Urusi yazindua kombora la Avangard lenye kasi mara 12 zaidi ya sauti na 'lisiloweza kuzuiwa'

Picha ya kombora la Avangard

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Picha ya wizara ya ulinzi nchini Urusi inaonyesha kichwa cha kombora la Avangard

Kombora la kwanza lenye teknolojia ya kisasa la Avangard Hypersonic limeanza kufanya kazi, wizara ya ulinzi ya taifa hilo imesema.

Hawakusema ni wapi kombora hilo lilifanyiwa majaribio lakini maafisa awali walikuwa wamesema kwamba litarushwa katika milima ya Urals.

Rais Vladimir Putin amesema kuwa kombora hilo lenye uwezo wa kinyuklia lina kasi ya mara 20 ya sauti na linaiweka Urusi mbele ya mataifa mengine.

Lina "mfumo wa glide" ambao unarahisisha usafiri wake na linaweza kuwa vigumu kujilinda dhidi yake

Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu alithibitisha kombora la "Avangard hypersonic glide liliianza kufanyakazi saa 10:00 za Moscow tarehe 27 Disemba", na kuliita "tukio muhimu".

Bwana Putin alisema Jumanne mfumo wa Avangard unaweza kupenya mifumo ya ulinzi ya makombora ya kisasa na ile ya baadaye, na kuongeza: "Hakuna hata nchi moja inayomiliki silaha kama hiyo mbali na ile ya masafa marefu inayoweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine."

Mataifa ya Magharibi na mataifa mengine yalikuwa "yakicheza nasi", alisema.

Bwana Putin alizindua silaha hiyo ya Avangard na mifumo mingine ya silaha katika hotuba yake ya kitaifa mnamo mwezi Machi 2018.

Mnamo mwezi Disemba 2018, silaha hiyo iligonga lengo la mazoezi ya umbali wa kilomita 6,000 (maili 3,700) katika uzinduzi wa jaribio lililofanyika katika kambi ya makombora kusini mwa milima ya Urals.

Silaha hiyo haiwezi kutunguliwa na mfumo wowote wa ulinzi wa adui, alisema bwana Putin bada ya jaribio hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Putin atazama huku jeshi la Urusi likifanyia majaribio kombora la Avangard Disemba 2018

Likiwa juu ya kombora la masafa marefu linaloweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine , silaha ya Avangard inaweza kubeba silaha ya kinyuklia ilio na uzani wa hadi megatani mbili.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imetoa video ya mfumo wa Avangard, lakini wataalam wa silaha wameelezea kutilia shaka ufanisi wake.

Katika taarifa, Pentagon ilisema "haitapinga madai ya Urusi" juu ya uwezo wa Avangard. Marekani ina mpango wake wa kombora la mfumo wa Hypersonic, kama ilivyo China, ambayo mnamo 2014 ilisema ilifanya majaribio ya silaha kama hiyo.

Mnamo mwezi Novemba tarehe 26 Urusi iliruhusu wataalam wa Marekani kukagua kombora hilo la Avangard chini ya sheria za makubaliano mapya ya 2010, azimio linalolenga kupunguza idadi ya silaha za kimkakati za kinyuklia .

Makubaliano hayo ambayo yataisha mnamo februari 2021, ni makubaliano makubwa ya mwisho ya kudhibiti silaha za nyuklia kati ya Urusi na Marekani.

Mnamo Agosti mwaka huu, Marekani ilijitoa katika Mkataba wa Vikosi vya Nyuklia (INF), ambao ulitiwa saini na Rais wa Marekani Ronald Reagan na kiongozi wa Soviet Mikhail Gorbachev mnamo 1987.

Rais wa Marekani, Donald Trump alisema kwamba anataka mkataba mpya wa kinyuklia kutiwa saini na Urusi pamoja na Uchina.

Uchanganuzi wa Jonathan Marcus

Ni vigumu kubaini iwapo mfumo mpya wa kombora la Urusi la Avangard umeanza kufanya kazi, kama inavyodaiwa na Moscow, au ni majaribio yake tu.

Lakini hamu ya Rais Putin kutaka kujivunia kwa kiwango fulani inahesabiwa kuwa haki yake. Urusi inaonekana kupiga hatua kubwa katika ujenzi wa makombora hayo ya kisasa. . China pia inaendeleza mifumo kama hiiyo wakati Marekani inaonekana kusalia nyuma kidogo.

Makombora ya mhemko, kama linavyomaanisha jina lake huruka kwa haraka sana, yaani lina kasi ya angalau mara tano ya ile ya sauti.

Yanaweza kuwa makombora ya aina ya cruise, yanayowezeshwa wakati wote wa urushaji wake. Au, yanaweza kubebwa juu ya kombora la masafa marefu ambalo hujitawanya na kuendelea kuelekea katika lengo lake kwa kasi ya juu.

Sio kasi ya silaha hiyo ya kisasa inayoifanya kuwa imara zaidi bali pia jinsi inavyotawanya upepo wakati inaposafiri ikielekea katika lengo lake.

Hii inaleta tatizo kubwa kwa mifumo ya ulinzi ya makombora iliopo.

Kwa hivyo, ikiwa madai ya Urusi ni ya kweli, huenda imeanzisha mfumo wa kombora la masafa marefu linaloweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine ambalo litakuwa vigumu kujilinda dhidi yake

Tangazo kwamba kombora hilo la Avangard limeanza kufanya kazi linazua enzi mpya na hatari katika ushindani wa kutengenza silaha za kinyuklia

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Onyesho la silaha ya Avangard jinsi linavyoweza kupenya

Inathibitisha kwa mara nyingine mtazamo wa Rais Putin juu ya kusisitiza na kurasimisha silaha za nyuklia za Urusi. Ni ishara ya kurudi kwa ushindani wa kiuwezo.

Wachambuzi wengine wanaweza kuona ni mpango wa muda mrefu wa Urusi kukabiliana na mikakati ya kudumu ya Washington ya utengenezaji wa mifumo ya kujilinda dhidi ya makombora .

Hoja ya Marekani kwamba hiyo ni mipango yake ya kujilinda na makombora dhidi ya mataifa yasioaminika kama vile Iran, Korea Kaskazini imepuuziliwa mbali na Urusi.

Yote haya yanajiri wakati ambapo mtandao mzima wa makubaliano ya kudhibiti silaha kutoka kwa vita baridi yanaporomoka .

Mkataba mmoja muhimu - Mkataba mpya wa Start - unatarajiwa kumalizika mnamo Februari 2021. Urusi inaonekana kuwa tayari kuongeza makubaliano lakini utawala wa Trump hadi sasa umeonekana kutilia shaka .

Pamoja na kizazi kipya cha silaha za nyuklia, wengi wanaamini sio tu kwamba mikataba iliyopo inapaswa kusitishwa, lakini mikataba mipya inahitajika kusimamia kinachoweza kugeuka kuwa ushindani mpya wa silaha za nyuklia.