Mogadishu: Bomu lililotegwa ndani ya gari lawaua watu76 Somalia

Walioshuhudia wanasema kwamba kulikuwa na watu wengi waliofariki

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Walioshuhudia wanasema kwamba kulikuwa na watu wengi waliofariki

Takriban watu73 wamedaiwa kufariki kufuatia mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari wakati wa pilka pilka nyingi katika mji mkuu wa Mogadishu nchini Somalia.

Mlipuko huo ulitokea katika kituo kimoja cha kukagua magari katika eneo la makutano ya barabara mjini Mogadishu.

''Mlipuko huo ulikuwa mbaya mno na naweza kuthibitisha kwamba zaidi ya raia 20 waliuawa , huku wengine wengi wakijeruhiwa'', afisa wa polisi Ibrahim Mohamed alinukuliwa na kituo cha habari cha AFP akisema.

Dkt Mohamed Yusuf, mkurugenzi wa hospitali ya Madina aliambia kitengo cha habari cha AP kwamba wamepokea miili 73 . Idadi ya watu waliofariki inatarajiwa

Hakuna kundi ambalo limekiri kutekekelza kitendo hicho lakiini wapiganaji wa kundi la al-Shabab wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara katika taifa hilo.

Mashahidi watatu waliambia Reuters kwamba mlipuko huo ulitokea karibu na kundi moja la wahandisi wa Uturuki ambao walikuwa wakijenga barabara.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Somalia Ahmed Awad alituma ujumbe wa twitter kwamba wahandisi hao wa Uturuki walifariki.

Wengi ya waliofariki ni wanafunzi waliokuwa na ari na juhudi wanaume kwa wanawake aliandika.

Uturuki imekuwa mfadhili mkuu wa Somali tangu kiangazi kilichokumba taifa hilo

Al-Shabab - kundi la wapiganaji , linaloshirikiana na kundi la kigaidi la Al-Qaeda limekuwa likitekeleza mashambulizi kwa zaidi ya miaka 10 . Lilifurushwa kutoka mji mkuu wa Mogadishu 2011 lakini linadhibiti maeneo ya taifa hilo.

Na punde baada ya mlipuko huo mitandao ya kijamii ilijaa habari kuhusu shambulio hilo.

Walioshuhudia walielezea kilichotokea katika eneo la mkasa huo..

''Kile ambacho niliweza kuona ni watu waliofariki...wakati wa mlipuko huo huku baadhi yao wakichomeka hali ya kutoweza kutambulika'', alisema Sakariye Abdulkadir, ambaye alikuwa karibu na mlipuko huo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Wengi walijeruhiwa katika mlipuko huo

Mbunge mmoja wa Somalia , Mohamed Abdirizak, amesema kuwa idadi ya watu waliofariki ni zaidi ya 90 , ijapkuwa habari hiyo aliyopata anasema kwamba haijathibitishwa.

Wengi ya waliouawa wanadaiwa kuwa wanafunzi wa chuo kikuu waliokuwa wakipita katika eneo hilo wakiabiri basi lao.

''Mungu awarehemu waathiriwa wa shambulio hili la kikatili'', aliongezea waziri huyo wa zamani wa usalama wa ndani.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmaajo alishutumu shambulio hilo.

''Adui huyu anafanyakazi ili kutimiza uharibifu wa ugaidi wa kimataifa, hawajafanyia lolote zuri taifa hili, hawajajenga hata barabara moja, hospitali na vituo vyovyote vya elimu'' , alinukuliwa akisema na kitengo cha habari cha Somalia SONNA.

''Kile wanachofanya ni uharibifu na mauaji na raia wa Somalia wana habari zote kuhusu vitendo vyao''.

Watu watano waliuawa mwezi huu wakati wapiganaji wa Alshabab waliposhambulia hoteli moja ya Mogadishu inayopendwa sana na wanasiasa, wanadiplomasia na wanajeshi.