungua mtoto wa kiume, Yididiya, na dakika 30 baadaye akafanya mtihani huo akiwa hospitalini.

Chanzo cha picha, Ilu Abba Bor Zone communication office

Maelezo ya picha,

Almaz Derese talifanya mitahani mitatu akiwa hospitali ya Karl Mettu magharibi mwa Ethiopia

"Kwasababu nilikuwa naharakisha niwahi kufanya mtihani, sikuwa na changamoto nyingi wakati wa kujifungua," Almaz alizungumza na BBC Afaan Oromoowakati huo.

Mume wake Tadese Tulu, anasema alilazimika kushawishi mamlaka ya shule kumruhusu kufanya mtihani akiwa hospitalini.

Juni, Almaz alibaini kwamba amepita mtihani kwa asilimia 75.

Mama huyo anasema hakutarajia kupata matokeo mazuri kama hayo, kwasababu alikuwa na maumivu makali wakati anafanya mtihani na alikuwa amechoka kipindi ana ujauzito.

"Wakati nina mimba, sikuwa naweza kulala usiku, kwa hiyo nilitumia muda huo kusoma," aliiambia BBC.

Matokeo yake bora kulimaanisha kwamba anaweza kuendelea na masoyo ya sekondari ya juu kwa miaka miwili zaidi na hatimaye kutuma maombi ya kujiunga na chuo kikuu. Kwa sasa yuko mbioni kutimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi.

3. ''Namna ya kuleta mabadiliko'

Jordan Kinyera

Chanzo cha picha, Jordan Kinyera

Maelezo ya picha,

Jordan Kinyera alikuwa na umri wa miaka sita mzozo wa ardhi uliomkabili babake ulipoanza

Kujitolea kwake kusoma kulifanya mwaka 2019 mwaka mpya kwa wakili Jordan Kinyera wa Uganda.

Wakili hyo mwenye umri wa miaka 29 alipata hamasa ya kusomea uwakili baada ya babake kupoteza mali katika mzozo wa ardhi uliotokea mwaka 1996. Miaka 23 baadaye, mahakama ya juu ilitoa uamuzi wa mwisho na kuwapa familia hiyo ushindi.

"Babangu alikuwa amestaafu kwa hiyo hakuwa na mali nyingi,"Kinyera ameiambia BBC, Aprili, wakati anazungumzia kesi iliyodumu kwa muda mrefu.

"Alikuwa na amekosa matumaini na hakuna jambo baya kama kuonewa na uwe huna uwezo wa kufanya lolote. Hilo ndilo lililonitia moyo zaidi."

Kwa bahati mbaya, uamuzi huo ulitolewa wakati babake Kinyera alishaaga dunia. Babake aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 82 akiwa amepata tatizo la kupoteza akili na tulihitajika kumkumbusha kila wakati kwamba kila kitu kiko sawa", Kinyera aliiambia BBC.

Tangu Aprili, hakuna kubwa ambalo limebadilika kwasababu kuna mengi ambayo bado yanahitaji kufanywa, ikiwemo kupatanishwa na majirani ambao walikuwa wamezozana kwasababu ya umiliki wa ardhi hiyo, amesema, Kinyera.

Lakini muhimu zaidi ni kwamba, kwa sasa kilammoja amepata amani ya akili", ameongeza.

Wakili huyo ambaye bado ni kinda katika taaluma hiyo, anashauri wengine walio katika migogoro ya ardhi kama aliokumbana nao.

Simulizi ya kujitolea kwake na juhudi zake, zilisababisha gumzo kubwa katika ukurasa wa mtandao wa Facebook.

"Kijana huyu ni mfano mzuri wa vile tunavyoweza kuleta mabadiliko, hongera kwa kazi nzuri," Paul Watson alijibu.

4. 'Mabalozi wanaojivunia Afrika'

Kwaya ya vijana ya Ndlovu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kiongozi wa kwanya Ralf Schmitt na wanakwaya watatu kabla ya kufanya onesho kwenye kipindi maarufu cha America's Got Talent, Marekani

"Umekuwa mwaka wa shgughuli nyingi lakini wenye mafanikio tele," amesema kiongozi wa kwaya ya Ndlovu ya Afrika Kusini, Ralf Schmitt.

Mambo yalianza kuwa mengi pale kwaya moja ya vijana ya kijijini, ilipopewa fursa ya kushiriki katika kipindi maarufu duniani cha kwenye Televisheni cha America's Got Talent.

Waimbaji wa kwaya hiyo walifanikiwa kuingia fainali iliyofanyika Septemba mwaka huu na wakati huo, nchi nzima Afrika Kusini ilikuwa shabiki wake.

Kwaya hiyo ilikuwa inaimba nyimbo za Afrika - zilizokuwa zinapigwa na bandi ya Toto ya Marekani miaka ya 1980 - na kuacha majaji na watazamaji vinywa wazi.

"Usiku huu tulikuwa mabalozi vijana wanaojivunia Afrika iliyo na umoja," kwaya hiyo iliandika katika mtandao wa Twitter.

Ndlovu haikushinda shindano hilo lakini ilifanikiwa kutia saini makubaliano ya kurekodi muziki na Novemba, wakatoa CD yao ya kwanza, ambayo ilikuwa juu kwenye chati kwenye iTunes Afrika Kusini.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kwaya ya vijana ya Ndlovu wakifanya onesho

"America's Got Talent ilibadilisha kila kitu," Schmitt anaelezea. "Wamekuwa kielelezo chema shuleni, katika jamii na hata kwa mamilioni ya vijana Afrika Kusini."

5. 'Mimi ni mjumbe tu'

Alfred Brownell

Chanzo cha picha, Goldman Prize

Maelezo ya picha,

Alfred Brownell

"Mimi ni mjumbe tu - washindi wenyewe ni jamii," Alfred Brownell wakili na mwanaharakati wa Liberia aliiambia BBC mwezi Aprili baada ya kushinda tuzo maarufu ya mazingir

Brownell alitunukiwa tuzo hiyo ya mazingira kwa juhudi zake za kuzuia uharibifu wa mazingira kwa zaidi ya hekta 500,000 za msitu wa mvua nchini Liberia

Kwa ushirikiano na viongozi wa jamii husika, Brownell aliandika kuhusu uharibifu wa misitu na mashamba ya kilimo kusini mashariki na kampuni ya kuteneneza mafuta ya mawese ya Golden Veroleum Liberia (GVL).

Matokeo yake, bodi ya usanifishaji duniani na mjadala kuhusu uendelezaji wa mafuta ya mawese walipelekea kusitishwa kwa shughuli za kampuni hiyo na uharibifu wa misitu ukafikia mwisho.

"Sasa ni wakati kwa mashirika makubwa, makampuni ya utengenezaji wa mafuta ya mawese na wawekezaji kuwekeza katika jamii, kuwalinda na kuwawezesha," alizungumza hivyo katika kipindi cha BBC cha Newsday.

Shughuli za mwanaharakati huyu zilizua ghadhabu kwa serikali ya Liberia na baada ya kuzushiwa vurugu akapokea vitisho vya kuuawa jambo lililomfanya atoroke Liberia na kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Marekani.