Faru Fausta: Faru mzee zaidi duniani afariki Tanzania

Fausta

Faru Fausta, ambaye anaaminika kuwa ndiye faru mzee zaidi duniani amefariki akiwa na miaka 57 nchini Tanzania, mamlaka zimethibitisha.

Fausta ameishi maisha yake yote katika Hifadhi ya Ngorongoro mpaka umauti ulipomkuta jana Ijumaa, Disemba 27, mhifadhi mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) Dkt Freddy Manongi ameiambia BBC.

"Huyu ndiye alikuwa faru mzee zaidi duniani, hiyo ni historia kwa Tanzania... tunahisi kifo chake ni cha kawaida kutokana na umri wake mkubwa. Madaktari wapo njiani watatueleza hasa sababu ya kifo chake baada ya kufanya vipimo," ameeleza Manongi.

Faru huyo jike alikuwa chini ya uangalizi maalumu kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita baada ya afya yake kudhoofu na kuanza kushambuliwa na wanyama wakali mwituni.

"Wanyama wakali hususani fisi walianza kumshambulia na akapata vidonda vikubwa sana. Ilipofika mwaka 2016 ilibidi tumtoe porini na kumuweka kwenye uangalizi maalumu. Vidonda vyake vilipona lakini afya yake bado ilikuwa dhoofu hatukuweza kumrejesha porini."

Mwaka 2017 kulizuka gumzo kubwa mpaka Bungeni nchini Tanzania juu ya gharama za matibabu na uhifadhi wa faru huyo baada ya kuwekwa kwenye uangalizi maalumu.

Maelezo ya video,

Fausta: Faru mzee zaidi duniani anayeishi Tanzania

"Suala la gharama ya matunzo wala halikuwa hoja kubwa, kwa mwaka mmoja toka Septemba 2017 alitumia milioni 16.2. Hauwezi kumuweka katika mazingira maalumu bila kutumia gharama...Lakini Hifadhi ya Ngorongoro inaingiza mapato yake kutokana na hawa hawa wanyama, mwaka jana pekee tumeingiza shilingi bilioni 143, lazima tuwatunze hawa wanyama," amesema Dkt Manongi.

Faru Fausta licha ya umri wake mkubwa hakuwahi kuzaa na hiyo inaelezwa kuwa huenda ikawa ni moja ya sababu ya kuishi kwake kwa muda mrefu.

Faru wanakadiriwa kuweza kufikisha umri wa miaka 37 mpaka 43 wakiwa porini na huweza kufikisha mpaka miaka 50 wakifugwa katika maeneo maalumu. Faru mweusi mwengine wa mwituni ambaye alifahamika kwa umri wake mkubwa ni Solio, jike liliokuwa likiishi Kenya na kufa likiwa na miaka 42 mwaka 2016.

Maelezo ya video,

Hatma ya kizazi cha faru weupe wa kaskazini ni ipi?

Wanyama hao wamekuwa wakiwindwa kwa kasi na wawindaji haramu ulimwenguni kutokana na thamani ya pembe zao. Kwa sasa inakadiriwa kuwa na faru weusi 5,500 pekee duniani kote.

Nchini Tanzania wanyama hao wanakadiriwa kuwa 200. Katika Hifadhi ya Ngorongoro kulikuwa na faru 108 mwaka 1968, idadi hiyo ikaporomoka mpaka 25 mwaka 1977 na hali ikawa mbaya zaidi mwishoni mwa miaka ya 80 ambapo walikuwa chini ya 10. Kwa sasa hifadhi hiyo ina faru zaidi ya 50.

"Juhudi kubwa na za makusudi za uhifadhi na kupambana na ujangili zimefanyika karika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Kwa sasa hali inaendelea vizuri, hata siku ambayo Fausta anakufa, kuna faru mwengine alikuwa amezaa," amesema Dkt Manongi.