Uwekezaji wa Mo ndani ya Simba upo mashakani?

Dewji Haki miliki ya picha AFP/GETTY IMAGES
Image caption Mo Dewji

Mwekezaji na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Simba Mo Dewji, ametoa kauli mbili ndani ya saa chache huihusu klabu hiyo ambayo zimezaa maswali lukuki.

Awalia kupitia mitandao yake ya kijamii jana usiku (Januari 13) alichapisha kauli ambayo ilitafsiriwa kama inaashiri kurudi nyuma kwenye nguvu yake ndani ya klabu.

Lakini leo amesema kuwa kilichotokea kwenye akaunti zake hapo jana baada ya mchezo kati ya Simba na Mtibwa ni cha 'bahati mbaya' na kuwa wameelekeza nguvu yao kwenye kujipanga kwa ajili ya ligi wakiwa na nguvu.

Mo ameandika leo kwenye ukurasa wake wa Twitter baada ya hapo jana kuandika kuwa anajiuzulu nafasi yake ya uenyekiti wa bodi muda mfupi baada ya Simba kupoteza fainali ya kombe la mapinduzi dhidi ya Mtibwa kwa kufungwa 1-0.

Hapo jana Dewji katika kurasa zake mbalimbali za kijamii alinukuliwa akitaja masikitiko yake ya kuwekeza fedha nyingi ikiwa ni zaidi ya bilioni nne za kitanzania huku matokeo yakiwa tofauti. Hata hivyo kauli yake ya jana ameifuta kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Baadhi ya mashabiki wa klabu ya Simba pia mbunge Ridhiwan Kikwete walimtaka Dewji kufikiria mara mbili uamuzi wake huo.

''Ninaheshimu sana maamuzi ya mtu lakini kaka sina hakika kama kafanya busara katika hili. Hela hazinunui ushindi, ni haki yao kulipwa kwa kazi wanayoifanya. Tafadhali kaka usifanye hasira. Huu ni mpira tu na matokeo yako matatu. Ninaamini utafikiria tena uliloamua.'' Ameandika Ridhwan.

Naye mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam ambaye ni mshabiki aliyetopea wa Simba ameandika.

''Matokeo ya mpira huleta furaha na huzuni kwa wanaofungwa. Natoa pole kwa timu yangu ya Simba pamoja na mashabiki wote na wanaoitakia mema Simba. Sina uhakika na kinachoendelea kwenye akaunti ya Mo kama ni yeye mwenyewe ameandika. Ninawaomba wana simba tutulie ukweli tutaupata muda si mrefu. Tusisahau kuwa wapo watu pia wabaya hutumia mwanya huu kuvuruga amani na utulivu wa timu zetu. Simba nguvu moja.''

Mo Dewji amekua mwanachama, mfadhili na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Simba kwa kipindi kirefu huku klabu hiyo ikitajwa kufanya vizuri ndani na nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni kwa kile kinachotajwa ni kutokana na uongozi wake.

Baadhi ya wachambuzi wa soka wanasema uamuzi huu ni wa haraka mno na unaweza kuwa na athari kubwa kwa Simba na kwa Mo Dewji mwenyewe.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii