Virusi vya Corona: Wanafunzi kutoka Tanzania waeleza namna walivyokwama Wuhan

Khamis Bakari Haki miliki ya picha Khamis Bakari

"Mji wa Wuhan ni kama umevamiwa na zimwi, hali sio nzuri kwa kweli. Hakuna mtu ambaye anaonekana akitembea barabarani, kupo kimya kabisa,"anaeleza Mtanzania Dkt Khamis Hassan Bakari ambaye yupo jijini Wuhan, China.

Jiji la Wuhan ni kitovu cha mlipuko wa virusi vya Corona, ambapo mpaka sasa watu 81 wamefariki.

Dkt Bakari ni mwanafunzi wa taasisi ya Tongji, chuo ambacho kiko Wuhan na kinahusika na utafiti wa magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

"Maisha yamebadilika sana kwa sababu kwa sasa haturuhusiwi kabisa kutoka nje na kuna baadhi ya vyuo wanafunzi hawaruhusiwi hata kushuka ngazi kutoka ghorofa moja kwenda nyingine, yani kama uko ghorofa la tano hupaswi kuonekana ghorofa la nne."

Aliongeza kuwa kuna utaratibu maalum katika baadhi vyuo ambapo wanaletewa chakula mpaka nje ya mlango.Lakini kwa upande wa chuo anachosoma anasema kuwa kuna muda maalum katika chuo chao ambapo duka kubwa(super market) hufunguliwa , "nilijaribu kwenda leo nikageuza kwa sababu nilikuta watu wengi sana".

Jumuiya ya wanafunzi nchini China inasema kuwa wanawasiliana na ubalozi wa Tanzania uliopo Beijing kwa kila kinachoendelea.

Dkt. Khamis anasema kuwa kuna watanzania 420 kwa sasa, huku wengine takribani 200 wakiwa wamerejea Tanzania kwa likizo kabla ya mlipuko wa virusi hivyo kutokea.

Haki miliki ya picha Khassim

"Kwenye vyuo vyote wameweka walinzi na hairuhusiwi kabisa mtu kutoka nje ya geti la chuo. Tunawasiliana kwa simu tu hata na majirani hatuonani.

Wanafunzi wengi wanataka kurudi nyumbani, "kundi moja la watanzania walikusanyika wengi juzi na wakanipigia simu wakitaka kurudi nyumbani, lakini changamoto ni usafiri, hakuna namna ya kutoka hapa tulipo".

Anasema kuwa China imeweka katazo hilo ili kuzuia mlipuko huo kuwa janga la kimataifa.

"Na sababu kuu ni kuwa wagonjwa wa virusi hivi wengine huwa wanapitiliza muda wa wiki mbili, wengine zinafika hata nne hivyo kama tutaweza kurudishwa nyumbani basi inabidi tutengwe eneo maalum kwa muda wa wiki nne."

Haki miliki ya picha Jafar
Image caption Maduka makubwa ya chakula yanafunguliwa kwa muda wa saa nane au chini ya hapo

Hilal Kizwi ni Mtanzania mwengine aliyepo jijini Wuhan, yeye pia ni mwanafunzi wa utabibu.

Kwa mujibu wa Kizwi kwa takribani siku nne wako kwenye taharuki na wapo kwenye zuio la kutoka nje na kutakiwa kuvaa mavazi ya kujikinga.

"Hali ilivyo sasa kupata mahitaji muhimu ni changamoto, naona kuna kipindi tutahitaji kutoka tu nje.

"Leo siku ya nne sijatoka nje, mimi ni mwanafunzi wa taaluma ya afya na hivyo nilipopata taarifa niliweza kujiandaa kwa vyakula kidogo, lakini karibu vinaisha."

Wanafunzi hao wanasema kuwa inawalazimu kula mlo mmoja kwa siku.

Haki miliki ya picha Hillal
Image caption Wanafunzi wa Tanzania wanahofia kuishiwa na chakula

Mamlaka husika zinajitahidi sana kupambana na hii hali licha ya kwamba kipindi hiki watu wengi wamesafiri tayari kwenda miji mingine wakati mlipuko ulikuwa umetokea tayari.

"Baadhi ya vyuo wameweka utaratibu wa kuwasaidia kuwapelekea wanafunzi mahitaji yao muhimu, licha ya kwamba kuna katazo lakini watu wenyewe tumekuwa waoga kutoka nje".

Kwa ujumla kuna utaratibu ambao umewekwa kwa sasa kwa kuweka muda wa maduka makubwa maalum kufunguliwa na gari ndogo za kukodishwa (taxi) 6000 zimetengwa ili watu watumie kwenda kujinunulia mahitaji maalum.

Haki miliki ya picha Hillal

Aidha ameeleza kuwa amekuwa akiwatoa hofu familia yake nyumbani, kwa sababu mara nyingi wanashuhudia takwimu kwenye mitandao hivyo wanakuwa na hofu.

Pia ameeleza kuwa vyuo vingi vimeongeza muda wa likizo kutokana na hali ilivyo kwa sasa na hata wale waliopo Tanzania wameshindwa kurudi mpaka hapo watakapotangaza vinginevyo.

"Nyumbani tunawasiliana mara kwa mara, wanatuombea na tunaongea mara kwa mara" .

Haki miliki ya picha Hillal

Jaffar Rajab pia yupo masomoni jijini Wuhan na anaeleza juu ya kuongezeka kwa wasiwasi kila siku mpya inavyoingia.

"Tunafuata maelekezo ya wataalamu, pale tunapotoka nje mara moja moja sana mfano kama tunajikinga kwa kuvaa mavazi ya kujifunika, kunawa mikono kwa maji yanayotiririka. Tunajaribu kuwafahamisha watanzania wenzetu namna ya kujikinga na kuzingatia kile ambacho shirika la afya limetangaza tufanye. Ni saa 36, au siku mbili sasa sijatoka nje niko ndani tu," Hillal ameeleza.

Haki miliki ya picha Jafar
Image caption Mji wa Wuhan kwa sasa ni kama 'umekimbiwa'

Kwa upande wa ubalozi wa Tanzania uliopo China unasema kuwa watu wamewekwa karantini na hakuna mtu anayeweza kuingia au kutoka katika mji wa Wuhan.

Makamu wa balozi wa China Tanzania, Bwana Said Masoro ameieleza BBC kuwa wanawasiliana na umoja wa wanafunzi wa Kitanzania Wuhan lakini hakuna namna ya kuwafikia kwa sasa.

"Tatizo lililopo sasa si la wageni peke yake bali hata wenyeji wenyewe... Tunafahamu kuna ambao wangependa kurudi nyumbani lakini kuna utaratibu maalumu umewekwa na mamlaka za China ili kuzuia maambukizo zaidi," amesema Masoro.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii