Kwanini Marekani imemuwekea vikwazo makamu wa rais wa Sudani Kusini?
- Wanyama Chebusiri
- BBC

Taban Deng Gai
Serikali ya Marekani imetangaza vikwazo vya kifedha dhidi ya makamu wa rais wa kwanza wa Sudani Kusini, Taban Deng Gai.
Utawala wa rais Donald Trump unadai kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, kwamba hatua hiyo ya kumwekea vikwazo bwana Taban Deng ni kuhusika kwake katika ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
Makamu huyo wa rais pia anashtumiwa kwa kutoweka na kuwaua raia wa Sudani Kusini.
Mauaji ya wanaharakati
Taarifa hiyo kutoka Washington pia ilidai kwamba makamu huyo wa rais wa kwanza alipanga na kuongoza kutoweka na kuuawa kwa wakili wa kutetea haki za kibinadamu Samuel Dong Luak na mjumbe wa chama cha upinzani cha SPLM-1O Aggrey Idris.
Deng anadaiwa kuongoza mauaji ya wanaharakati hao wawili ili kuhujumu ushawishi wa kiongozi wa upinzani Riek Machar, na hivyo basi kuimarisha na kuhifadhi wadhifa wake wa makamu wa rais wa kwanza katika serikali ya rais Salva Kiir.
Inaaminika pia kwamba Deng alitaka wawili hao kuuawa ili kuzua hofu na kutuma ujumbe kwa wanachana wa SPLM-1O kwamba hawako salama hata wakiwa nje ya Sudani Kusini na kwamba kile wanachostahili kufanya ni kumuunga mkono.
Luak na Idris, walikuwa wakosoaji wa serikali ya Sudan Kusini na walitoweka mjini Nairobi mnamo Januari 23 na 24 mwaka wa 2017.
Makundi ya kutetea haki za raia pamoja na jamaa walitoa tetesi kwamba wawili hao walitekwa nyara na maafisa wa usalama wa Kenya kutokana na agizo kutoka kwa serikali ya Sudan Kusini na kusafirishwa hadi mjini Juba.
Hata hivyo, serikali ya Juba kila mara imekuwa ikikanusha kuhusika na kutoweka kwa wanaharakati hao.
Hujuma dhidi ya amani
Marekani pia inasema kwamba makamu huyo wa rais wa kwanza amekuwa kizingiti kikubwa katika juhudi za mazungmzo ya amani ya Sudan Kusini kati ya rais Kiir na kiongozi wa upinzani Riek Machar.
Inadaiwa kwamba Deng amekuwa mstari wa mbele kusababisha mgawanyiko na kupanda mbegu za kutoaminiana ndani ya chama tawala cha Sudan People's Liberation Movement, kile cha SPLM-1O na katika kabila la Nuer.
Hatua ambayo Washington inadai imesababisha kulemazwa kwa juhudi za mazungmzo ya amani na maridhiano, na kuhujumu utekelezwaji wa mkataba wa amani na hivyo basi kuendeleza mzozo wa umwakigaji damu wa wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Salva Kiir na Riek Machar waliposaini makubaliano ya amani
Mkataba wa amani
Mnamo Septemba 2018, rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa upinzani Riek Machar waliafikiana upya kuhusu mkataba wa amani ambao ulipendekeza kuundwa kwa serikali ya muungano mwezi Mei 12, 2019.
Viongozi hao wawili waliahirisha pendekezo hilo mara mbili, kuahirishwa kwa hivi karibuni kukifanyika Novemba mwaka jana.
Hata hivyo, tangu wakati huo, juhudi mahususi za kiusalama zimefanywa ili kutoa ishara ya utekelezwaji wa mkataba huo wa amani.
Hali hii imesababisha mateso na mauaji ya raia ambapo umoja wa mataifa unasema kwamba zaidi ya watu elfu hamsini wamefurushwa katika makazi yao kutokana na vurugu.
Marekani sasa inaonya kwamba haitasita kuwalenga wale wanaoendeleza mzozo, na pia itaendelea kutoa shinikizo kwa viongozi ili kuchukuwa hatua madhubuti za kuleta amani na uthabiti nchini Sudan Kusini.
Vikwazo vya kifedha
Kwa mujibu wa naibu wa waziri wa fedha wa Marekani Justin Muzinich, sasa pesa zilizoko kwenye akaunti na mali yote ya makamu huyo wa rais wa Sudan kusini iliyoko nchini Marekani zimezuliwa.
Pia, Deng haruhusiwi kufanya biashara yoyote na kampuni za Marekani na washirika wake, ikiwa ni pamoja na benki za kimataifa zilizoko Marekani.
Mwezi jana, Washington pia iliwawekea vikwazo vya kifedha mawaziri wawili wa Sudan Kusini kwa madai kwamba walihujumu mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka wa 2018.