Makubaliano hayo yanaathiri vipi biashara ya dunia

Liu He na Donald Trump Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Liu He na Donald Trump

Marekani na China wamesaini makubaliano yanayolenga kumaliza vita vya kibiashara ambavyo vimeathiri masoko na uchumi wa dunia.

Akizungumza mjini Washington, Rais Trump amesema makubaliano hayo ni mapinduzi makubwa kwa uchumi wa Marekani.

Viongozi wa China wametaja makubaliano hiyo kama ushindi kwa pande zote mbili ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

China imeahidi kuongeza bidhaa zinazouzwa Marekani kwa bilioni 200 za Marekani ikiwa ni ongezeko la mwaka 2017 na kuimarisha sheria za haki miliki.

Aidha, Marekani imekubali kupunguza kwa asilimia 50 kodi mpya dhidi ya bidhaa za China zinazoingizwa Marekani.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wajumbe wakuu wa mazungumzo Robert Lighthizer ba Liu He

Makubaliano yanahusisha nini?

  • China imejitolea kuongeza bidhaa zinazoingizwa Marekani kwa angalau bilioni 200 za marekani kiwango cha juu zaidi ya mwaka 2017, kuimarisha manunuzi ya bidhaa za kilimo kwa bilioni 32 za marekani, uzalishaji kwa bilioni 78 za marekani, nishati kwa bilioni 52 za marekani na huduma kwa bilioni 38 za marekani.
  • China imekubali kuchukua hatua zaidi dhidi ya bidhaa ghushi na kufanya iwe rahisi kwa makampuni kuchukua hatua za kisheria dhidi ya uchukuaji kisiri taarifa muhimu za kibiashara.
  • Marekani itadumisha asilimia 25 ya kodi kwa bidha zinazoingizwa kutoka China zenye thamani ya bilioni 360; China ambayo imeweka kodi mpya kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya bilioni 100 pia inatarajiwa kuendeleza kiwango kikubwa cha kodi zao.

Uchambuzi wa mwanauchumi Dharshini David

Makamu rais wa China Liu He, ambaye alitia saini makubaliano kwa niaba ya China, amesema makubaliano hayo yalitokana "usawa na kuheshimiana kwa pande zote mbili" na kutetea mfumo wa kiuchumi wa nchi yake wakati wa hotuba yake.

"China ina mfumo wa kisiasa na wa kiuchumi ambao unaendana na maslahi ya taifa," amesema.

"Hii haimaanishi kwamba China na Marekani haziwezi kushirikiana. Badala yake, nchi hizi mbili zinashirikishana maslahi mengi ya kibiashara."

"Ni matumaini yetu kwamba pande zote mbili zitashirikiana na kutimiza waliokubaliana na kudumisha makubaliano kwa dhati."

Makubaliano hayo yamesifiwa na Ikulu ya Marekani na kuchukuliwa kama mwanzo wa kumalizika kwa vita vya kibiashara ambapo Rais Trump alisema ni kwa ajili ya kulinda kazi za wa Marekani na makampuni kutokana na kile anachokitathmini kama ushindani usiyo wa haki wa kibiashara.

Silaha ya machaguo upendayo: mabilioni ya madola kwa kodi, au ada za ziada kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje. Na hilo limekuwa msumari moto kwa wafanyakazi hao hao ambao walikuwa wanalindwa, kwa nchi zote mbili.

Kwa yote yaliyokuwa yanafurahiwa - na uwepo usio wa kawaida wa rais kusaini mkataba wa pande mbili - haya yako kimakubaliano zaidi ya ushindi - huku kiwango kidogo tu cha kodi kikifanyiwa marekebisho na maridhiano kidogo yakifikiwa na pande zote mbili. Kodi bado zimesalia kwa karibia thuluthi mbili ya bidhaa ambazo Marekani inanunua kutoka kwa China.

Aidha, malalamishi ya msingi ya Marekani kuhusu tabia za China - kuanzia mtazamo wake, utoaji wa ruzuku za kibiashara hadi wizi wa kimtandao bado hakijapata ufumbuzi.

Na shabaha ya Trump ya kutaka kuandika tena sheria za kibiashara ulimwenguni ambako bado hakijafikiwa, wengine wanahofia kwamba huenda baada ya China, nguvu yake akaielekeza Ulaya - wakati ambapo Uingereza inatafuta kufikia makubaliano ya Brexit yenye manufaa na kulinda maslahi yake.

Je uhusiano wa kibiashara wa China na Marekani kwa Afrika ukoje?

Marekani imekuwa ikipoteza ushawishi barani Afrika- lakini mwanadiplomasia wa juu wa nchi hiyo barani Afrika anataka kubadili hali hiyo.

''Kwa muda mrefu wakati wawekezaji walipokuwa wakibisha milango na waafrika wakifungua, mtu pekee aliyekuwa hapo ni mchina,'' Tibor Nagy, mjumbe wa maswala ya Afrika wa Marekani aliwahi kuiiambia BBC.

Marekani imekuwa chanzo kikubwa cha uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika, lakini mchango wake umekuwa ukipungua.

''Nafikiri ni kwa sababu ushindani kutoka kwa nchi nyingine umeongezeka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita,'' amesema bi Benabdallah.

Katika utawala wake, Rais Trump Trump ameripotiwa kueleza mataifa ya kiafrika kuwa ni ''nchi chafu'' na kuongelea Afrika kama sehemu ambayo marafiki zake wanakwenda kujaribu kutajirika.

China nayo, mwaka 2018, ilitangaza uwekezaji wa thamani ya dola za kimarekani bilioni 60 kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Lina Benabdallah, mtaalamu wa mahusiano ya China na Afrika katika chuo cha Wake Forest aliwahi kusema kuwa biashara kati ya Marekani na mataifa ya Afrika imeshuka kwa sababu ya ongezeko la uhitaji si tu China, lakini nchi nyingine kama vile Urusi na Uturuki.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mfanyakazi wa kampuni ya China akitathmini uzalishaji

Makampuni ya ujenzi ya China yamechangia maendeleo makubwa katika miundo mbinu iliyosahaulika kwa muda mrefu, zikiwemo barabara, katika baadhi ya mataifa ya Afrika.

Lakini Marekani imekuwa ikiishtumu China kwamba inahimiza mataifa ya Afrika kuitegemea, na ilitumia mikataba ya kifisadi na kuhatarisha rasilmali asili za mataifa ya Afrika.

Pia imewahi kuutaja uwekezaji wa China kwa Afrika kama wenye uwezo wa kuimarisha miundo mbinu Afrika lakini unoongeza madeni na uliounda nafasi kidogo za ajira.

Chimbuko la vita vya Marekani na China ni khaja ya utawala wa Trump kuwa na uwiano katika sera yake ya kigeni, na ambayo inaishi kwa kauli ya Marekani kwanza, ambaye pia imetikisa uhusiano wa Marekani na mataifa ya Afrika.

Marekani ina kibarua kigumu cha kurejesha mahusiano na bara la Afrika ikiwa inataka kujihusisha na nchi za uchumi unaochipukia wakati ambapo ukuaji wa uchumi wa China, bila shaka kutakuwa na athari za kibiashara na uwekezaji barani Afrika.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii