Human Rights Watch yadai Tanzania 'inaminya' haki za afya za wapenzi wa jinsia moja

  • Sammy Awami
  • BBC Swahili, Dar es Salaam
Wapenzi wa jinsia moja
Maelezo ya picha,

Human Rights Watch ladai Tanzania 'inaminya' haki za afya za wapenzi wa jinsia moja

Shirika la kutetea haki za binaadamu la kimataifa Human Rights Watch limeishutumu serikali ya Tanzania kwa kutekeleza sera za afya zinazowanyima huduma za kutosha watu wanaovutiwa kimapenzi na watu wa jinsia moja, LGBT.

Shirika hilo limeongeza pia kwamba wengi wa watu katika kundi la wapenzi wa jinsia moja wamekuwa wakikosa kupata huduma na haki za msingi za kisheria na haki zingine za binadamu.

Katika ripoti yake yenye kurasa takribani 114 iitwayo "Tusipopata huduma tutakufa': Kuandamwa kwa LGBT na Kunyimwa Haki ya Afya Tanzania", Human Rights Watch wamekusanya ushahidi unaoelezea namna gani haki za wana-LGBT zimekuwa zikikiukwa - kama vile kunyimwa huduma za afya, ukamatwaji wa kiholela na vipimo vya kulazimishwa vya njia ya haja kubwa

"Mamlaka nchini Tanzania zimekuwa zikitekeleza mashambulizi dhidi ya haki za wana-LGBT, ikiwa ni pamoja na kuwanyima haki yao ya afya. Vitisho vya kukera kama kile kinachosemekana kuwa ni 'kutangaza ushoga' vimesababisha kuondolewa kwa huduma bora zilizo na ushahidi wa ufanisi katika kuongoza sera ya VVU nchini Tanzania," amesema Neela Ghoshal, mtafiti mwanadamizi wa haki za wana-LGBT katika shirika la Human Rights Watch.

Miaka mine iliyopita, serikali ya Tanzania kupitia wizara ya afya ilipiga marufuku mashirika ya kiraia kusambaza vilaini bure kwa wanaume wanaovutiwa kimapenzi na wanaume kama sehemu ya jitihada za kupambana na maambukizi ya VVU/UKIMWI.

Pia unaweza kusoma:

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Shirika la haki za kibinadamu la Human Rights Watch linasema kwamba wapenzi wa jinsia moja wananyimwa haki zao za kimsingi nchini Tanzania

Wataalamu wa afya waliukosoa uamuzi huo na kuonya kwamba unaweza kusababisha ongezeko kubwa la maambukizi ya VVU, hasa kwa makundi yaliyo hatarini.

Hata hivyo wizara ya afya imeendelea kusisitiza kwamba hospitali na vituo vingine vya afya vya serikali vinatoa huduma za afya bila ubaguzi wa aina yoyote ile, hivyo hakuna sababu ya kuwa na huduma maalum zinazowalenga wana-LGBT zinazotolewa na asasi za kiraia.

Serikali ya Tanzania haijajibu shutuma hizi mpya.

Hata hivyo huko nyuma, iliwahi kukanusha shutuma zozote za kubagua wananchi wake kwa misingi ya mrengo wa kimapenzi ama kijinsia.

Ilisema pia kwamba inaheshimu na itaendelea kufanya hivyo hivyo katika kulinda haki zote za binadamu nchini.

Nchini Tanzania, vitendo penzi wengi wa jinsia moja kuishi kwa hofu na kuficha mrengo wao wa kimapenzi