Corona: Maafisa wameonya 'huenda vikazaana na kusambaa mbali zaidi'

Mamlaka ya afya imethibitisha kuwa maambukizi ya ugonjwa huo ni kupitia kwa binadamu

Chanzo cha picha, Kevin Frayer

Maelezo ya picha,

Mamlaka ya afya imethibitisha kuwa maambukizi ya ugonjwa huo ni kupitia kwa binadamu

Virusi vipya vya Corona huenda vikazaana na kusambaa katika maeneo ya mbali, maafisa wa afya wa China wameonya, huku wakiongeza juhudi za kudhibiti maambukizi.

Idadi ya waliofariki kutokana na ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo imeongezeka na kufikia tisa huku visa vingine 440 vikithibitishwa, walisema.

Afisa wa tume ya kitaifa ya afya amekiri kuwa nchi hiyo kwa sasa iko "katika awamu muhimu" ya kuzuia na kudhibiti kusambaa kwake.

Siku ya Jumanne , mamlaka ilithibitisha usambazaji wa virusi hivyo kupitia binadamu.

Katika taarifa ya kwanza kwa umma tangu mwanzo wa mlipuko wa ugonjwa huo, naibu waziri wa tume ya afya ya China, Li Bin alisema kuna ushahidi kuwa ugonjwa huo "unasambazwa kupitia mirija ya kutoa pumzi".

Lakini China haijafanikiwa kubaini chanzo halisi cha virusi hivyo.

"Japo mfumo wa maambukizi haujaeleweka, kuna uwezekano virusi hivi vinaweza kuzaana na hatari ya kusambaa," alisema Bw. Li.

Onyo hilo linakuja wakati mamilioni ya watu kote nchini China wakisafiri kutoka eneo moja hadi lingine kuadhimisha mwaka mpya wa China

Maelfu ya wengine wanasafiri nje ya nchi.

Kenya pia iko hatarini

Wizara ya afya nchini Kenya imeimarisha uangalizi katika bandari zake zote za kuingia na kufanya na kupima abiria kuona kama wana virusi vya corona, ambavyo mpaka sasa watu takribani 400 wana maambukizi na watu 9 wamepoteza maisha nchini China.

Kenya imekuwa ikipokea wageni wengi kutoka China.

Kenya ni moja kati ya nchi iliyo hatarini kukumbwa na virusi vya Corona kutokana na mahusiano ya kibiashara na China. Kila wiki, shirika la ndege la Kenya hupeleka ndege zake mbili kati ya jiji la Nairobi na Guangzhou.

Mamlaka za China zimewataka watu kutosafiri ndani na nje ya mji wa Wuhan, mji virusi hivi vilipoanzia kisha kusambaa katika majimbo kadhaa ya China, pia nchini Marekani, Thailand na Korea Kusini.

WHO inatazama kama mlipuko huu unaweza kuwekwa kwenye kundi la dharura ya kiafya kimataifa.