Je, wajua Oman imewahi kutawaliwa kutoka Zanzibar?

Qaboos alikuwa ni kizazi cha sita kutoka kwa Seyyid Said ambaye aliifanya Zanzibar kuwa kitovu cha dola ya Oman.
Image caption Qaboos alikuwa ni kizazi cha sita kutoka kwa Seyyid Said ambaye aliifanya Zanzibar kuwa kitovu cha dola ya Oman.

Mwaka 1832, Sultani wa Oman Said al-Said alihamisha makao makuu yake kutoka Muscat, Oman mpaka visiwani Zanzibar.

Huo haukuwa mwanzo wa muingiliano baina ya Oman na Afrika Mashariki bali muendelezo wa mahusiano ambayo mpaka sasa yanaendelea.

Tangu kutokea kwa kifo cha aliyekuwa Sutani wa Oman Qaboos al-Said siku ya Ijumaa, watu mbali mbali Afrika Mashariki kwa kupitia majukwaa mbalimbali, kuanzia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii(hususani WhatsApp) mpaka mitandaoni wamekuwa wakizungumzia kifo hicho na mahusiano ya baina ya Oman na ukanda huo.

Qaboos ni kizazi cha sita (moja kwa moja) kutoka kwa Seyyid Said ambaye aliifanya Zanzibar kuwa kitovu cha dola ya Oman.

Na hata sultani aliye madarakani kwa sasa Harith al-Said pia ni kizazi cha sita kutoka Seyyid Said.

Kuhamia Zanzibar

Lakini hata kabla ya makao makuu ya Oman kuhamia Zanzibar tayari kulikuwa na muingiliano baina ya nchi hiyo na Afrika Mashariki.

Vikosi vya wanamaji wa Oman ndivyo vilivyoongoza mashambulizi ambayo yalimaliza miongo ya utawala wa kireno katika pwani ya Afrika Mashariki.

Kutoka mwaka 1696, vikosi vilivyotumwa na Imamu wa Oman Saif bin Sultani viliizingira Ngome ya Yesu (Fort Jesus) kisiwani Mombasa kwa miaka miwili mpaka vikosi vya Ureno viliposalimu amri 1698.

Kwa mujibu wa mwanahistoria kutoka Mombasa Kenya, Stambuli Abdillahi Nassir ameiambia BBC kuwa mahusiano hayo yalikuwa ya makubaliano baina ya pande mbili (watu wa pwani ya Afrika Mashariki na watawala wa Oman).

"Wazee wetu wa kale wa hapa (Mombasa) wakishirikiana na ndugu zetu wengine kutoka (kisiwa cha) Pemba na kwenda kuomba msaada kwake (Sultani) baada ya kuteswa kwa miaka 200 mfululizo na utawala wa Wareno ambao waliuwa mababu zetu na kuchinja watawala...baada ya hapo ikaingiwa mikataba ambayo ilimruhusu Sultani kutawala kwa niaba ya wananchi wa eneo."

Haki miliki ya picha SOPA Images
Image caption Ushawishi wa Oman kwa Afrika Mashariki ulianza baada ya kuwafurusha Wareno kwenye Ngome ya Yesu, Mombasa mwaka 1698.

Baada ya Mombasa, majeshi hayo ya Oman yaliwafurusha Wareno Zanzibar na Kilwa na kisha miji yote hiyo kuwekwa chini ya magavana ambao baadhi yao walijitangazia utawala wao.

Mwaka 1806, Seyyid Said aliingia madarakani Oman, mwaka 1828 akaitwaa Ngome ya Yesu na baada ya miaka minne akahamia rasmi Zanzibar, kwa kipindi chote hicho wafanya biashara na wakuliwa walowezi kutoka Omani waliingia pwani ya Afrika Mashariki.

Sultani huyo pia alihamasisha kilimo cha karafuu, zao kuu la bishara la Zanzibar mpaka leo.

Dola ya Oman ikawa na ushawishi pwani yote ya Afrika Mashariki, na kuingia ndani bara kutokea lango la Bagamoyo, Tabora Ujiji Kigoma, Rwanda Burundi Uganda mpaka mashariki ya Congo.

Kote huko wafanyabiashara wa Kiomani walikwenda kusaka vipusa, pembe za ndovu pamoja na watumwa.

Moja ya wafanyabiashara maarufu katika historia alikuwa Hamad bin Muhammad el Murjebi, maarufu kwa jina la Tippu Tip aliyezaliwa Zanzibar 1832 na kufariki 1905.

Baadhi yao walilowea na mpaka hii leo bado vizazi vyao vingalipo kote.

Zanzibar 'kutengana' na Oman

Sultan Seyyid Said aliaga dunia mwaka 1856 kisiwani Ushelisheli akiwa katika moja ya safari zake baina ya Zanzibar na Oman.

Baada ya kifo chake, watoto zake wakashindwa kuendeleza umoja wa kidola baina ya Oman na Zanzibar. Kutokana na mzozo huo mtot wake wa kiume wa tatu Thuwaini akarithi usultani kwa upande wa Oman na mtoto wake wa kiume wa sita Majid akarithi usultani kwa upande wa Zanzibar.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Masultani wa Zanzibar wenye asili ya Oman ndio walioujenga Mji Mkongwe ambao sasa unahifadiwa kama urithi wa dunia chini ya Unesco.

Kwa wakati huo, Zanzibar ilikuwa tajiri kuliko Oman na Sultan Majid alitakiwa kuilipa fidia kila mwaka Oman japo alifanya hivyo kwa miaka michache ya awali.

Vizazi vya familia ya al-Said ama Busaidi viliendelea kuitawala Zanzibar mpaka yalipofanyika mapinduzi ya mwaka 1964, Sultani wa mwisho wakiwa ni Jamshid bin Abdullah al-Said.

Kwa miaka 56 sasa Sultani huyo wa zamani anaishi uhamishoni nchini Uingereza.

Kufuatia mapinduzi, maelfu ya Waarabu walikimbia visiwa vya Zanzibar na kurudi katika nchi yao ya asili Oman.

Kwa upande wa Oman, watawala wa kisultani bado wanatoka kwenye familia hiyo.

Kwa upande wa Qaboos, anasifika baada ya kumpindua baba yake madarakani mwaka 1970 kwa kufungua milangowote kutoka Afrika Mashariki ambao wana asili ya Oman kurudi na kupata uraia wa nchi hiyo.

Miaka 50 ya Qaboos madarakani pia imeitoa Oman kutoka umasikini wa kutupwa mpaka utajiri kwa kutumia vyema rasilimali ya mafuta.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa zamani wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Sultan Qaboos

Si ajabu kusikia kiswahili kikiongelewa katika mitaa ya jiji la Muscat kutokana na utajiri huo wa mwingiliano baina ya pande mbili.

Mwandishi wa zamani wa BBC kutokea Zanzibar ambaye sasa ni mbunge nchini Tanzania anaeleza kuwa pameshakuwa mpaka na mawaziri watano wa serikali ya Oman kwa mkupuoa ambao wamezaliwa Zanzibar ama wazazi wao walizaliwa Zanzibar.

Mwaka 2017, Waziri wa Mafuta wa Oman, Dkt Mohammed Al Rumhy aliongoza ujumbe maalum kutoka Sultan kutembelea Kenya na Tanzania.

Dkt Rumhy ni mzaliwa wa Zanzibar na kote Kenya, Zanzibar na Tanzania Bara alikuwa akiongea Kiswahili fasaha, ambao hawajui uhusiano wa pande hizi mbili walionekana kustaajabu.

Mada zinazohusiana