Tanzania: Huenda mamilioni ya watu wakafungiwa laini zao juma lijalo

Makao makuu ya TCRA

Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) imetoa wito kwa Watanzania waliokamilisha usajili wa laini zao kuhakiki upya.

Katika taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, mkurugenzi mkuu wa TCRA, James Kilaba amesema mchakato huo unapaswa kufanyika kabla ya simu ambazo hazijasajiliwa kuzimwa Januari 20, 2020.

Kumekuwa na hofu kuwa mamilioni ya watu wanaomiliki simu za mkononi nchini Tanzania huenda wakakosa mawasiliano ya simu kutokana na kufungwa kwa laini zao za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole.

Mwananchi mmoja mjini Dodoma Haruna Mkupe anasema ''Nimefuatilia namba yangu kwa NIDA tangu mwezi wa tano mpaka sasa sijapata namba yangu, tunapata taabu kwa sababu pia ya umbali wa ofisi za NIDA''

Doris anasema amechelewa kujiandikisha kwa sababu ya pilika nyingi za maisha: ''Nilichukua fomu nimejaza nimekuja kukamilisha usajili wa NIDA, nilikuwa nikiishi nje ya mkoa wa Dodoma, dakika za majeruhi hizi.''

Haki miliki ya picha Eagan Salla
Image caption Usajili kwa alama za vidole

Muongozo huo wa kuhakiki unasemaje?

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na TCRA:

  • Kila aliye na laini ya simu anastahili kuhakiki kwa kupiga simu kwenda *106#
  • Muda wa mwisho wa Januari 20, 2020 unawahusu wale ambao wana laini za simu lakini hawakutumia kitambulisho cha taifa(Nida) na kuthibitishwa kwa alama ya vidole.
  • Watakaokasitishiwa huduma za simu Januari 20 wanaweza kuendelea na utaratibu wa usajili ili waweze kurudisha laini zao.
  • Wale wanaonunua upya laini za simu wanaweza kuzisajili wakati wowote kwa kutumia stakabadhi zinazohitajika
  • Wanadiplomasia ambao hawajakamilisha usajili wa laini zao za simu zinazotumika katika vifaa vyao vya mawasiliano wanatakiwa kuendelea na utaratibu waliopewa.

Zikiwa zimesalia siku nne pekee kabla ya tamati ya zoezi hilo, mamia ya watu wamejitokeza katika vituo mbalimbali vya mamlaka za vitambulisho vya taifa NIDA kwa ajili ya kupata namba zao ambazo ni kigezo katika kukamilisha zoezi la usajili kwa alama za vidole.

Huwezi kusikiliza tena
Mamilioni ya watu huenda wasiwe na mawasiliano juma lijalo

Afisa mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA Semu Mwakyanjala ameiambia BBC kuwa mpaka tarehe 12 mwezi Januari mwaka huu idadi ya waliojisajili kwa alama za vidole ni milioni 26 na laki moja sawa na asilimia 53.8.

''Wakati tunasajili laini lazima tujue lengo ni nini, kwa kuwa watu milioni 24 wako kwenye mifumo ya kibenki kwa njia ya mtandao wa simu hivyo kwa masuala ya usalama ni muhimu kukamilisha zoezi hili kwa kuwa serikali imeamua kuboresha mifumo na kuboresha usalama wa mtumiaji wa simu''.

Haki miliki ya picha Eagan Salla
Image caption Nembo ya Mamlaka ya vitambulisho vya taifa NIDA

Kumekuwa na hali ya kunyoosheana vidole, raia wakiilaumu mamlaka ya vitambulisho vya taifa NIDA na mamlaka hiyo pia ikieleza kuwa watumiaji wa simu hawazingatii matangazo yanayotolewa na mamlaka kuhusu usajili kwa alama za vidole.

Kwa sasa, karibu ofisi zote za Nida hujaa wananchi wanaosaka vitambulisho hivyo ambavyo vimegeuka kuwa nyaraka muhimu na moja ya vigezo katika zoezi la usajili wa laini za simu kwa njia ya alama za vidole, pia kwa mahitaji mbalimbali ya huduma nchini Tanzania.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii